28 August 2012

Zao la pareto likiangaliwa upya litakuwa mkombozi kwa wakulima



Na Alfred Mwahalende

LICHA ya kilimo kuwa ni uti wa mgongo kwa watanzania wengi
bado kuna kusuasua kwa sera na utekelezaji wa mipango na mikakati inayohusu sekta hiyo.

Ni wazi kwamba asilimia kubwa ya watanzania  ni wakulima na wengi wao wanaishi vijijini ambako kuna  miundombinu
mibovu na kukosekana kwa soko la uhakika la bidhaa.

Asilimia 80 ya watanzania ni wakulima na wengi wao huishi vijijini ambako kuna maeneo mengi ya kufanyia kazi au kilimo yaani ardhi ya kutosha.

Hatuwezi kusema watu wote waishio kijijini ni wakulima bora
tu kwa sababu ya uwepo wa ardhi ya kutosha huku wengine kilimo ni msingi wa maisha na ajira kwao.

Hata hivyo wapo wakulima wanaolima kwa sababu ya njaa tu na wengine kwa ajili ya chakula na biashara. Aidha wapo wakulima ambao wamekata tamaa hivyo wanalima kwa sababu ya kudumisha utamaduni wao, watu hawa wanalima bila kuzingatia kanuni za kilimo, pembejeo na aina ya mbegu.

Kero kubwa kwa wakulima wetu ni kukosekana kwa sera bayana
zinazozungumzia  kwa kina na kuonyesha mchakato wa utekelezaji wa mipango inayohusiana na  sekta ya kilimo.

Pembejeo na vitendeakazi  ni changamoto kubwa kwa wakulima wadogo nchini kwa muda mrefu sasa, kuhimiza kauli ya kilimo ni uti wa mgongo tunawanyima wakulima fursa ya kikiona kama nguzo ya taifa.

Aidha soko ni changamoto kubwa kwa mazao ya watanzania walio wengi na kilio chao kwa serikali ni kuhakikisha wanapata soko la uhakika.

Serikali kupitia wizara na viongozi wa sekta ya kilimo
waangalie namna ya kumwezesha mkulima wa kijijini ili aweze kupata barabara nzuri zinazopitika msimu mzima wa mwaka, kadhalika soko la bidhaa za wakulima wa vijijini ziangaliwe kwa jicho la kuwanufaisha ili kuondoka na utabaka uliopo katika vipaumbele katika sekta zote.

Utafiti uliofanywa na Majira kufuatilia kwa kina faida na changamoto ya wakulima wengi wa zao la pareto ilibisha hodi katika Bodi  ya Pareto kwa nyanda za juu kusini.

Mtakwimu wa bodi hiyo nyanda za juu kusini Bw.Tumaini Ngojile anasema, wamiliki wa makampuni ya ununuzi wa pareto wanatakiwa kufuata taratibu zilizowekwa katika ununuzi ili kuwanufaisha wakulima.

Anasema taratibu zilizowekwa zikifutatwa zitasaidia kupata kupata mazao bora kwa faida ya mkulima ambaye kwa kiasi kikubwa ndiye anayeumia.

Anasema, taratibu hizi kuwa kukikisha kuwa wanakuwa na leseni ya kazi, kununua pareto inayoletwa kituoni na siyo kuifuata majumbani.

"Wanunuzi wanatakiwa kutekeleza makubaliano yao kwa kuweka vibao vya majina ya makampuni na bei rasmi za ununuzi kwa
siku husika ya soko," anasema.

Anasema, mizani zinazotumika zikaguliwe kabla ya kwenda kufanyia kazi ili kuepuka udanganyifu unaofanywa na
wanunuzi na kupiga marufuku kununua pareto mbichi kwani inalenga kuzooretesha ubora wa zao hilo.

Anayataja makampuni yaliyopewa kibali cha kufanya biashara  ya kununua pareto kuwa ni matano ambayo ni pamoja na Acto General business company limited, KATI General enterprisese, TABECO International limited, TARKIS phamermed limited and Pyrethrum company of Tanzania(PCT).

"Katika mkutano uliofanyika chuo cha kilimo uyole
tulikubaliana kwamba makampuni yatakayonunua  pareto kwa mwaka huu yahakikishe yananunua pareto yenye ubora na yenye sumu nyingi,".

"Bei elekezi ilikuwa ni 1800 kwa mwaka huu huku bei ya
juu ikiwa nia 2200, wito kwa wakulima na makampuni, wakulima wasikubali kuuza pareto kwa walanguzi kwani lengo lao siyo la kibiashara na badala yake wanalenga kuzoretesha zao hili," anasema.

Aidha makampuni yatakayobainika kulangua na kununua pareto majumbani sheria kali zinachukuliwa.

Wakati huohuo wakala wa kamapuni ya kununua pareto wa shirika la PCT Ilembo b, anadai kuwa kumekuwa na ugumu wa kazi  ya kununua pareto kutoka na na kwamba yapo makampuni yanayojihusisha na ulanguzi wa pareto  kwa kununua  majumbani badala ya kununua katika vituo husika.

"Kampuni ya  PCT imeendelea kufauta sheria zote za ununuzi cha kushangaza tunasikia kuna watu wananunua pareto majumbani badala ya kusuburi kwenye vituo, hawa wametufanya kukosa pareto katika vituo vyetu vya kununulia," anasema.

Anasema, kama kiwango cha pareto kitakuwa kizuri kwa mwaka huu wamedhamilia kufikia Tsh 2300 juu ya kiwango walichokubaliana na bodi ya pareto nyanda zajuu.

Anadai kuwa fedha zimemwagwa kilichobaki wanasubiri wakulima kupeleka pareto yenye ubora wa kukidhi soko.

Mmoja wa wakulima hao, Bi. Mbushi Buli ambaye alitajwa na wakala wa bodi ya ununuzi wa pareto ya kampuni ya PCT kuwa mkulima bora wa pareto kwa ukanda wa Umalila anasema zao hilo limempa faida kubwa lakini kero ni kutofautiana kwa bei za pareto na vipimo kati ya kampuni moja na nyingine hali inayompa wasiwasi wa kuendelea kunufaika na zao hilo pekee.

"Nilianza kilimo cha pareto miaka ya 1980 nikiwa kijana mdogo kutokana na shauku ya kutaka kuwa mkulima bora,".

Anasema, hakuna kitu muhimu kama kilimo duniani, kwani hakuna
jamii yoyote inayoweza  kuishi bila chakula na chakula ni msingi wa uhai wa mwanadamu.

Aidha kilimo ni uti wa mgongo wa taifa letu, kama
huu ndiyo ukweli wa mambo lazima jamii na taifa iangalie njia mbadala ya kuhakikisha suala la kilimo linatiwa mkazo ili kujikwamua kimaisha.

Anasema, suala la usafiri limekuwa kero kwa wakulima wengi kwani wao wanalima mazao mengi mbali na miji ambako hakuna usafiri na badala yake wanabeba mazao kichwani.

Anatoa wito kwa wakulima kuzingatia kanuni za kilimo ili kupata pareto nzuri aidha anasema pareto nzuri ni ile iliyovunwa kwa kuzingatia muda maalumu, kukaushwa vizuri angalau siku nne, na sehemu isiyo na vumbi na kuuza mara baada ya kukauka ili kuepusha kupungua kwa sumu.

Anasema faida wanazozipata kutokana na zao la pareto kuwa ni pamoja kupata fedha za kuendesha maisha ya kila siku, pia kutunza chakula kwani kwa muda mrefu waliuza mazao ya chakula kujikimu kimaisha.

Anasema, tatizo kubwa kwa wakulima wa pareto kuyumba kwa bei,
udanganyifu katika vipimo (mizani), utunzaji mbaya na mabadiliko ya hali ya hewa, ukausha, uvunaji chini ya kiwango vinachangia kushuka kwa bei.

Pia alilalamikia kitendo cha baadhi ya watu wanazunguka
majumbani kukusanya pareto huku wakinunua bila mizani na bei tofauti tofauti.


Zao la pareto likiangaliwa upya litakuwa mkombozi kwa watanzani waisho vijijini ambao kwa kiasi kikubwa ajira yao ipo katika kilimo ambayo ni uti wa mgongo wa Tanzania na tutaondokana na  umaskini ambao umechangia kuzorota kwa shughuli za maendeleo ya taifa.

No comments:

Post a Comment