07 September 2012
TFF, Vodacom kufunga 'ndoa' Jumanne ijayo
Na Elizabeth Mayemba
KAMPUNI ya simu za mikononi ya Vodacom inatarajia kuingia mkataba wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Jumanne ijayo.
Akizungumza Dar es Salaam jana Ofisa Habari wa TFF Boniface Wambura alisema wadhamini hao wataingia mkataba huyo Jumanne katika ofisi zao zilizopo Dar es Salaam.
" Taarifa rasmi juu ya muda wa kusaini na pande zitakazoshuhudia hafla hiyo itatolewa hivi karibuni, hivyo tutawatangazieni waandishi wa habarim," alisema Wambura
Alisema Ligi Kuu inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Septemba 15, mwaka huu huku ligi hiyo ikishirikisha timu 14.
Mechi ambazo zitafungua dimba la michuano hiyo ni kati ya Simba na African Lyon ambao watacheza Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Polisi Morogoro na Mtibwa Sugar (Jamhuri, Morogoro), Tanzania Prisons dhidi ya Yanga (Sokoine, Mbeya), Mgambo JKT watacheza na Coastal Union (Mkwakwani, Tanga) na JKT Ruvu wao watacheza na ndugu zao Ruvu Shooting (Azam, Dar es Salaam).
Mechi nyingine ni kati ya Kagera Sugar na Azam (Kaitaba, Bukoba), ambapo Toto African watapambana na maafande Oljoro JKT Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Kama ilivyokawaida misimu yote mechi ya Ngao ya Jamii kati ya Simba na Azam FC inatarajiwa kuchezwa Septemba 11, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa,Dar es Salaam.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment