21 October 2013

WANANCHI WAONYWA UUZAJI HOLELA WA ARDHI Na Mwandishi Wetu, Korogwe
  Wananchi wa vijiji vya Kwagunda na Mnyuzi katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga, wameaswa kuwa makini na kutolaghaiwa kuuza ardhi yao mara baada ya kazi ya kupanga matumizi bora ya ardhi, kupimwa na kugawiwa hatimiliki katika maeneo yao kukamilika
. Rai hiyo imetolewa juzi na Meneja Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA), Makame Juma Pandu wakati akifungua mafunzo ya mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa wananchi wa vijiji hivyo vitakavyoshiriki kuandaa mpango na kufanya kazi ya upimaji wa ardhi za vijiji vyao yaliyofanyika kwa pamoja katika Kijiji cha Mnyuzi.
Pandu aliwaeleza wananchi hao kuwa ardhi ikishapimwa na kupatiwa hati huongezeka thamani maradufu; na hivyo wapo wajanja ambao wakisikia ardhi ya Kwagunda na Mnyuzi imepimwa na kutolewa hati watafika katika vijiji hivyo kwa lengo la kuinunua ili waweze kunufaika nayo.
"Baada ya kupimiwa na kupatiwa hati wajanja watakuja kutaka muwauzie ardhi, kuweni makini kwani tumekuja kupima ardhi hii ili iwanufaishe ninyi wakazi wa vijiji hivi na watoto wenu kwani mkishakuwa na hati mtaweza kuzifanyia matumizi mbalimbali kama kuweka dhamana benki na kuchukua mikopo, hata watoto wenu kusomeshwa na mikopo ya vyuo vikuu kwa dhamana ya hizo hati,hivyo kabla hamjauza jihakikishieni masilahi yenu na vizazi vyenu kwanza," aliongeza Pandu.
Aidha, Pandu aliwaomba wadau hao kuzingatia mafunzo hayo na kueleza kuwa vijiji vyao vimewaamini na kuwachagua wao kufanya kazi hiyo kwa niaba yao; hivyo kwa kushirikiana na wataalamu wataandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi ambao ukipitishwa na vijiji vyao ndipo watafanya zoezi la upimaji wao wenyewe kwa kushirikiana na wataalamu wa ardhi wa Halmahauri ya Wilaya ya Korogwe.
  Nao wananchi wa kijiji hicho walieleza matumaini yao ya kupatiwa fursa hiyo ya kupimiwa maeneo yao kwa kueleza kuwa ni kuondokana na umaskini kupitia mpango huo na wako tayari kushawishi wenzao wa vijiji jirani vya Lusanga,Shambakapori na Kwamzindaha kuuomba mpango huo kupitia halmashauri ya wilaya ili kwa pamoja waweze kunufaika.
  "Sisi tumefurahi sana kupata mpango huu kwani tunajua gharama za upimaji tusingeweza kumudu mwananchi mmoja mmoja,hivyo tunaishukuru sana serikali kupitia MKURABITA na tutawashawishi wenzetu wa vijiji jirani waombe mpango huu kwani wakazi wengi wa Mnyuzi wana mashamba katika vijiji jirani," alisema Judith Muro mkazi wa kijiji cha Myuzi.
  Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe ina vijiji 122 ambapo ni Kwagunda na Mnyuzi pekee ndivyo vilivyofikiwa na mpango wa kurasimisha rasilimali ardhi vijijini (MKURABITA) ambao pia umekwishafanyika katika vijiji vingine vichache nchini.

No comments:

Post a Comment