19 September 2012

Kila la kheri darasa la saba



LEO na kesho wanafunzi wa darasa la saba nchini kote, watafanya mitihani ya kumaliza elimu ya msingi.

Kwa mara ya kwanza watahiniwa hao watatumia tekinolojia mpya iitwayo Optical Mark Reader (OMR), ambapo fumu za majibu ya mitihani yao zitasahihishwa kwa kutumia kompyuta.

Jumla ya wanafunzi 894,881 wamesajiliwa kufanya mtihani huo kati ya hao, wavulana 426,285 sawa na asilimia 47.64 na wasichana 468,596 sawa na asilimia 52.36.

Kati ya hao wanafunzi 874,379 watafanya mtihani huo kwa lugha ya Kiswahili na 20,502 watafanya kwa lugha ya Kiingereza ambayo ndiyo waliyoitumia kujifunzia.

Wanafunzi 92 wasioona nao wamesajiliwa kufanya mtihani huo kati ya hao wavulana 53 na wasichana 39. Watahiniwa wenye uono hafifu wanaohitaji maandishi makubwa ni 495, kati yao wavulana 238 na wasichana 257.

Sisi tunasema kuwa, kuhitimu elimu ya msingi isiwe mwisho wa kuendelea na elimu ya sekondari hivyo ni wajibu wa kila mzazi na mlezi kuhakikisha watoto ambao watakosa nafasi za kuchaguliwa kidato cha kwanza katika shule za Serikali wanasoma shule binafsi.

Ni wazi kuwa, elimu ndio uti wa mgongo katika ulimwengu wa sayansi na teknolojia ndiyo maana nchi mbalimbali duniani, zimewekeza katika sekta hiyo ili jamii kubwa isome na kuitumia elimu waliyonayo kwenye harakati za maendeleo ya Taifa na kuboresha ustawi wa jamii.

Taifa ambalo lipo nyuma kielimu, linakabiliwa na hali ngumu ya maendeleo katika nyanja mbalimbali. Ni muhimu wazazi kuhakikisha elimu wanayopewa watoto wetu inakuwa bora na inakidhi mahitaji ya jamii husika.

Serikali na wadau wa sekta hii wanapaswa kuendeleza harakati za kuiwezesha jamii kubwa kupata elimu iliyojaa maarifa, ubunifu, ujuzi, ufundi wa aina mbalimbali na kuvumbua dhana mpya.

Hiyo ndio nguvu ya elimu inayoleta maendeleo katika jamii kwani Watanzania wengi wanaishi katika lindi la matatizo ambayo nchi nyingi waliyatatua miongo kadhaa iliyopita.

Hivi sasa, nchi zilizoendelea zinatafuta maarifa mapya ya kuibadili dunia wapendavyo kwa kurahisisha kila kitu kwa teknolojia hivyo suala la kuwekeza katika elimu bora haliepukiki bali linapaswa kutiliwa mkazo na kila mtu.

Ili nchi yetu ipige hatua ya maendeleo, ipo haja ya kila mwananchi kuona umuhimu wa kusomesha mtoto wake ili aelimike.

No comments:

Post a Comment