11 September 2012

Ujasiriamali nguzo ya kuondoa umaskini nchini



Na Juliana John

UMASKINI ni hali ya ukosefu wa mahitaji ya msingi kwa binadamu kama vile chakula, maji safi, huduma za afya, mavazi na malazi kutokana na kukosa uwezo wa kuvinunua.


Kutokuwa na rasilimali za kutosha husababisha pato la taifa kupungua hali inayoifanya serikali kukosa fedha za kuboreshea huduma za jamii.

Afya duni na ukosefu wa elimu pia ni vishairia vya umaskini kwani wananchi wasipokuwa na afya na elimu hawawezi kuzalisha bidhaa bora zinazoweza kushindanishwa katika soko la dunia.

Nini hatma ya umaskini uliokithiri nchini? Ni swali lisilo na jibu kwani tangu mwaka 1967 rais wa awamu ya kwanza Tanzania alipotangaza azimio la Arusha, walinuia kuondoa ujinga, maradhi na umaskini lakini sasa ni zaidi ya miaka 46 tangu vita hiyo itangazwe na hatujaweza kuishinda, tatizo ni nini?

Natamani kujua tatizo kwani tunaingiza bidhaa toka nje ya nchi zenye thamani karibia ya bilioni nane ilihali tunauza  bidhaa ama huduma nje ya nchi zenye thamani ya bilioni 1.5.

Tumeua kilimo, viwanda  na  kusababisha soko la ajira kuwa gumu, uchumi umebakia kukua katika makaratasi lakini mifukoni mwa watanzania hakuna kitu.

Viko wapi viwanda vya mkonge? vipi kuhusu uvuvi wa baharini?sekta ya madini tumeachiwa mashimo na isitoshe elimu yetu tunayojivunia kukuza imebakia kuwa ya kinadharia zaidi bila ya vitendo.

Si hayo tu kwani tumebaki kununua rada kuangalia juu wakati madawa ya kulevya yanapitishwa chini, twiga wanapanda ndege wakati bibi yangu hajawahi, badala ya serikali kuwekeza katika kilimo inawekeza katika siasa kwani hata matangazo ya kondomu yanatujia kwa hisani ya watu wa Marekani.

Licha ya hayo, ipo mikakati mingi kutoka upande wa serikali kama vile mpango wa kupunguza umaskini Zanzibar,(MKUZA), Mpango wa Kupunguza Umasikini Tanzania (MKUKUTA) na dira ya Taifa ya maendeleo 2025 kama mpango mkakati wa kukuza uchumi na kupunguza umaskini, lakini mipango inaonekana kwa wananchi kama hadithi za kufikirika kutokana na faida yake kutoonekana.

“Ili tuendelee tunahitaji rasilimali watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora bila kusahau utekelezwaji wa ujasiriamali kama nyenzo muhimu ya kutukwamua kiuchumi kutoka katika hali duni ya kimaisha tuliyonayo hadi kuyafikia maisha bora kwa kila mwananchi kama kila mtu kwa nafasi yake atachukua hatua,” aliyasema hayo hayati mwalimu Julius  Kambarage Nyerere.

Ujasiriamali ni nini basi? Ujasiriamali ni ile hali ya kuwa radhi kuthubutu au kuanzisha jambo jipya kwa njia ya ubunifu ambao utampa faida hapo baadaye baada ya kunadi ufanisi wake kwani hata wanauchumi wengi wanakubali kuwa ujasiriamali ni kiungo muhimu katika kukuza na kuendeleza uchumi wa Taifa.

Wengi wao hutazama ujasiriamali kama vile upo kwa ajili ya watu ambao hawana kazi. Siwalaumu wote wenye mtazamo wa aina hiyo kwani haya ni matokeo ya mfumo wa uchumi uliotukuza pia ni mfumo unaoamini kuwa mafanikio ya kweli yanapatikana kwa mtu kusoma na kisha kuajiriwa.

Licha ya hayo, kwa kipindi kirefu sasa serikali na sekta binafsi zimeshindwa kukidhi wimbi la vijana wanaomaliza shule ama vyuo hivyo basi wakati umefika wa kushawishi vijana kuangalia na kutafuta mbinu mpya za kujiajiri kama wajasiriamali ili kuweza kujikimu katika maisha yao ya kila siku.

Pamoja na nia nzuri walizonazo vijana, kipo kizingiti ambacho ni lazima watu wajifunze mbinu mpya za kukivuka. Kizingiti hicho ni elimu itolewayo mashuleni kwani haijawekwa bado katika msingi unaomuwezesha kujiajiri au kuwa mjasiriamali pindi amalazapo.

Bado tupo katika mfumo wa elimu ya kikoloni, ukimaliza shule unachotakiwa ni kuanza kutafuta kazi, mfano ukizunguka jijini Dar es Salaam utakutana na vijana waliohitimu kutoka katika vyuo vikuu mbalimbali wakiwa wamebeba vyeti vyao katika bahasha wakizurura kutafuta kazi.

Wengi wao kati ya hao hakuna anayefikiria kujiajiri kwa kutumia elimu aliyoipata chuoni, kwanini? Ndivyo ilivyo kwani elimu aliyopewa haikumuandaa kinadharia zaidi kuliko vitendo.

Mfano utakutana na mhitimu wa masomo ya kilimo na mazingira ambaye hajui hata shamba lilivyo.

Kwa ujumla dhana ya ujasiriamali imeegemea katika mihimili ya ugunduzi na ubunifu unaohusisha bidhaa mpya, njia mpya za uzalishaji au uendeshaji, masoko mapya na mtandao ambao wenzetu wa magharibi wanaita networking ili kujiletea faida na hata utajiri wa kuweza kuwa muwekezaji mkubwa nchini.

Ikumbukwe kuwa utajiri utokanao na ujasiriamali ama kufanya kazi kwa bidii au umaskini wa mtu huanzia katika fikra na mitazamo yake kwani tajiri huwa tajiri kabla hajamiliki mali yoyote na maskini huwa maskini kabla ya kuridhika na hali yake.

Ujasiriamali ni zaidi ya kuanzisha biashara na hata wale waliojiriwa wanaweza kuwa wajasiriamali kwenye kazi zao kwa kuwa wabunifu na kuanzisha mbinu mpya zitakazorahisisha kazi zao na kuleta ufanisi ili kuepuka  kuwa wabangaizaji na wahangaikaji ilihali tukitaka kuitwa wajasirimali.

Lakini basi tutajipima vipi kujua kama ni wajasiriamali?Kwanza ni kuwa na maarifa ya biashara, kujua mazingira ya biashara, mwelekeo wa uchumi, sheria na masuala ya kifedha.

Aidha vitu vinavyomjenga mjasiriamali ni pamoja na mtaji, fursa, ubunifu na mawasiliano kwani mawasiliano hutuunganisha na kutuweka pamoja ili kupata habari au taarifa za vitu mbalimbali zikiwemo biashara zinazowahusisha wajasiriamali wakubwa na wadogo.

Pia ni vyema kuainisha malengo yako ya miaka mitatu hadi mitano kama mjasiriamali, kuainisha wateja wako wa sasa na wa baadaye, kufahamu washindani wako bila kusahau kujua faida na hasara za kufanya biashara peke yako, ubia au kampuni.

Hii ni kwasababu ujasiriamali ni nyanja ambayo ikitiliwa mkazo inaweza kuleta mapinduzi katika ukuaji wa uchumi, teknolojia, siasa na utamaduni kwa jamii husika ili kutengeneza fursa za kimaendeleo kwa namna moja au nyingine.

Faida nyingine za ujasiriamali ni kwamba hutusaidia kutumia ipasavyo rasilimali tulizo nazo, kupelekea kwenye matumizi sahihi ya rasilimali watu pia hutupa mwanga katika kufanya na kuanzisha shughuli mpya pamoja na kupunguza idadi ya watu tegemezi baada ya kujipatia kipato.

Hali kadhalika ujasiriamali ni njia mbadala ya kuongeza nafasi za ajira katika nchi zinazoendelea kwani ni msingi katika kujiongezea kipato na kupunguza umaskini, hivyo basi ni wajibu wa serikali kusaidia wajasiriamali wakubwa na wadogo ili kuongeza tija katika uzalishaji wa bidhaa na huduma kutoa mchango chanya katika mipango ya maendeleo ya nchi au taifa husika.

No comments:

Post a Comment