21 December 2012

Uwanja wa Ndege Mugumu wapatiwa bil. 4.7/-


Na Mwandishi Wetu

JUMUIYA ya Grumeti na Mfuko wa Hifadhi ya Wanyamapori, wamekubali kutenga fedha sh. bilioni 4.7, kwa ajili ya mradi wa Uwanja wa Ndege Mugumu, uliopo mkoani Mara.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana
na Meneja Mawasiliano wa jumuiya hiyo, Bw. Shaaban Madanga, imesema fedha hizo zitaboresha miundombinu ya uwanja huo.

Alisema uwanja huo upo nje ya Hifadhi ya Taifa Serengeti, ambao utatumika kama uwanja wa Mkoa na uboreshaji huo pia utahusisha Ofisi za Uhamiaji ili wageni waweze kufika kirahisi kuangalia vivutio mbalimbali vya wanyamapori.

“Mpango wa kuuboresha uwanuja huu tayari umekubaliwa na Serikali ya Tanzania na mashirika mengine ya uhifadhi maizngira kaama Mamlaka za Hifadhi za Taifa (TANAPA).

“Uwanja huu ambao utakuwa wa kimaataifa lakini hautafikia hadhi ya viwanja vikubwa vya kimataifa vilivyopo mikoa ya Kilimanjaro, Mwanza na Dar es Salaam,” alisema Bw. Madanga.

Aliongeza kuwa uwanja huo utasaidia Magharibi ya Serengeti kufikiwa kirahisi na ndege ndogo kama Twin Otter na Cessna ambazo tayari zinafanya safari za kwenda Serengeti.

“Hivi sasa waendeshaji kampuni za kitalii hutumia Kiwanja cha Ndege Seronera kilichopo katika kitovu cha Hifadhi ya Taifa Serengeti, uwekezaji katika miundombinu ya ndani utaleta faida kubwa kiuchumi kwa jamii zenye hali duni kimaisha.

“Pia utazalisha ajira na kuongeza mapato ikiwa ni matokeo ya ongezeko la shughuli za kitalii,” alisema.


No comments:

Post a Comment