21 October 2013

MUNGAI ATAKA VIBALI WALIMU WA NJE VIPUNGUZWE GHARAMA Na Rachel Balama
  Serikali imeshauriwa kufuta malipo ya vibali vya kazi kwa walimu wanaotoka nje ya nchi ili kuzisaidia shule hizo kutoa elimu bora na kutoathiri mapato na matumizi ya shule husika. Mwito huo ulitolewa Dar es Salam, mwishoni mwa wiki na aliyewahi kuwa Waziri wa Elimu, Joseph Mungai, katika mahafali ya kidato cha nne ya Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Ghomme ya Jijini.

  Alisema kuwa serikali imekuwa ikiziteka shule binafsi zinazoajiri walimu toka nje ya nchi dola 1,500 kwa ajili ya vibali vya kufanya kazi hapa nchini. "Gharama kwa sasa zimepanda kutoka dola 4,000 kipindi cha nyuma hadi kufikia dola 1,500, gharama ambazo ni mzigo kwa shule hizo," alisema. 
  Alisema kuwa ni vyema Serikali ikafuta gharama hizo kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ili shule zenye uwezo wa kuajiri walimu toka nje waweze kuajiri na kutoa elimu bora. Aliongeza kuwa pia katika operesheni ya kuwaondoa wahamiaji haramu maarufu kama operesheni kimbunga, aliitaka serikali isiwakamate na kuwarudisha kwao walimu kutoka nchi nyingine. 
  Alisema ni vyema Serikali ikawawekea utaratibu mzuri wa kurekebisha vibali vyao vya kazi kwa walimu hao ili waweze kufundisha katika shule mbalimbali hapa nchini.
   Pia aliongeza kuwa Serikali iwe na wepesi wa kuzisaidia shule binafsi kwa kuwa inao uwezo na pia ni wajibu wa serikali kuzisaidia shule hizo. Katika mahafali hayo Mkurugenzi wa Benki ya Habib Afrika Limited, Syed Mukhtar, alitoa vyeti na zawadi kwa wahitimu 62. Naye, mmiliki wa shule hiyo, Emmanuel Malangalila, aliwataka wazazi kuhakikisha kuwa wanafunzi wao wanaomaliza kidato cha nne wanajiendeleza na kozi ndogo ndogo wakati wakisubiri majibu yao. 
  Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi, George Mlawa, alisema kuwa katika dunia ya sasa hauwezi kupambana na umaskini kama elimu haizingatiwi. Alisema kuwa hakuna umaskini mbaya kama wa mawazo ambao unatokana na watu kukosa elimu.

No comments:

Post a Comment