27 December 2012
Wawekezaji wazawa wapewe kipaumbele kuharakisha maendeleo
Na Eliasa Ally
ILI nchi iweze kunufaika na maliasili ilizonazo, kuna haja ya kutumia wawekezaji wa ndani ama mfumo wa ubia katika utafutaji wa maliasili hizo.
Siku zote wazawa huwa na uchungu wa mali zao hivyo wanaweza kuzilinda na kuzitumia kwa uangalifu.
Uwekezaji unasaidia kuongeza ajira kwani kwa vyovyote anayenufaika nao ni mtu wa karibu na eneo hilo kwakua ndiye mlengwa wa kwanza.
Idara ya Maliasili na Utalii ya katika Halmashauri ya wilaya ya Iringa Vijijini mkoa wa Iringa sasa imeanza kuvutia mwekezaji mzawa kutoka mkoani humo katika Hifadhi ya Ruaha kwa kuwapatia vitalu vya uwindaji na kufanya shughuli za miradi mbalimbali katika vijiji vinavyoizunguka.
Mwekezaji huyo Mkwawa Safari Hunting inayomilikiwa na inamilikiwa na Ahmed Huwelambaye anapatiwa kitalu cha uwindaji cha Kinyangesi chini ya Halmashauri ya Mbomipa kwa sasa amelenga kuhakikisha anatatua kero mbalimbali ambazo wananchi wamekuwa wakizisubiria kwa muda mrefu hali ambayo wawekezaji wengi wa nyuma walikuwa hawafanyi kwa wananchi wa maeneo hayo.
Mwandishi wa Makala hii, ambaye alitembelea katika vijiji 21 vya tarafa za Pawaga na Idodi vinavyopakana na hifadhi hiyo amekutana na wananchi wa vijiji hivyo pamoja na wao wenyewe kutoa hisia zao kuhusiana suala hilo walisema kwa sasa manufaa ya hifadhi hiyo yanaonekana dhahiri.
Wakizungumzia baadhi ya maendeleo ya vijiji kutokana na uwekezaji, wananchi hao walisema kuwa awali walikuwa hawaoni maendeleo yoyote wala manufaa yoyote kutokana na vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo kukosa huduma muhimu.
Wanasema kwa sasa wameanza kunufaika na uwekezaji ambao Mbomipa umewavutia zaidi wazawa ambao kwa sasa wameweza kufanya shughuli za maendeleo kutokana na kuwafahamu wananchi wanachohitaji.
Laurent Matelega mkazi wa Idodi anasema kuwa tarafa za Pawaga na Idodi endapo juhudi zitaendelea kuwapata wawekezaji kama huyo zitawezesha watu kukabiliana na umaskini.
"Kwa sasa tunashuhudia maendeleo ambayo anaendelea kuyafanya mwekezaji huyu ambayo amefanya mikutano na wananchi wa vijiji 21 ili kupata mawazo ya kila kijiji wanataka awafanyie nini katika maendeleo ya wote huu ni mwanzo mzuri," anasema.
Anasema kuwa kwa muda mrefu sasa hakuna maendeleo ambayo wanatakiwa wafanyiwe katika maeneo ya vijiji vyao ikiwemo kuboresha zahanati kwa kuleta madawa ya kutosha, maji, kuchangia katika elimu kwa kuchonga madawati kama mkataba wake unavyozungumza ili wananchi wanufaike moja kwa moja.
Mwenyekiti wa kijiji cha Idodi, Mussa Kigelelo anasema mwekezaji huyo ni wa kwanza ambaye ameleta matumaini kwa wananchi na kuongeza kuwa kupatiwa kwa kitalu cha uwindaji kutaongeza maendeleo ya vijiji ambavyo vinaizunguka Hifadhi ya Ruaha.
Anasema mwekezaji wa kwanza ambaye ameshindwa kufikia tija za kulipa fedha kwa ajili ya kuchangia maendeleo alikuwa anatakiwa kutoa fedha milioni 50 ambapo alikuwa anazilipa kidogo jambo ambalo lilikwamisha kuwalipa walinzi wa vitalu na shughuli za maendeleo kusimama ambapo pia mwekezaji huyo alikuwa hana mahusiano mazuri na wananchi.
Mwekezaji aliyepewa kitalu hicho Huwel, anasema kuwa atahakikisha anafanya maendeleo makubwa kwa wananchi wanaoishi kuzunguka hifadhi hiyo kwa kuchangia shughuli za maendeleo zikiwemo maji, zahanati ambapo alisema kuwa anawatembelea wananchi katika vijiji vyao vyote 21 ili kuongea nao na kujua matatizo yao.
"Kwanza nipo nyumbani, kwa hiyo nitahakikisha ninasaidia kwa nguvu zangu zote, kwa moyo wa dhati na nitaashirikiana kwa karibu zaidi na wananchi wa vijiji husika, ninachoamini ni kwamba wananchi wakishirikishwa katika kila kinachofanyika tunaweza kujadiliana kwa uwazi zaidi na kufikia maendeleo ambayo yanatarajiwa", anasema, Ahmed Huwel.
Anasema kuwa mojawapo ya sifa za mwekezaji anatakiwa kuyajua matatizo na kero mbalimbali za wananchi, na kuongeza kuwa suala hilo ndilo lililomsukuma kuanzisha ziara ya kuwatembelea wananchi katika kila kijiji kati ya vijiji 21 ambavyo vinaizunguka hifadhi hiyo na kujadiliana nao kuhusiana na shughuli za maendeleo ambazo wanataka kufanyiwa.
“Wananchi kutoa maoni yao kuhusiana na shughuli za maendeleo ambayo wanataka kufanyiwa itakuwa ni sehemu ya haki na ni msingi mzuri zaidi kwa kuwa maendeleo ambayo yatafanywa watakuwa wameridhia wao tofauti na pale ambapo mwekezaji unaibuka na kuanza kuwafanyia maendeleo ambayo jamii husika haihitaji wala hainufaiki kwa chochote na maendeleo unayofanya”, anafafanua Huwel.
Anaongeza kuwa kama mzawa wa Iringa imempa hamasa kuhakikisha anafanya shughuli za uwindaji na wakati huo anafanya shughuli za maendeleo yanayokubalika na wananchi ambayo wananchi wenyewe wanakuwa wameridhia katika vijiji vyao, ambapo wageni wanaofika kutembelea hifadhi wataleta mwanya wa kuwanufaisha moja kwa moja tofauti na wakati uliopita.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya MBOMIPA, Philipo Mkumbata akizungumzia kupatiwa kwa kitalu mwekezaji huyo anasema kuwa, alimpatiwa kitalu hicho baada ya kamati ya Mbomipa kupitia majina ya watu wote ambao waliomba na kuanza kuwahoji, kukagua vifaa vyao vya kazi, makambi pamoja na magari ambapo kampuni hiyo ilishinda na kampuni nyingine hazikuweza kushinda.
Anasema kuwa kamati ilimkubali mwekezaji huyo kutokana na kutimiza vigezo vyote hali ambayo iliwawezesha kamati nzima ambayo ilikusanyika kukubali kwa asilimia 80 ambapo Mbomipa walimtangaza ameshinda na kupatiwa kitalu cha uwindaji cha Kinyangesi.
Wawekezaji wazawa daima huwajali wananchi kwanza kuliko wanaopenda kuchukua faida badala ya kuwatumikia wananchi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment