*Yachapwa na Ethiopia 2-1
Na Elizabeth Mayemba
TIMU ya taifa ya Kenya 'Harambee Stars' imeondolewa katika michuano ya Kombe la CECAFA Tusker Challenge, baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Ethiopia jana, katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.Hii ni mechi ya pili kwa
Kenya kufungwa, ambapo mechi ya kwanza walifungwa na Malawi mabao 3-2, hivyo wamebakiwa na mechi ya kukamilisha ratiba dhidi ya Uganda kesho.
Mpira huo ulianza kwa Kenya kufanya mashambulizi, ambapo sekunde ya 38, Bob Mugalia alikosa bao la wazi baada ya kuupiga mpira nje akiwa amebaki na kipa wa Jemel Bushera.
Ethiopia walipata bao la kwanza dakika ya 25, baada ya Shemeles Bekele Godo kupiga mpira wa adhabu uliokwenda moja kwa moja wavuni.
Bao hilo liliwaongezea nguvu Ethiopia na kulishambulia zaidi lango la Kenya, dakika ya 45, Godo aliyekuwa mwiba kwa wapinzani wao, aliifungia timu yake bao la pili.
Kipindi cha pili kila timu ilikianza kwa kasi huku kila moja ikitafuta mabao, lakini Kenya ndiyo waliokuwa na kazi wakisaka mabao ya kusawazisha.Kenya itabidi wajilaumu kwani mara kwa mara wachezaji wake walikuwa wakifika langoni mwa Ethiopia, lakini walishindwa kuukwamisha mpira wavuni.
Dakika 15 za mwisho, Kenya walionekana kuutawala mchezo, ambapo dakika ya 84, walifanikiwa kupata bao lililofungwa na Fred Ajwang.Kwa matokeo hayo, Kenya wanasubiri mechi ya mwisho kukamilisha ratiba wakiungana na Sudan.Katika mechi iliyochezwa mchana, timu ya taifa ya Uganda 'The Cranes', imetoka sare ya bao 1-1 na Malawi.
Malawi ndio walioanza kupata bao dakika ya pili, baada ya nahodha wa Uganda, Andrew Mwesingwa kujifunga bao akiwa katika harakati za kuokoa mpira wa hatari langoni kwao.
Uganda walisawazisha bao hilo dakika ya 80, kupitia kwa Emmanuel OKwi.Leo, kutakuwa na mechi kati ya Somalia na Zambia, ambayo itachezwa saa nane mchana, na kufuatiwa na mechi kati ya Zanzibar na Rwanda.Wakati huo huo, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limeongeza siku kwa mashabiki wa soka nchini kuingia bure uwanjani, badala ya ofa hiyo kumalizika kesho, sasa itamalizika Jumapili.
Rais wa TFF, Leodegar Tenga, alisema wameamua kufanya hivyo ili kuongeza hamasa katika michuano hiyo, hivyo kuanzia Jumatatu mashabiki wataanza kulipa kiingilio, ambapo kiingilio cha chini kabisa kitakuwa sh.2,000 na cha juu sh.10,000.
No comments:
Post a Comment