25 September 2012

Hukumu ya Mch. Mtikila kutolewa leo


Na Rehema Mohamed

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, leo  inatarajiwa kutoa hukumu ya kesi ya kuchapisha na kusambaza walaka wa uchochezi dhidi ya Rais Jakaya Kikwete inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila.


Awali mahakama hiyo iliahirisha kutoa hukumu hiyo mara mbili mfululizo kwa sababu mbalimbali ikiwemo ya hakimu aliyekuwa akiisilikiza Bw. Ilvin Mugeta, kuwa na majukumu ya kikazi.

Mara ya kwanza hukumu hiyo ilipangwa kutolewa Agosti 30 mwaka huu na kuahirishwa hadi Septemba 6 mwaka huu lakini ilisogezwa mbele na kupangwa kutolewa leo.

Katika kesi hiyo, Mchungaji Mtikila anadaiwa kuwa kati ya Januari 2009 na Aprili 17, 2010, jijini Dar es Salaam, kwa nia ya uchochezi, alisambaza kwa umma nyaraka zilizosomeka “Kikwete kuuangamiza ukristo', wakristo waungane kuweka mtu Ikulu”.

Katika utetezi wake, Mchungaji Mtikila alikiri kuandaa waraka huo na kusambaza nakala zaidi ya 100,000 nchini akidai kuwa, waraka huo si wa uchochezi bali unahusu maneno ya Mungu.

Mmoja wa mashahidi waliomtetea ambaye ni mwandishi wa habari Gazeti la Mwananchi, Bw. Mpoki Bukuku, alitoa kielelezo cha gazeti hilo la Agosti 6, 2009 ambalo lilikuwa na kichwa cha habari kinachosema “Mtikila apiga kampeni Kanisani kumpinga JK, achunguzwa na polisi kumwaga sumu Rais asichaguliwe 2010”.

Akitoa ushahidi wake, Bw. Bukuku aliieleza mahakama hiyo kuwa habari hiyo ilikuwa ikiripoti kilichotokea jijini Mwanza katika mkutano wa Maaskofu ili kuelimisha jamii.

Alidai anaamini habari hiyo haikuwa na tatizo lolote kwa sababu polisi hawajalalamika na kama ingekuwa na matatizo, huomba radhi au kufanya mapatano mengine.

Bw. Bukuku alisema habari hiyo ilikuwa inahusu mafundisho ya viongozi wa dini.

No comments:

Post a Comment