24 August 2013

KAMATI YABAINI MADUDU HAZINA



Anneth Kagenda na Mariam Mziwanda
KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), imebaini wizi wa mabilioni unaofanywa na Hazina kwa kutakatisha fedha katika malipo ya halmashauri nchini.Utakatishaji huo unadaiwa kufanywa kwa kufoji malipo hewa na kuongeza takwimu za fedha kwenye bajeti za halmashauri
.Mwenyekiti wa Kamati hiyo Bw. Rajabu Mbarouk aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa kikao cha kamati hiyo."Kuna utoroshaji wa fedha haramu kutoka Hazina kwenda katika halmashauri, kamati hii imelifanyia uchunguzi jambo hili na tuna mifano ya Halmashauri ya Mbarali ambayo ilihitaji sh. milioni 70 kwa ajili ya bajeti yake lakini ikapewa sh. milioni 724.6.
"Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Mjini (Tanga), walitakatisha sh. milioni 500, Mvomero (Morogoro), sh. milioni 85 zote kutoka Hazina...hapa kuna mchezo mchafu," alisema.Akizungumzia utendaji wa Halmashauri ya Kiteto, alisema halmashauri hiyo imekuwa na matumizi yasiyo na tija zaidi ya sh. milioni 25 na kumtaka Mwenyekiti wa halmashauri hiyo kuhakikisha anazingatia sheria na kuheshimu  maamuzi ya Mkurugenzi licha ya kuwa mwanamke.
"Mwenyekiti tunakuomba sana zingatia sheria...huyu mama ni Mkurugenzi, msitumie mila na tamaduni kumuona hana mamlaka hii nchi inaendeshwa kwa sheria, mila na taratibu zisije kuendesha nchi mzingatie mamlaka ya Serikali tunalisema hili kwa sababu tumeliona hata katika majibu yenu," alisema.
Naye Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Bw. Seleman Zedi, alisema halmashauri hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo kushindwa kukusanya sh. milioni 500 kutoka kwa mawakala wa mapato ya kilimo ambao ni vyama vya ushirika vya kilimo.
Alisema halmashauri hiyo ina ushirikiano mdogo kiutendaji kati ya halmashauri, madiwani, vyama vya ushirika vya kilimo pamoja na kuwepo ubadhirifu mkubwa katika nidhamu ya fedha."Kuna mtandao wa ubadhirifu hivyo kamati imeitaka ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kufanya ukaguzi wa nyaraka mbalimbali," alisema

No comments:

Post a Comment