07 January 2013

Wasanii watakiwa wapeleke kazi zao TRA



Na Heri Shaaban

WASANII wa sekta ya muziki na filamu nchini, wametakiwa kabla kupeleka albamu sokoni kazi zao zipitie Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili waweze kuwekewa stika ikiwa na lengo kudhibiti wajanja wanaodurufu kazi zao.

Tamko hilo lilitolewa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa Taasisi ya Muziki Tanzania, Angelo Luhala wakati wa mahafali ya pili ya Chuo cha Muziki cha Alphabetha kilichopo Tabata, Ilala, Dar es Salaam.

Luhala alisema tamko hilo la kuwataka wasanii wa sekta hiyo kazi zao zipitie TRA inatokana na serikali kutambua rasmi kazi zao kuanzia Januari mwaka, huu.

"Naomba wasanii wangu nchini kabla kazi zenu kwenda sokoni zipitie TRA kuweka stika nje na ndani ya kava ili wajanja wasipate nafasi ya kuingiza kipato kupitia kazi zenu "alisema Luhala.

Alisema mkakati huo wa serikali utasaidia kuwainua wasanii kimapato baada ya kulia kwa muda mrefu kuchezewa na wajanja kutokana na kazi zao kuingizwa sokoni kabla ya kutoa albamu.

Pia alisema kuwa wasanii wa sekta hiyo kazi zao zilizopo sokoni zipelekwe TRA kuwekwa mihuri na stika ndipo zirudi sokoni na wasanii ambao watakaidi pindi itakapoanza operesheni ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) wasije kulaumu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Chuo Cha Alphabetha, Mark Manji alisema wanafunzi wengi hupenda kujifunza  vifaa kama vinanda, magitaa, ngoma, kuimba na wachache huonesha kutaka kujifunza  kupiga vifaa vya kupuliza kama tarumbeta au saxophone.

Alisema hadi sasa kuna wanafunzi 10 waliojifunza kutumia vifaa hivyo vya kupuliza.

No comments:

Post a Comment