17 September 2012

'Mabadiliko katika kilimo yanaanza na mkulima'


Na Daniel Samson

KILIMO ni sekta muhimu katika maendeleo ya nchi yoyote
duniani, Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi zinazotegemea kilimo kama uti wa mgongo serikali imeweka sera na mikakati ya kuboresha kilimo ili kuinua uchumi wa nchi na kuwaletea maendeleo wananchi.

Sera ya Kilimo Kwanza ambayo inatekelezwa sasa imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali zinazokwamisha maendeleo ya kilimo chenye tija nchini.

Imekuwa inazungumzwa kisiasa kuliko kiutendaji na kuacha lengo kuu la kumuinua mkulima mdogo ili afaidike
na mazao anayoyapata kutokana na kutumia teknolojia mbadala.

Kwa wachambuzi wa masuala ya kilimo wanaiona sera hii inalenga kuwawezesha wakulima wakubwa ambao wengi wao ni wawekezaji kutoka mataifa ya nje ambao hupewa ardhi kubwa kwa madhumuni ya kuendeleza sekta ya kilimo lakini hakionyeshi mabadiliko kwa wakulima wa hali ya chini.

Matokeo yake wananchi wanaporwa ardhi yao na kuwa wanatumwa
katika nchi yao na hata waliopewa dhamana ya kutekeleza sera hii wanakabiliwa na changamoto nyingi ambazo huchangia kuwakandamiza wakulima wadogowadogo.

Kwa kuliona hilo wapo wananchi wachache wenye upeo wa kuona na kujiletea maendeleo wanaungana na kukuza kilimo katika maeneo yao bila kusubiri serikali iwawezeshe.

Taasisi ya Amsha ya Ujasiriamali wa Vijijini ni moja ya taasisi chache binafsi nchini iliyofanikiwa kuunda mradi wa kilimo cha biashara katika wilaya ya Kilwa mkoani Lindi na kuleta mafanikio katika kukuza kilimo cha wakulima waliopo vijijini.

Mwanzilishi na Mwenyekiti wa taasisi hiyo Bi. Ubwa  Maingo
amekuwa ni mwanamke wa kwanza kuleta mapinduzi ya kilimo katika wilaya ya Kilwa kutokana na uzalendo alionao wa kuwainua wanyonge ili wafaidike na rasilimali za nchi. 

Wilaya hii inategemea korosho kama zao kuu la biashara lakini harakati zake zimebadili historia ya wakazi wengi na kuanza kulima mazao mengine ya biashara ili kukuza kipato cha familia.

Bi.Maingo anasema alihamasika kuanzisha mradi wa Amsha katika wilaya hiyo kwa sababu ya umaskini na hali duni waliyonayo watu wa kata za Miteja, Kinjumbi, Mingumbi na Chumo.

Anasema alianza kufanya utafiti wa kilimo katika wilaya hiyo
akihusisha sera ya Kilimo Kwanza na Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania (MKUKUTA).

Anasema aliunda mfumo binafsi tofauti na mfumo mwa serikali wa kuwawezesha wananchi katika kuinua kilimo cha jembe la mkono kwa sababu ya urasimu uliopo katika utekelezaji wake.

Baada ya kuwa na taarifa za kutosha alianzisha programu ya kutoa mafunzo kwa wananchi wa kata zote za Kilwa kwa sababu  anaamini kuwa huwezi kutekeleza sera yoyote ya kilimo bila kuwaelimisha wakulima na kuonyesha mafanikio watakayoyapata katika sera husika.

Anaongeza kuwa sera ya Kilimo Kwanza inaonyesha mapungufu kwa sababu wakulima hawana elimu ya kuwawezesha kutekeleza sera hiyo.

Anaongeza kuwa alitumia miaka miwili kubadilisha mawazo,
mitazamo na itikadi walizokuwa nazo za kuendelea kukaa katika umaskini ikiwa wana ardhi kubwa ya kulima na kuwa na
kilimo cha biashara ili kuondokana na dhana ya kulima kwa ajili ya chakula tu.

Anasema alizunguka vijiji 27 vya kata zote nne na kutoa mafunzo ya kilimo cha kibiashara kwa wanachi akishirikiana na viongozi wa vijiji. Ingawa alipata upinzani mkubwa toka kwa watu mbalimbali na viongozi wa serikali kuwa mradi wake hautafanikiwa kwa sababu viongozi wametumia njia nyingi kuinua kilimo lakini wameshindwa kuleta mabadiliko ya kweli.

Changamoto hizi hazikumzuia kutimiza azma yake ya kuwakomboa wananchi na  alitumia miaka miwili ya kubadili mawazo ya watu ambao wakati wote waliamini kuwa mwanamke hawezi kuishawishi jamii na kuleta mabadiliko.

"Niliwajengea uwezo wa kujiamini na kuunda vikundi vya
ujasiliamali ambapo kila kikundi kina mtaji wake ambao unatokana na michango ya wanachama. Juhudi zimewesha kuunda  vikundi kazi 275 chini ya uangalizi wa tasisi ya Amsha vikijihusisha na shughuli mbalimbali za kilimo.

Baada ya miaka miwili ya kutoa mafunzo ya kilimo cha biashara, akishirikiana na wakulima wa vijiji walianza kutekeleza maazimio yao kivitendo kwa kutafuta ardhi ya kulima bila kutegemea ufadhili wa serikali.

Kwa kuwa wanachama wa vikundi hivyo walikuwa na ardhi kubwa
ambayo haijalimwa walianza harakati za kufyeka na kusafisha mapori ili kupata ardhi ya kulima.

Anasema mtaji wa kuendeshea mradi wa kilimo ulipatikana kwa kuuza miti na kuchoma mkaa katika mashamba ya wakulima, fedha zilizopatikana zilitumika kununua pembejeo za kilimo.

Anaongeza kuwa aliamini kuwa wakulima wana fedha katika ardhi yao na kulikuwa hamna haja kukopa katika taasisi nyingine japokuwa alipata upinzania kwa watu wengi kuwa
hawezi kuwainua wakulima kwa fedha zao wenyewe lakini walifanikiwa kukusanya zaidi ya milioni 48 na kuanza kulima mazao ya ufuta, mtama, mahindi na mihogo.

Anasema vikundi vingi vya wakulima havifanikiwi kwa sababu ya
kuwa na mitazamo tofauti na kutegemea  misaada ambayo huzua mitafaruku mikubwa kwa sababu ya kukosa uaminifu na uwajibikaji wa kuendeleza miradi yao.

“Sisi kama  AMSHA hutupokei fedha yoyote kutoka serikalini wala kwa wafadhili lakini tunachojali ni ushirikiano, umoja na uaminifu kwa kila mwanachama katika kukuza kilimo chenye tija kwa kila mtu”.

Ushirikiano  uliopo katika taasisi ya  AMSHA uliwafanya wafanye kazi kwa mafanikio makubwa japo wanatumia jembe la mkono lakini muitikio wao wa kubadilisha mitazamo na mawazo umewasaidia kuwa na kilimo cha kibiashara ambacho kimekuza kipata cha mwanachama mmoja mmoja na kuboresha familia zao na kutoka katika umaskini uliokithiri.

Baada ya awamu ya kwanza ya mradi huo, vikundi 50 kati ya 275
vilivyokuwa na mtaji wa milioni 48 vimefanikiwa kutengeneza faida ya shilingi milioni 191  kutokana uuzaji wa mazao ya ufuta na mtama kwa viwanda vya ushindikaji na wa tumiaji wengine.

Pia uzalishaji wa mihogo umetengeneza soko kwa kiwanda cha Bia (TBL).

"Mafanikio haya yamechangiwa zaidi na mafunzo ambayo yanaendelea kutolewa kwa wakulima hao kutoka kwa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya Naliendele ambao wanatoa mafunzo ya kuchagua mazao ya kulima kulingana na aina ya udongo unaopatika sehemu husika," anasema.

Kutokana na mwamko walioupata wakulima hao wanajishughulisha na shughuli nyingine za ujasiarimali ambapo wameanzisha mradi wa kujenga mabwawa ya kufugia samaki, ufugaji wa
nyuki na wanyama kama ng’ombe, mbuzi na kuku.

Ili kufanya kilimo kiwe cha msimu wote wa mwaka wakulima wamejifunza na kuendeleza miradi ya kutunza bustani za mbogamboga na matunda ili kutengeneza kipato hivyo kuwa na kilimo cha mwaka mzima.

Changamoto kubwa iliyopo ni ushirikiano mdogo kutoka kwa Maafisa wa kilimo ambao kiasi kikubwa wameshindwa kutimiza majukumu yao ya kuendeleza kilimo katika maeneo yao kutokana kwa sababu ya majukumu mengi ambayo yanawafanya wasiwahudumie wakulima kwa wakati.

Anaongeza kuwa alipata upinzani mkubwa kwa viongozi wa kimila na jamii kwa sababu katika  jamii nyingi za Afrika mwanamke haruhusiwi kutoa mawazo mbele ya jamii na yakakubalika, lakini kwa sababu alikuwa na dhamira ya kuwakomboa wananchi wa Kilwa kutoka katika umaskini kwa
kuanzisha kilimo cha kibiashara alifanikiwa na jamii  imebadili mtazamo hasi dhidi ya wanawake na kutambua kuwa mwanamke ni nguzo muhimu katika sekta ya kilimo.

Anasema wanatumia jembe la mkono ambalo kwa zama hizi halifai lakini wana mipango ya kutumia teknolojia mbadala ya kilimo ili kupata mazao mengi zaidi.

AMSHA imeingia mkataba na kampuni ya ALIGRAM kuzalisha tani laki moja za ufuta ambapo kampuni hiyo itatoa pembejeo muhimu kwa wakulima ili kuzalisha zao hilo.

Pia kutokana na mabadiliko ya hali hewa nchini hasa katika mikoa ya kusini, mvua zimepungua lakini katika msimu ujao wanatarajia kutumia kemikali ambazo huwekwa katika udongo ili kusaidia ukuaji wa mazao hata kama mvua ni chache.

Kutokana na faida inayopatikana katika kilimo, AMSHA imeandaa mradi mwingine wa kuwawezesha wakulima kujenga nyumba bora za bei nafuu.

Mradi huu unalenga kuboresha mazingira na makazi  ya wakulima ili wawe sehemu nzuri ya kuhifadhi mazao na kupata haki ya kuwa na nyumba zitakazoboresha afya zao na kuwa na uwezo wa kushiriki katika shughuli za kilimo kwa ukamilifu.

Anatoa wito kwa serikali na wadau wanaohusika na kilimo nchini kuitekeleza sera ya Kilimo Kwanza kivitendo, wananchi
na wakulima wengi bado hawana elimu ya kutosha kuhusiana na kilimo bora.

Taasisi ya AMSHA ni chachu na mfano wa maendeleo ya kilimo nchini, wakulima wadogo wadogo wakiamua kuungana na kufanya kazi kwa umoja mapinduzi ya kilimo yanawezekana.



No comments:

Post a Comment