*Uganda, Malawi zatoka kifua mbele
Na Zahoro Mlanzi.
BAADA ya mashindano ya Chalenji kukosa msisimko kwa mashabiki kushindwa kuingia uwanjani, Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), limetoa ofa kwa
siku nne kuanzia leo, wapenzi wa soka kwenda kushuhudia mashindano hayo bure.
Mashindano hayo yalianza kutimua vumbi Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam lakini idadi ya mashabiki waliofika kushuhudia mashindano hayo ni ndogo tofauti na miaka ya nyuma.
Mbali na hilo, jana kwenye uwanja huo, kulipigwa michezo miwili ambapo wa kwanza uliopigwa saa nane mabingwa watetezi wa kombe hilo, Uganda 'The cranes' iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ethiopia na Malawi iliinyosha Kenya mabao 3-2.
Akizungumza kwenye ukumbi wa mkutano ndani ya uwanja huo, Rais wa CECAFA, Leodegar Tenga alisema anashukuru mzunguko wa kwanza kumalizika bila matatizo yoyote.
Alisema licha ya mzunguko huo kwenda vizuri, lakini bado hajaridhishwa na idadi ya watu wanaokwenda uwanjani, hivyo anawaomba wajitokeze kwa wingi kwani kuanzia leo mpaka Ijumaa hakutakuwa na kiingilio.
"Mpira ni watu na ninajua inawezekana watu bado wanadunduliza fedha za kujia uwanjani, hivyo waziweke mpaka Jumamosi ndiyo kutakuwa na kiingilio lakini kuanzia kesho (leo), mpaka Ijumaa ni bure," alisema Tenga.
Mbali na hilo, Tenga aliipa pole timu ya Somalia kwa kupata ajali jana asubuhi wakati wakienda mazoezini na kwamba wachezaji wawili waliumia na wanaendelea vizuri.
Katika michezo iliyopigwa jana, Uganda ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Ethiopia ambapo mabao yao yalifungwa na Massa Simeone dakika ya 32 na Henry Kisseka dakika ya 47, huku lile la kufutia machozi likifungwa na Shemeles Godo dakika ya 28.
Mchezo uliofuata ilizikutanisha Malawi na Kenya ambapo Malawi ilishinda mabao 3-2 na mabao yao yalifungwa na Victor Nyirenda dakika ya kwanza na David Banda dakika za 26 na 81.
Mabao ya Kenya yalifungwa na John Baraza kwa kichwa akiunganisha krosi ya Bob Mugalia na la pili lilifungwa na Fredy Ajwang, dakika ya 44 kutokana na mpira wa adhabu uliopigwa na Christopher Litswa kushindwa kuokolewa.
No comments:
Post a Comment