Na Peter Mwenda
MAMLAKA ya mawasiliano Tanzania (TCRA) inatarajia kuweka wazi mpango kazi wa kuandaa wananchi kuingia kwenye teknolojia mpya ya utangazaji wa digitali katika mkutano wake wa kutimiza miaka kumi kwa utangazaji nchini.Mkurugenzi wa
Mawasiliano wa TCRA, Bw. Habbie Gunze alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la waandishi wa habari lililotaka kufahamu jinsi gani wananchi wameandaliwa kupokea mfumo huo mpya ambao utawahitaji kununua ving'amuzi ili kupata amatangazo ya televisheni.
Bw. Gunze alisema kila mabadiliko ya teknolojia yana gharama zake, na kuwa katika mabadiliko hayo kuna watu ambao watalazimika kubadili televisheni zao na wengine kununua ving'amuzi.
"Katika mkutano wa kesho tutaweka wazi mpango wa kuhamasisha wananchi," alisema.Maelezo hayo yalitolewa wakati mamlaka hiyo inaeleza kwa waandishi wa habari mkutano wa wadau wa utangazaji, unaofanyika leo jijini Dar es Salaam, ukiwa ni maadhimisho ya miaka 10 ya utangazaji nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Bi. Rehema Makuburi akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, alisema mkutano huo utakutanisha wadau wa sekta ya utangazaji nchini na Afrika Mashariki.
Bi. Makuburi alisema mkutano huo wenye kaulimbiu ya Fursa ya Matumizi ya Miundombinu ya Mfumo wa kasi wa intaneti katika Afrika Mashariki umelenga kuonesha kukua kwa mifumo wa njia za mawasiliano kutoka analogia kuingia digitali.
"Mkutano huu unatarajiwa kuhudhuriwa na watangazaji na wamiliki wa vyombo vya habari vya redio, televisheni kutoka nchini na kwingineko Afrika Mashariki," alisema Bi. Makuburi.
Alisema mfumo wa digital umechangia kukua kwa haraka na kubadili sekta ya utangazaji nchini ambako kumeleta muonekano mpya.Pia alisema kuingia kwa mfumo wa kasi wa intaneti katika Afrika Mashariki baada ya kuwepo mikongo miwili ya mawasiliano, Easy Fibre na Seacom kumeongeza mawasiliano na matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano.
Alisema mfumo huo utasaidia huduma nyingi za utangazaji na kutoa fursa mpya za kutengeneza vipindi kwa ajili ya mfumo wa utangazaji wa digitali.
"Hivi sasa ni rahisi kuona Watazamaji wa vipindi mbalimbali wakishiriki katika vipindi kupitia ujumbe mfupi (sms) au kupiga simu moja kwa moja studio na wengine kuona vipindi wakiwa safarini," alisema Bi. Makuburi.
No comments:
Post a Comment