Na Peter Mwenda.
HATIMAYE kitendawili cha lini fidia ya wakazi wa Kigilagila wanaotakiwa kuhamishwa kupisha upanuzi wa uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) kimetenguliwa baada ya
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Bw. Leonidas Gama kutangaza kuanza kutoa malipo hayo kesho.
Akitangaza mbele ya waandishi wa habari na Kamati aliyoiunda Juni mwaka huu kama njia mbadala ya kulipa wakazi 864 wa Kigilagila, Bw. Gama alisema wataanza kulipa wakazi 330 wenye maeneo ambayo watapisha kupimwa viwanja vipya.
Alisema jumla ya sh. bil. 10.4 zitatumika kulipa wakazi 864 wa Kigilagila na sh. mil. 600 zitatumika kulipa wakazi wa Nyeburu, Zavala, Kigogo Fresh, Kivule na Kinyamwezi ambao maeneo yao yamechukuliwa na serikali kwa ajili ya kuhamia watu wanaohamishwa kutoka Kigilagila.
"Wananchi wa Kigilagila na maeneo ya Zavala, Nyeburu, Kinyamwezi, Kivule na Kigogo Fresh katika manispaa ya Ilala, serikali kupitia Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania itaanza awamu ya pili ya kuwalipa fidia na mali kwa ajili ya upanuzi wa kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere," alisema Bw. Gama.
Alisema Desemba 1-2 malipo yatatolewa kwa wananchi 77 wa eneo la Zavala ambao mashamba yao watahamia wakazi wa Kigilagila, Desemba 3-4 kwa ajili ya wakazi 73 wa Nyeburu, Desemba 6-8 wakazi 126 wa Kinyamwezi, Desemba 10-11 kwa ajili ya wakazi (54) wa Kigogo Fresh na Kivule.
Bw. Gama alisema malipo hayo yatafanyika kwa njia ya hundi kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 10 kamili katika bwalo la Maofisa wa Magereza, Ukonga na wakazi hao wanatakiwa kuwa na vitambulisho halali pamoja na fomu za uthamini.
Alisema baada ya kukamilisha fidia kwa wenye mashamba, itafuata kazi ya ugawaji wa viwanja kwa wakazi wa Kigilagila ambao wanatakiwa wafike na vitambulisho vyao halali kuchukua hundi zao katika bwalo la Magereza kuanzia Desemba 29 hadi Januari 22 mwakani kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa 10 jioni.
Alisema ulipaji findia umezingatia usumbufu uliojitokeza katika malipo ya fidia kwa wakazi wa Kipawa ambao walizusha malumbano na mapambano ya silaha kugombea viwanja.
Mhandisi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA)Injinia William Shechambo alisema eneo lote litakuwa na ekari 1,240 baada ya kuhamisha watu wa Kigilagila na Kipunguni A.
Alisema eneo la Kigilagila litakuwa kwa ajili ya kujenga njia ya pili ya kurukia ndege, eneo la Kipawa zitajengwa hoteli na kumbi za mikutano.
No comments:
Post a Comment