21 February 2013

Tuunge mkono TASAF III kuokoa kaya masikini



WIKI hii Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) umeanza kutoa mafunzo ya kujenga uelewa wa wadau kuhusu Mpango wa Kijamii wa Uhawilishaji Fedha kwa Kaya Masikini.

Mpango huu unaotekelezwa katika Awamu ya Tatu ya TASAF ambapo umeanzishwa ili kuwezesha kaya masikini na zilizo katika mazingira hatarishi kupata fedha za kujikimu katika mahitaji muhimu ya lishe bora, huduma za afya na elimu.

Pia mpango huo unalega kuwezesha kaya masikini kupiga hatua kutoka katika hali ya umasikini na mazingira hatarishi na hatimaye kuondokana na umasikini kabisa.  

Ndiyo maana mafunzo hayo yameanza kwa watendaji ili wawe na uelewa mzuri wa utekelezaji wa mpango huo. Mafunzo hayo yameanza kwa watendaji wa Bagamoyo na yataendelea kwenye wilaya zingine.

Utekelezaji wa Mpango huo unatarajiwa kuimarisha uwazi, uwajibikaji na kutoa fursa kwa makundi mbalimbali kushiriki kwa kutumia mfumo madhubuti wa kubaini walengwa katika vijiji.

Tuna imani kuwa mpango huu utafanikiwa kwa kuangalia mafanikio yaliyopatikana wakati wa utekelezaji wa miradi ya awamu ya kwanza na ya pili ya TASAF, ingawa kulikuwa na changamoto zilizojitokeza, kubwa ikiwa ni uhaba wa fedha za kukidhi mahitaji makubwa ya miradi.

Changamoto hizo zilizojitokeza ndizo zilizoifanya Serikali kuandaa awamu ya tatu ya TASAF. Hatua ya Serikali kuanzisha awamu ya tatu  ni kielelezo kuwa ina imani na menejimenti ya TASAF na sisi tuna imani nayo kwani waliobahatika kutembelea miradi iliyotekelezwa katika awamu zilizopita watakubaliana na sisi kuwa awamu hii ya tatu itakuwa mkombozi kwa walengwa wengi.

Na hii inatokana na utaratibu mzuri uliowekwa wa kuwatambua walengwa wa mpango huu ili waweze kunufaika. Tunatoa mwito kwa wale wote watakaokabidhiwa dhamana ya kusimamia mpango huo kuhakikisha wanatanguliza uaminifu ili lengo lifikiwe.

Kama watendaji watakaohusika na utekelezaji wa mpango huu watakuwa wazalendo kama wale waliosimamia awamu mbili zilizopita, basi hali ya Watanzania wanaoishi katika hali ya umasikini itabadilika.

Kila mmoja ajidhatiti kuhakikisha malengo yanafikiwa kwa ukamilifu. Ushiriki wa wadau wote katika mpango huu ni jambo la muhimu, hivyo tuna imani wale watakaopatiwa mafunzo hayo ambayo yamezinduliwa wilayani Bagamoyo watakuwa mabalozi wazuri wa kuieleza na kuitekeleza kikamilifu miongozi na taratibu watakazopewa katika maeneo husika.

Wao ndiyo askari wanaotegemewa na Serikali kuunga mkono utekelezaji wa mpango huu katika vijiji vyetu ili kuondoa umasikini kwa manufaa ya jamii.

Kwa hili hatutakiwi kurudi nyuma hasa kuzingatia kuwa mikakati ya Serikali ni kuhakikisha inatekeleza malengo yaliyomo kwenye Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUKUTA) na yale yaliyomo kwenye Malengo ya Maendeleo ya Milenia MDGs).

No comments:

Post a Comment