24 December 2012

CHF mfuko unaowakomboa Watanzania mijini na vijijini



Na Gladness Mboma

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) upo chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii umeendelea kuimarika tangu kuanzishwa kwake Julai 2001.

Wakati harakati za kutangaza mfuko huo ulipoanzishwa watu wengi walikuwa wakiudharau wakiona kuwa watakapojiunga nao hakuna watakachofaidika nacho.

Serikali inapokuwa ikianzisha kitu inakuwa inatambua faida ya kitu amabacho wanakianzisha kwa kuwa wanakuwa wamekifanyia utafiti na siyo kwamba wanakurupuka kama ambavyo watu wengine wanatambua hivyo.

Katika suala la mfuko huu walikaa na kufanya utafiti na kutambua utakapoanzishwa utakuwa na faida kubwa kwa Watanzania watakaojiunga nao.

Serikali ilipoanza kutangaza mfuko huo wapo Watanzania walioona umuhimu wake wakaitikia wito na kujiunga nao na mpaka sasa wamenufaika nao kimatibabu licha ya kuwepo na changamoto kidogo ambazo zinaweza kurekebishika.

Kutokana na Watanzania kujiunga na mfuko huo na kuona umuhimu wake ilisababisha watu wengi kuanza kuoba faida yake na kujiunga nao.

Tukumbuke kwamba mfuko huu mwanzo ulikuwa ni kwa wafanyakazi wa serikali,lakini serikali kwa kuona umuhimu wake waliamua kupanua wigo wake hadi ngazi vijiji nchini, ambapo Watanzania wengi sasa wamejiunga na mfuko huo na kuona matunda yake.

Ifahamike kwamba unapoamua kujiunga na mfuko huo unarahisisha matibabu yako, badala ya kwenda kupanga foleni kupata matibabu na dawa unakurahisishia wewe kupata huduma ya afya mapema kuliko ambavyo utakuwa ujajiunga na kulazimika kupanga foleni ndefu na kwenda kununua dawa.

Unapokuwa umejiunga na mfuko huo utapata matibabu na dawa papo kwa papo badala ya kupanga foleni kama ilivyokuwa zamani wakati ambao ulikuwa ujajiunga na mfuko huo.

Mkurugenzi Mkuu wa NHIF,Bw.Emanuel Humba anaelezea jinsi mfuko huo ulivyoimarika toka kuanzishwa kwake, ambapo anasema kuwa idadi ya wanachama imeongezeka kutoka 164,708 mwaka 2001, hadi kufikia 474,760 mwezi Juni mwaka huu, ambapo Mfuko una jumla ya wanufaika 2,502,794.

Anasema vituo vya matibabu vilivyosajiliwa kutoa huduma kwa wanachama hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu vimeongezeka na kufikia 5,426.

Kwa upande wa vituo vya Serikali ni asilimia 80, vituo vinavyomilikiwa na mashirika ya kidini ni asilimia 12 na vituo vinavyomilikiwa na watoa huduma binafsi ni asilimia 8.

Bw. Humba anasema mafao yanayotolewa na Mfuko kwa wanachama wake yameongezeka, "hivi sasa tunatoa mafao kumi na moja yakiwemo yale ambayo hayatolewi na mifumo mingine ya bima duniani kote, kama vile huduma za miwani na matibabu kwa wanachama wastaafu.

"Hadi sasa mfuko una watumishi wapatao 345, wanaume ni 205, sawa na asilimia 59 wakati wanawake ni 140 sawa na asilimia 41. Asilimia 38 ya wafanyakazi hawa wako katika Makao Makuu, wakati asilimia 62 wako katika ofisi za Kanda na Mikoa,"anasema.

Anasema Mfuko umesogeza zaidi huduma kwa wanachama wake kwa kufungua ofisi katika Mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar isipokuwa Mikoa mipya.

Aliongeza kuwa usimamizi wa CHF na hamasa ya wananchi tangu mwaka 2009 Serikali ilikasimu madaraka ya usimamizi wa Mifuko ya Afya ya Jamii (CHF) kwa NHIF, awali Mifuko hii ilikuwa inasimamiwa na halmashauri moja kwa moja.

Bw. Humba anasema wakati NHIF inakabidhiwa jukumu hilo idadi ya wanufaika wa CHF walikuwa ni 691,774 tu, lakini hivi sasa Mfuko wa Afya ya Jamii unahudumia zaidi ya wanufaika 3,850,518.

"Kutokana na umuhimu wa Mfuko huu ambao unawalenga Watanzania wengi walio katika sekta ya ajira zisiyo rasmi, NHIF imejiwekea mikakati ya pekee ya kuelimisha umma ili kusajili wanachama wengi zaidi.

"Changamoto za Huduma Pamoja na kuwa na mafanikio mengi, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya bado unakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za elimu kuhusu dhana ya bima ya afya,"anasema.

Anasema changamoto hizo ni pamoja na uhaba wa dawa katika vituo vya huduma,Ukosefu wa Vifaa Tiba katika vituo vilivyosajiliwa,na upungufu wa wahudumu katika vituo vya huduma.

Bw. Humba anasema Mfuko umekuwa ukizitumia changamoto hizi kama fursa ya kuboresha huduma za Mfuko na mazingira wanayopatia huduma wanufaika wa Mfuko.

Akizungumzia mipango ya baadaye anasema ni kuongeza kazi ya utoaji elimu kwa wananchi kupitia mikutano ya siku za wadau, elimu kata kwa kata, Elimu sehemu za kazi, mpango wa elimu kwa njia ya magari ya sinema na matangazo na kutumia vyombo vya habari.

Mipango mingine ni kuboresha mfumo wa vitambulisho vya wanachama,Kujenga vituo zaidi vya matibabu vya mfano katika kanda ili kupunguza uhaba wa vituo vya aina hiyo nchini na kwamba wameanza na Mkoa wa Dodoma.

Anasema kuwa wataendelea kutoa mikopo ya vifaa tiba na ukarabati wa majengo ili kuboresha huduma kwa wanachama na wananchi kwa ujumla,Kuimarisha kaguzi za vituo vya matibabu vilivyosajiliwa ili kuhakikisha wanachama wanapata huduma bora kwa mujibu wa miongozo na mikataba iliyopo baina ya NHIF na watoa huduma.

Pia anasema kuwa watahakikisha vituo vinakuwa na dawa za kutosha kwa kushirikiana na mamlaka husika.

Bw. Humba anasema Mfuko huo umewekewa lengo la kuhudumia asilimia 30 ya Watanzania wote ifikapo 2015. Ili kufanikisha lengo hilo ameiomba serikali iwasaidie kuangalia namna ya kuwapa motisha watumishi wa sekta ya afya wanaofanya kazi katika mazingira ya vijijini ili kuwahamashisha waendelee kufanya kazi katika vituo vya maeneo hayo ambavyo vina uhaba mkubwa wa watumishi.

Pia vitio vihamasishwe kutumia fursa ya mikopo ya vifaa tiba na ukarabati wa majengo ili kuboresha zaidi mazingira na huduma kwa wanachama na wananchi kwa ujumla.

Naye Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Bi.Mwanaidi Mtanda, anasema
baada ya mfuko huo kuanza shughuli zake mwaka 2001, uligundua ugumu uliokuwepo wa kuhudumia wanachama wake waliopo nchi nzima kupitia ofisi yake ya Makao Makuu tu na hivyo kuamua kufungua ofisi za Kanda.

Anasema Mfuko kwa kuanzia ulifungua ofisi 6 za kanda (Kanda za Mashariki, Kati, Kusini, Nyanda za Juu Kusini, Magharibi na kanda ya Ziwa). Hata hivyo kanda hizo ziliongezeka na kufikia 12.

"Kutokana na ongezeko kubwa la wanachama wa Mfuko mwaka hadi mwaka na ongezeko la vituo vya kutolea huduma Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umeona ni vema kusogeza huduma zake karibu zaidi na wanachama kwa kufungua ofisi katika kila Mkoa.

"Mfuko una ofisi katika mikoa karibu yote nchini pamoja na Unguja (isipokuwa mikoa michache iliyotangazwa hivi karibuni).Miundombinu ya kiutawala ya mikoa hii mipya ikikamilika Mfuko utafungua ofisi katika mikoa hii ili kutimiza azma ya yake ya kusogeza huduma karibu na wadau wake na kuwaondolea gharama na usumbufu wa kufuata huduma za Mfuko mbali,"anasema

Anasema kwa mfano kabla ya kufunguliwa kwa ofisi Kibaha, wanachama wao wa mkoa wa Pwani walikuwa wanahudumiwa na ofisi ya Morogoro, mahali ambako ni mbali na kupelekea hali hiyo kuwanyima wanachama haki ya kupata utatuzi wa matatizo yao kwani wengi wao waliishia kukaa bila kutafuta ufumbuzi.

Bi.Mtanda anasema hospitali nyingi hapa nchini zinakabiliwa na tatizo sugu la kukosa vifaa vya kisasa vya uchunguzi wa magonjwa.

Anasema hali hiyo imesababisha wagonjwa wengi kulazimika kwenda Muhimbili, KCMC au Bugando kufuata vipimo hivyo.

Mjumbe huyo wa Bodi anasema Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya uliliona tatizo hilo na kwa dhamira safi kabisa Bodi ya Wakurugenzi ilipitisha uamuzi wa kuanza kutoa mikopo nafuu kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba na ukarabati wa majengo kwa vituo vya kutolea huduma za matibabu vya ngazi zote ambavyo vimesajiliwa na Mfuko.

Fursa hii ya mikopo ya vifaa tiba, inatoa fursa kwa vituo vya ngazi zote kuboresha huduma zake hasa kwa kuwa na vifaa tiba ambavyo vitawawezesha waganga kupata uhakika wa magonjwa ya wagonjwa wanaowahudumia, lakini pia vitasaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza mapato ya vituo husika.

"Kutokana na hali hii, kwa niaba ya Bodi ya Mfuko nawaahidi kuwa, Mfuko una nia ya dhati ya kuisaidia Hospitali ya Tumbi na Mkoa wa Pwani kwa ujumla kwa lengo la kuboresha huduma za afya. Pale Mfuko utakapopokea maombi hayo kutoka kwenu yatafanyiwa kazi haraka,"anasema

Tunatambua kuvisaidia vituo vilivyopo Mkoa wa Pwani kutaimarisha huduma kwa wanachama wetu na wananchi kwa ujumla, lakini pia kutaondoa malalamiko au kero ambazo Watanzania wamekuwa wakikabiliana nazo wakati wa kupata huduma za afya,"anasema

Mikopo hiyo ya Vifaa Tiba imeanza kutolewa tangu mwaka 2007, lakini hamasa ya ukopaji hasa kutoka kwa vituo vya matibabu vya serikali bado ni ndogo sana. Naomba nitumie nafasi hii kuwatangazia viongozi na wamiliki wa vituo vyote vya matibabu vilivyosajiliwa na Mfuko waje kuomba mikopo hii ili waboresha huduma katika vituo vyao,"aliongeza.

Anasema mikopo hii itolewayo na Mfuko si ya kibiashara, bali ina lengo la kuvisaidia vituo kuboresha huduma zake, na hivyo haina riba za kibiashara.

Akizungumzia uboreshaji wa huduma anasema huduma bora za matibabu ndiyo tumaini la kila mwanachama wa Mfuko na kila mwananchi anapokwenda kwenye kituo cha matibabu. Hata hivyo mara nyingi kumekuwa na mazingira ambayo yanakwamisha upatikanaji wa huduma bora za matibabu katika vituo vya huduma.

Anasema moja ya sababu ya hali hiyo ni ukiukwaji wa maadili ya kazi kwa watoa huduma wa vituo vya huduma za matibabu kwamba Mfuko unapenda uwakumbusha watoa huduma kote nchini kwamba wajibu wao wa kuhudumia afya za wananchi ni mkubwa na wautimize wajibu huo kwa kuzingatia taratibu, sheria na miongozo iliyowekwa.

"Kipindi cha nyuma, kulikuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wanachama wetu kwamba wanabaguliwa na kuonekana watu wa bure. Nashukuru kuwa hivi sasa malalamiko hayo yamepungua sana na kubaki katika maeneo machache ambayo watumishi wachache si waadilifu,"anasema.

Amewaomba watoa huduma wasaidiane kuimarisha sekta ya afya kwa kuzingatia maadili ya kazi. "Napenda niwakumbushe kuwa kazi ya kuhudumia watu ina changamoto nyingi na hasa unapomhudumia mgonjwa. Muwe makini na kuzingatia ukweli huo,"anasema.

Anasema Mfuko umejipanga kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2015 uwe unahudumia asilimia 30 ya Watanzania wote. Hili litawezekana iwapo suala la Mfuko wa Afya ya Jamii unaohudumia wananchi walio katika sekta ya ajira isiyo rasmi litapewa msukumo utakaowezesha wananchi wote waandikishwe katika utaratibu wa Bima ya Afya.



No comments:

Post a Comment