26 February 2013

Tuisaidie Serikali kuinua kiwango cha elimu nchini


NCHI mbalimbali zilizopiga hatua ya maendeleo, ziliona umuhimu wa kuwekeza katika elimu ili wananchi wake waweze kutumia maarifa waliyonayo kutatua matatizo yaliyopo kwa wakati.

Ni wazi kuwa, matarajio ya elimu bora kwa jamii yanatokana na mafunzo bora ya walimu ambao ndiyo watendaji wakuu katika mchakato wa kufundisha.

Serikali na wadau wa elimu nchini, wamefanya jitihada kubwa za kuboresha elimu kupitia Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya
Msingi (MMEM) na ule wa sekondari (MMES).

Jitihada hizo zimesaidia kuongeza idadi ya wanafunzi katika
shule nyingi za kata nchini. Idadi ya walimu, nayo imeongezeka tofauti na siku za nyuma kabla ya kuanzishwa MMEM na MMES.

Pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa ili kuboresha mazingira ya sekta hiyo nchini, ubora wa elimu haujafikia kiwango kinachostahili kama inavyokusudiwa na Watanzania wengi.

Ni jambo la kawaida kuona wahitimu wa darasa la saba hawajui kusoma wala kuandika. Uduni wa elimu nao unaendelea kushamiri katika ngazi zote kuanzia msingi, sekondari na vyuoni.

Wanafunzi wanamaliza masomo na kutunukiwa vyeti wakiwa na maarifa finyu na uwezo mdogo wa kufikiri hivyo kushindwa kuchangia kikamilifu maendeleo ya jamii inayowazunguka.

Zipo sababu nyingi zinazochangia kushuka kwa kiwango cha elimu na moja wapo ni walimu wetu kuzidiwa na mzigo wa wanafunzi darasani pamoja na mazingira duni ya kufanyia kazi.

Hali hiyo inachangia walimukukata tamaa ya kufundisha kwa sababu ya kubinywa haki zao na kulipwa masilahi kidogo.

Sisi tunasema kuwa, shule zenye walimu wa kutosha na waliopata mafunzo bora ya ualimu, wanajituma kufundisha ndiyo maana
shule zao zinafanya vizuri mwaka hadi mwaka.

Upo umuhimu mkubwa wa kushirikisha wadau wa elimu ili kuangalia sababu zinazochangia wanafunzi wetu kutofanya
vizuri katika masomo yao sambamba na kufanyia kazi tafiti zinazofanywa na wadau kama HakiElimu.

Ushahidi mzuri ni shule za seminari na baadhi ya shule binafsi ambazo kila mwaka, zimekuwa zikiongoza katika matokeo ya mitihani hali inayowafanya wazazi wapigane vikumbo ili
mtoto wake apate nafasi ya kujiunga na shule husika.

Imani yetu ni kwamba, umefika wakati wa kuwekeza katika elimu
ili kuchochea maendeleo ya sekta mbalimbali pamoja na kuboresha mafunzo ya walimu wetu kwani bila walimu bora, hakuna elimu bora wala maendeleo.

2 comments:

  1. Tutaisaidia kwa kuizalia watoto wengi zaidi labda pengine watakaozaliwa wanaweza wakawa na akili hawa wa saizi ni feki maana wamezaliwa kipindi cha harakati za usawa (HAKI SAWA)huwezi jua na wao wanatekeleza mfumo huo huo wa haki sawa( KUFELI NA KUFAULU KUWE SAWA)Ukichunguza kwa umakini idadi ya watoto wanaolelewa na mzazi mmoja inazidi kuongezeka siku hadi siku. KAMA NI KWELI TUJIULIZE NI KWANINI?

    ReplyDelete
    Replies
    1. Yawezekana ni mpango maalum ili watoto wao wanaosoma nje ya nchi ndiyo waje wapate ajira kiurahisi na hatimaye watuongoze kwani hawa watoto wa walalahoi hawatakuwa na mpango kulingana na matokeo yao ya mitihani

      Delete