07 December 2010

Wilaya ya 'Mnali' yashika mkia tena

Na Livinus Feruzi, Bukoba

WILAYA ya Bukoba mkoani Kagera ambayo mwaka jana baadhi ya walimu wake walichapwa viboko kwa matokeo mabaya imeendelea kushika nafasi ya mwisho kwa mwaka nne mfululizo, katika matokeo ya mtihani ya darasa la saba katika mkoa huo.Kwa miaka mitatu iliyopita
halmashauri ya wilaya hiyo imekuwa ikishika nafasi ya mwisho katika matokeo ya mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi, na mwaka huu imeendelea kushika nafasi hiyo.

Februari mwaka jana aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Albert Mnali alikosa uvumilivu wa kufeli kila mwaka, akamwamuru askari mmoja awacharaze viboko baadhi ya walimu ambao shule zao zilikuwa zimefanya vibaya, hatua ambayo ilisababisha kibarua cha mkuu huyo kuota mbawa.

Ofisa Elimu Taaluma Mkoa wa Kagera, Bw. Renatus Bamporiki alisema katika matokeo ya mwaka jana wilaya hiyo ilipata ushindi kwa asilimia 33 na mwaka huu imefikia asilimia 50.4 lakini bado ikashika mkia.

Hata hivyo, alisema kuwa kiwango cha elimu katika mkoa kwa ujumla kimepanda kwa asilimia tano, kutoka asilimia 55 mwaka 2009 hadi 60.1%, huku wilaya ya Ngara ikiongoza kwa wilaya zote za mkoa huu.

Kwa mujibu wa Bw. Bamporiki, watoto waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani kwa mkoa wa Kagera ni 29,385, sawa na asilimi 60.1 ya wanafunzi 49,804 waliofanya mtihani. Kati yao wavulana ni 15,252 na wasichana 14,133.

Alisema kuwa kati ya wanafunzi hao waliochaguliwa,  wanafunzi 2,127 hawakupata nafasi za kuendelea na elimu ya sekondari kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa.

Bw. Bamporiki alisema kuwa kutokana na tatizo hilo mkoa umeweka mikakati ya kila wilaya kuongeza vyumba vya madarasa katika shule za zamani na kukamilisha shule mpya ili zifunguliwe na kuchukua wanafunzi waliosalia vijijini licha ya kufaulu mitihani yao.

Aliagiza kama kuna shule ambazo zimebaki na nafasi zitangazwe, ili wazazi waweze kuombea watoto wao, hata kama itakuwa nje ya wilaya zao.

3 comments:

  1. Mimi natoka wilaya ya Bukoba na mara kwa mara uwa naenda likizo etc.Tatizo kubwa la wilaya hiyo ni walimu kukat tamaa na kuijiingiza kwenye ulevi wa kupindukia,sio siri waalimu wengi ni walevi na wamepoteza heshima katika jamii,sabau nyingine ni kuwa waalimu wnegi wanafundishia vijijini kwao waliko zaliwa ama sehemu walizoisha kaa muda mrefu na ku establish makazi ya kudumu,matokeo yake muda mwingi wanakuwa kwenye mashamba yao ama kwenye shughuli nyingine za kijamii na za kifamilia,unapotokea msiba kijijini siku hiyo ni public holiday,shule inafungwa kuruhusu waalimu kwenda msibani etc Waalimu wengi pia uwezo wao umefikai kikomo na hawapati mafunzo yoyote ya kuchangamsha vichwa na wengine hata kusahau waliyojifunza vyuoni,kwa kweli inabidi mbinu za maksudi zifanyike kusaidia wanafunzi kwani wao ni innocent victims

    ReplyDelete
  2. Hayo yaliyosemwa na `anonymous` hapo juu yanawezekana yakawa hivyo, lakini pia inawezekana isiwe hivyo.Serikali ya mkoa husika itafute tatizo kwa kuunda tume huru kabisa ikafanye uchunguzi yakinifu.Nasema tume huru kwa sababu inawezekana tatizo likawa sio kwa waalimu likawa kwa uongozi wa elimu mkoa au wilaya husika.Nawakumbusha viongozi wa elimu,walimu na wadau wote kwamba, Elimu ndio urithi bora na ni funguo ya maendeleo ya mahali husika.

    ReplyDelete
  3. pETRO eUSEBIUS mSELEWADecember 7, 2010 at 1:14 PM

    Turudishieni Mnali wetu...hata Mwalimu Nyerere aliwachapa viboko akina nanihiu!Lakini,CCM hapo ndo wanafurahia..wajinga wanaongezeka ili waendelee kutawala kwa 'amani na utulivu'.

    ReplyDelete