13 December 2012
'Uboreshaji sekta ya afya utaharakisha maendeleo'
Na Hamisi Nasiri
KATIKA nchi zilizopiga hatua ya maendeleo na yenye kuwajali wananchi kuhakikisha kuwa wanapata huduma bora za afya, wameipa kipaumbele sekta ya afya kwa kuipatia bajeti ya kutosha ili kutekeleza majukumu yake kikamilifu.
Licha ya mambo mengine muhimu kwa ustawi wa Taifa, suala la afya njema kwa wananchi wake ni la msingi ili kupata maendeleo yanayostahiki yatakayowafanya wananchi kupata maisha bora.
Ikiwa Taifa halina watu wenye afya njema, ni wazi litakuwa katika hali ngumu ya kiuchumi na hata kupoteza mwelekeo wa kiutalawa jambo litakalosababisha wananchi wengi kuishi maisha yasiyo na uhakika.
Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoendelea ambazo zinakabaliwa na changamoto nyingi katika sekta ya afya ikiwemo kiasi kidogo cha bajeti kinachotengwa kwa ajili ya utekelazaji wa mikakati mbalimbali inayowekwa na sekta hiyo jambo ambalo linasababisha huduma za afya zinazotolewa kwenye vituo vya afya na hospitali za umma kuwa duni.
Baadhi ya changamoto zinazoikabili sekta hiyo ni uhaba wa wataalamu mbalimbali kama wauguzi, madaktari, dawa, wataalamu wa maabara na wahandisi pamoja na mafundi
sanifu wa vifaa tiba.
Licha ya hayo sekta hiyo pia inakabiliwa na uhaba wa vifaa tiba, hali hiyo inachangia kuwepo kwa dawa na vifaa tiba visivyokidhi viwango vya matumizi kulingana na sheria za nchi.
Kuwepo kwa changamoto hizo katika sekta ya afya kunachangia utoaji wa huduma za afya kwa wananchi na jamii kwa ujumla kuwa duni na hivyo kusababisha malalamiko ya mara kwa mara kuhusu huduma zinazotolewa katika hospitali, zahanati na vituo vya afya nchini.
Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali ili kuhakikisha huduma za afya nchini zinaimarika na
kufanya wananchi wanapata huduma bora lakini bado jitihada hizo hazijazaa matunda.
Kukosekana kwa wauguzi, madaktari na wataalamu wa maabara kunachangia kwa kiasi kikubwa kurudisha nyuma juhudi za serikali za kuhakikisha utoaji huduma bora za afya katika hospitali zake nchini kuwa duni hali inayosababisha kushindwa kufikia malengo.
Ukosefu huo umekuwa ukiwaathiri wananchi wengi hasa wa kipato cha chini ambao wamekuwa na mazoea ya kutibiwa
katika hospitali za serikali kushindwa kupatiwa huduma zinazostahili ambapo kutokana na hilo wale wenye kipato huamua kwenda katika hospitali binafsi ambazo hutoa huduma bora kwa gharama kubwa.
Serikali inapaswa kutilia mkazo suala la ukosefu wa wataalamu, madaktari na wataalamu wa maabara katika sekta ya
afya ili kuhakikisha maeneo hayo yanaondokana na changamoto hiyo na hatimaye kuweza kutoa huduma bora za afya zinazohitajika kwa wananchi.
Changamoto kubwa katika sekta ya afya ni kukosekana kwa wahandisi na mafundi sanifu wa vifaa mbalimbali vya tiba
ikiwemo mashine za maabara x-Ray, CT-scan pamoja na Ultra Sound ambapo vifaa hivyo vinapoharibika huchukua muda mrefu kufanyiwa matengenezo jambo linalosababisha huduma zinazotolewa kupitia vifaa hivyo kusimama kwa muda
mrefu.
Hatua kama hiyo husababisha vifaa hivyo kutengenezwa kwa gharama kubwa ambapo kama nchi ingekuwa na wataalamu
wake wa vifaa hivyo gharama kama hiyo isingetumika hivyo ni jambo ambalo serikali inatakiwa kulitupia macho ili kuhakikisha nchi inakuwa na wataalamu wa kutosha
wa vifaa hivyo.
Kutokana na serikali kutotenga bajeti ya kutosha katika sekta ya afya imejikuta ikijisahau katika suala zima
la kufanya matengenezo ya kawaida ya vifaa tiba na kuangalia namna ya kuwa na mafundi sanifu kwa ajili ya vifaa hivyo, hiyo ni moja ya sababu kutodumu kwa muda mrefu na kwamba wananchi kukosa huduma.
Licha ya kukosekana kwa wataalamu wa vifaa tiba nchini utaratibu wa serikali uliopo hivi sasa hauwezi kuleta
tija katika utoaji wa huduma kupitia vifaa hivyo katika hospitali zote nchini kwa kuwa hospitali husika haijapewa
mamlaka ya kutengeza vifaa hivyo pindi vinapoharibika.
Kwa kuwa serikali kupitia wizara ya afya na ustawi wa jamii imeingia mkataba na kampuni ya Philips kwa ajili ya
kusambaza vifaa tiba mbalimbali kama vile 'Ultra Sound' katika hospitali zote nchini hivyo suala la matengenezo ya vifaa hivyo pindi vinapoharibika kampuni hiyo ndiyo
yenye dhamana ya kufanya matengenezo ya vifaa hivyo.
Hivyo suala la ukosefu wa madaktari, pamoja na wataalamu wa vifaa tiba iwe katika hospitali, zahanati na kituo cha afya limesababisha baadhi ya madaktari wachache tulionao kuacha kazi na kuamua kwenda katika maeneo mengine hasa kwenye sekta binafsi ambako wanaona kuwa wanaweza kufanya kazi katika mazingira bora.
Naibu waziri wa afya na ustawi wa jamii Dkt Seifu Rashidi wakati akijibu swali bungeni kuhusu mikakati ya serikali kulipa deni lake inalodaiwa na Bohari ya Dawa (MSD) Sh 36
bilioni.
Alisema kwa mwaka huu wa fedha 2012/13, serikali imetenga Sh 268,530,025,036 kwa ajili ya kununua vifaa tiba, dawa na vitendea kazi ili kuboresha utendaji kazi katika zahanati na vituo vya afya pamoja na hospitali za umma nchini.
Alisema kiasi hicho ni tofauti na Sh 181,477,959,040 zilizotumika kwa mwaka fedha 2011/12 juhudi hizo zimekuwa zikifanywa na serikali katika kuhakikisha kwamba changamoto zinazoikabili sekta ya afya zinapungua na kila mwananchi anapata huduma bora ambapo imekuwa ikiongeza mgao wa fedha kwa ajili ya vifaa tiba na dawa kadiri mapato yake yanavyoongezeka.
Wizara ya afya na ustawi wa jamii kupitia kitengo cha vifaa tiba katika wizara, Mkurugenzi wake Magreth Mhando, inadhibitisha kuwa kujisahu kwa serikali katika suala la kuvifanyia matengenezo ya kawaida vifaa tiba kama Ultra Sound, x-Ray na CT-Scan inachangia kuvifanya vifaa hivyo kutodumu kwa muda mrefu hali inayosababisha kukwamisha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi kikamilifu.
Pia wizara hiyo inatambua kuwa ukosefu wa mafundi sanifu wa kutengeneza vifaa tiba ndiyo tatizo linalokwamisha utendaji kazi katika hospitali nyingi za umma na kusababisha kutokuwa na vipimo vilivyopelekwa na serikali.
Ni wakati muafaka kwa serikali kuanza kuchukua hatua za makusudi ambazo zinalenga kuwa na wataalamu wa kutosha
katika fani ya mafundi sanifu wa vifaa tiba ili kuondokana na tatizo la ukosefu wa mafundi wa aina hiyo katika sekta ya afya.
Mapema mwaka huu akiongea katika mkutano wa tatu wa Afrika Mashariki wa Chama cha wahandisi na Mafundi Sanifu wa
vifaa tiba (HAMMET) Samwel Hhayuma ambae ni katibu mkuu wa Chama hicho alisema serikali inapaswa kuhakikisha kuwa sekta ya afya inakuwa na bajeti ya kutosha ambayo itakidhi mahitaji tofauti na sasa ambapo tatizo kubwa ni ufinyu wa bajeti.
Alisema kuwa ni bora Serikali kupitia Halmashauri za wilaya na miji ingetenga bajeti kwa ajili ya kufanya matengenezo ya vifaa tiba katika hospitali ikiwa ni hatua mojawapo ya
kuboresha huduma za afya katika hospitali.
Hatua hiyo ya kutenga bajeti kupitia Halmashauri za wilaya na miji kwa ajili ya kufanya matengenezo ya vifaa tiba kwa kuwatumia mafundi wa vifaa hivyo wachache waliopo ingesaidia kuongeza ufanisi wa huduma za afya katika hospitali za umma nchini.
Ili kuweza kuondokana na changamoto zinazoikabili sekta ya afya ikiwemo uhaba wa madaktari, dawa na wataalamu mbalimbali hasa katika kada ya wataalamu wa vifaa tiba ambayo ni muhimu kama ingeungwa mkono na serikali na ingeweza kuboresha huduma za afya.
Serikali inapaswa kuunga mkono kwa vitendo HAMMET katika kuimarisha sekta hiyo na kwamba hivi sasa kuna haja kwa serikali kuhamasisha vijana kusoma masomo ya fani hiyo ili kupata wataalamu wengi watakaotumika katika ngazi ya
zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, mikoa na za rufaa hatimaye huduma za afya kuimarika.
Bado jitihada kwa serikali katika kuhakikisha sekta ya afya nchini inaondokana na changamoto zilizopo ambazo zinakwamisha
utoaji wa huduma za afya zinahitajika na kwamba cha msingi ni kutilia mkazo suala la kutenga bajeti itakayokidhi mahitaji, ndio mwarobaini wa kuondokana na changamoto katika sekta ya afya.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Vizuri sana naona sasa wananchi wameanza kuelewa msingi wa mgomo wa madaktari
ReplyDelete