23 August 2013

EBSS KUINGIA KAMBINI WIKI IJAYO


Na Ester Maongezi
WASHIRIKI 20 waliopita katika mashindano ya kuimba ya Epiq Bongo Star Search (EBSS), wanatarajia kuingia kambini wiki ijayo kwa ajili ya kujiandaa na fainali ya michuano hiyo.Akizungumza Dar es Salaam jana Mkurugenzi wa Kampuni ya Benchmark Production inayoandaa mashindano hayo, Rita Poulsen alisema wameamua kuwaingiza kambini washiriki hao, ili kujifunza mambo mengi zaidi
.Rita alisema amefurahi kupata idadi nzuri ya vijana na wenye ubora waliojitokeza kwenye usaili na anaamini kwa mwaka huu kutakuwa na ushindani mkubwa."Tumepata washiriki makini kutoka mikoa mbalimbali, hivyo mashindano ya mwaka huu yatakuwa na ushindani mkubwa tofauti na miaka iliyopita na nina imani tutapata wasanii bora zaidi," alisema Rita
Rita alisema mashindano hayo kwa mwaka huu yatarushwa kupitia kituo cha TBC Taifa kila Jumapili.
Alisema wameamua kuitumia TBC kwa sababu za kibiashara na hiyo ni kutokana na tafiti alizozifanya, kabla ya kufikia uamuzi huo."Hakuna sababu nyingine iliyosababisha kuyahamishia matangazo ya EBSS kutoka ITV, kama uvumi unavyoenezwa na baadhi ya watu ila nilijaribu kufanya uchunguzi na kugundua TBC inatazamwa karibu mikoa yote ya Tanzania.
"Hiyo kwangu nikaona ni fursa kwa Watanzania kupata burudani na kutambua vipaji vilipo nchini," alisema Rita.Naye mshindi wa mwaka jana wa EBSS, Walter Chilambo alisema vijana wajitokeze kwa wingi katika mashindano hayo na kwa wale waliokosa nafasi ya kujisajili kwa mwaka huu nafasi bado ipo kwa mwakani, hivyo wasikate tamaa.Usaili wa EBSS mwaka huu, ulifanyika katika Mikoa sita ya Arusha, Mbeya, Mwanza, Zanzibar, Dodoma na Dar es Salaam. Washiriki 50 walipatikana lakini walichujwa na kubaki 20.

No comments:

Post a Comment