19 September 2012

Kivumbi cha Ligi Kuu kuendelea leo: Huku Simba kule Yanga



Na Zahoro Mlanzi

LIGI Kuu ya Soka ya Tanzania Bara, inazidi kushika kasi ambapo leo kwenye viwanja saba tofauti nchini moto utawaka lakini macho na masikio yataelekezwa mkoani Morogoro na jijini Dar es Salaam.

Mechi za mikoa hiyo ndizo zitakazovuta hisia za mashabiki wengi kwani mabingwa wa Kombe la Kagame, Yanga itakuwa na kibarua kigumu mbele ya wenyeji Mtibwa Sugar huku mabingwa wa ligi hiyo, Simba ikiumana na JKT Ruvu.

Timu hizo kongwe za Yanga na Simba ambazo, zinajivunia udhamini wake mnonono kutoka kwa bia ya Kilimanjaro kila moja imesajili wachezaji wenye viwango kwa lengo la kufanya vyema katika ligi hiyo.

Yanga ambayo katika mechi ya kwamza iliyopigwa Mbeya ilitoka suluhu na Prisons huku Simba, ikianza ligi hiyo kwa kishindo baada ya kuifunga African Lyon mabao 3-0.

Mabingwa hao wa Kagame, watashuka kwenye Uwanja wa Jamhuri wakiwa na kumbumbuku ya kuchapwa bao 1-0 na timu hiyo lililofungwa na Kessy Mapande kwa mkwaju wa penalti msimu uliopita, hivyo mechi hiyo inatarajiwa kuwa na ushindani wa aina yake.

Katika mechi ya msimu uliopita, baada ya kipyenga cha mwisho kupulizwa kulizuka vurugu zilizodaiwa kufanywa na mashabiki wa Yanga na kusababisha askari kuziondoa kwa ulinzi timu hizo.

Yanga itashuka uwanjani ikiwategemea zaidi washambuliaji wake, Didier Kavumbagu, Hamis Kiiza na Said Bahanunzi ambaye msimu uliopita aliichezea Mtibwa hivyo atakuwa na kazi ya ziada kuziba masikio kutokana na mashabiki wa timu hiyo watakavyomzomea.

Kocha wa timu hiyo, Tom Saintfeit aliunzungumzia mchezo huo kwa kusema: "Hapendi kuona mashabiki wake wakiwa na huzuni, watajitahidi kuondoka na pointi tatu katika mechi hiyo licha ya Mtibwa kuwa ni timu nzuri.

Wakati Yanga ikijiuliza hayo, yenyewe Simba itakuwa na kazi moja ya kuendeleza wimbi la ushindi katika ligi hiyo na kuwadhihirishia mashabiki wao kama wana uwezo wa kutetea ubingwa wao.

Simba inayonolewa na Milovan Cikovic, inatarajia kuzianzisha bunduki zake Emmanuel Okwi, Mrisho Ngassa na Daniel Akuffor kuhakikisha inaondoka na pointi tatu muhimu na kuzidi kujikita kileleni mwa ligi hiyo.

Mechi ya mwisho kwa timu hizo kukutana, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo mabao yao yalifungwa na Uhuru Selemani, Haruna Moshi 'Boban' na Mwinyi Kazimoto.

Mechi zingine zitakazopigwa leo ni kati ya African Lyon itakayoialika Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Azam Coplex, ambapo Lyon itashuka uwanjani ikiwa na hasira ya kufungwa mabao 3-0 na Simba pamoja na kuzuiwa kutumia nembo ya mdhamini wao, Kampuni za simu ya Zantel.

Mkoani Pwani kwenye Uwanja wa Mabatini, wenyeji Ruvu Shooting wataialika Mgambo Shooting, ambapo timu zote zitashuka uwanjani zikiwa na machungu baada ya kupoteza mechi zao za kwanza kwa Ruvu kufungwa mabao 2-1 na JKT Ruvu na Coastal Union iliichapa Mgambo 1-0.

Huko Mbeya kwenye Uwanja wa Sokoine, Prisons itaikaribisha Coastal Union wakati kwenye Uwanja wa Kaitaba, mkoani Kagera, wenyeji Kagera Sugar wataumana na JKT Oljoro ya Arusha na kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza Toto African itacheza na Azam FC.

No comments:

Post a Comment