07 December 2010

SAKATA LA UMEME

*Mafundi TANESCO waamriwa kukesha
*Kazi hiyo kukamilika ndani ya siku nane
*Transifoma ya Chalinze kuziba pengo Dar


Na Grace Michael
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Bw. David Jairo amemtaka mkandarasi na wataalamu wa TANESCO wanaoshughulikia uwekaji wa transfoma jipya katika Kituo cha Kupooza Umeme cha Kipawa, Dar es Salaam kufanya kazi hiyo usiku na mchana ili
imalizike haraka na kupunguza mgawo wa umeme.

Kutokana na amri hiyo ya kufanya kazi usiku na mchana,  siku nane zitatumika katika kumaliza kazi hiyo ili transfoma hiyo ambayo imeazimwa kwenye mradi mwingine wa umeme iweze kuwashwa na kupunguza makali ya mgawo uliopo kwa sasa.

Transifoma hiyo iliyochukuliwa Chalinze, mkoani Pwani ilikuwa mojawapo kati ya nne zilizokuwa zimepangwa kwa ajili ya mradi wa kuboresha umeme katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwamo Pwani, Tanga, Shinyanga na Mwanza.

Tayari suala la mgawo wa umeme limeibua taharuki katika jamii, huku mbunge wa Kigoma Kusini, Bw. David Kafulila akipanga kuwasilisha hoja binafsi ya kutokuwa na imani na Waziri wa Nishati na Madini, Bw. William Ngeleja kwa kushindwa kwake kumaliza tatizo la umeme ndani ya uongozi wake.

Kwa mujibu wa mbunge huyo, tangu mwaka 2006 serikali imeshindwa kupunguza tatizo hilo na viongozi wakuu wa serikali na hasa Waziri wa Nishati na Madini mara kadhaa wamekuwa akipotosha Watanzania kuwa serikali inalishughulikia lakini siku hadi siku sekta ya umeme imevuka upeo wa viongozi kiasi cha kauli zao kupoteza imani kwa Watanzania.

Hali hiyo ambayo imeikumba karibu mikoa yote nchini, imekuja ikiwa ni siku chache baada ya Waziri Ngeleja kuingia madarakani kwa mbwembwe huku akiapa kumaliza kabisa tatizo la mgawo huo nchini.

Akizungumza na mafundi hao jana, Bw. Jairo aliwataka kufanya kazi hiyo kwa umakini na haraka kwa kuwa tatizo la umeme lina athari kubwa za kiuchumi lakini pia linasababisha kero kubwa kwa wananchi.Hili ni janga la kiuchumi hivyo kinachotakiwa ni kufanya kazi usiku na mchana ili kuondokana na hili tatizo, alisema Bw. Jairo.

Alisema kuwa kuharibika kwa transfoma hiyo ambayo ilikuwa inazalisha megawati 36 za umeme imesababisha kuongeza makali ya mgawo, na ikifungwa mpya itazalisha megawati 44 kutasaidia kupunguza makali hayo.

“Mgawo huu mbali ya kuharibika kwa baadhi ya mitambo lakini umechangiwa na hali ya hewa kama kutokuwepo kwa maji ya kutosha na katika kukabiliana na hili, serikali inachukua hatua mbalimbali za kumaliza tatizo hilo,” alisema Bw. Jairo.

Akielezea walivyojipanga katika kufanya hiyo kazi, Meneja Mwandamizi Udhibiti Mifumo na Njia Kuu za Umeme Bw. Abudullah Fereshi alisema kwa kufanya kazi kwa saa 24 kila siku itawezekana kumaliza kwa huo muda wa siku nane.

Akizungumzia transfoma hiyo, alisema kuwa imechukuliwa kutoka kwenye mradi mwingine wa kuboresha umeme ili kukabiliana na tatizo hili la mgawo wa umeme. Kutokana na hali hiyo, aliwataka wananchi kuwa na matarajio ya kupungua kwa mgawo wa umeme mara baada ya kuwashwa kwa transfoma hilo.

1 comment:

  1. TUNAWAPONGEZA TANESCO PAMOJA NA WIZARA KWA BIDII MNAYOIONYESHA,INGAWA NI WAJIBU WENU LAKINI TUNAWATAKIA KILLA LA KHERI NA PIA ISIWE KILA MARA TATIZO HILI LIKITOKEA IWE KAMA ZIMA MOTO TUWE NA MIKAKATI YA MUDA MREFU NA YA KUDUMU MAANA HATA WAWEKEZAJI WANASHINDWA KUJA KWA WINGI KWA TATIZO LA UMEME,NA TUNA GESI NYINGI SANA KULE SONGOSONGO,MAANA KUNA KISIMA KINGINE HATA KUGUSWA KUTUMIA BADO.TUONDOKANE NA HABARI YA MAJI KUKAUKA MAJI YAWE NI YA KILIMO NA KUNYWA TU.TUJIPANGE VIZURI NA PIA NI BORA KUWAPA WAWEKEZAJI WA UMEME KATIKA BAADHI YA MIKOA IWE YA USHINDANI,TANESCO PEKE YAO HAWAWEZI KUENEZA UMEME NCHI NZIMA.MAANA KILA KUKICHA WANAHANGIKIA MATENGENEZO MBELA HAWAENDI!! NA NCHI NI KUBWA HII

    ReplyDelete