28 August 2012

Jitihada zinahitajika kuukomboa ushirika Mtwara


Na Cornel Antony

SHERIA ya ushirika ni mwongozo uliopo kisheria ambao umepitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kupewa kibali kwa kusainiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa mujibu wa kifungu cha 131 cha sheria ya ushirika Na.20 ya 2003 Waziri mwenye dhamana ya Maendeleo ya Ushirika baada ya kushauriana na Mrajis wa Vyama vya Ushirika, anatengeneza Kanuni za Vyama vya Ushirika ambazo zinakuwa ni sehemu ya
Sheria ya Ushirika.

Kanuni ni tafsiri ya kina ya vipengele mbali mbali vya Sheria. Sheria ya Vyama vya Ushirika Na 20 ya 2003 pamoja na kanuni zake za 2004 zilianza kutumika rasmi Agosti, 2004.

Pamoja na kanuni Mrajis pia anaweza akaandaa Waraka pale inapobidi ili kufafanua baadhi ya mambo ambayo anaona yanahitaji ufafanuzi zaidi na waraka huo kuwa ni sehemu ya miongozo inayotambilika kisheria.

Wahenga walisema kila shetani na mbuyu wake, hii ni kweli kwani kila mtu na fani yake aliyojaliwa na Mwenyezi Mungu sio kila mtu kujiingiza au kuingilia fani isiyo ya taaluma yake.

Nchini tabia ya kuingilia madaraka na fani asiyoweza imekuwa kama utamaduni ambapo hata kama hawezi fani ama kazi flani lakini kwa kutaka sifa atajipenyeza au kulazimisha au kwa kutumia madaraka yake kufanya ili apate sifa tu kwamba anaweza.

Mara nyingi maeneo yanayoingiliwa hukumbwa na matatizo ya kuuwa mradi au taasisi kutokana na kukosekena kwa ubunifu na ujuzi wa wasimamizi.

Hali hiyo imesababisha baadhi ya miradi kutofanikiwa na kurudisha nyuma nyuma maendeleo.

Leo tuelekeze macho na masikio yetu katika ushirika wa Tanzania ambao una umri wa mtu mzima tena na mjukuu lakini mpaka leo imekuwa kichekesho kwani tumebaki pale pale miaka mingi sasa.

Ni kweli tumefika hapa kutokana na uzembe wa watendaji wachache, lakini ni kweli hatuwezi kufika panapohitajika?

Tuna kila sababu ya kufika kwani wataalmu wa kutosha wenye moyo wa uzalendo na wenye vipaji vya hali ya juu walivyopata katika vyuo mbali mbali vya ushirika vya ndani na nje ya nchi.

Lakini wataalamu hawa wameweza kutafsiri na kujenga ushirika kwenye maeneo mengi ya nchini.

Changamoto inayovikumba vyama vya ushirika nchini ni kuingiliwa na siasa huku wakimuumiza mkulima.

Ushirika na siasa ni vitu viwili tofauti ambavyo haviendani kwani kukifuata hicho ndio chanzo cha kufa kwa vyama vya ushirika  na kudidimiza ukuaji wa sekta hii muhimu kwa maendeleo ya wananchi wa vijijini.

Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliweka mkazo wa kwanza kwenye ushirika kwakua ni dira ya maendeleo ya mwananchi wa ngazi ya chini na mwanzo wa maisha bora.

Leo tumeshuhudia viongozi wa vyama vya ushirika wakikumbana na matatizo mbalimbali yakiwemo kuchomewa moto nyumba zao au kuharibiwa mali zao na wengine kupewa adhabu zisizo stahili.

Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika cha TANECU (LTD) Limited Bw. Yusuf Nannilah, anaiomba serikali iingilie kati juu ya mwenendo mzima wa ushirika kwani umeshaanza kuvurugwa na wanasiasa ili wapate umaarufu.
           
"Ushirika ni vikundi vya hiari ambavyo tumeunda kwa hiani yetu bila shuruti yoyote lakini cha ajabu tunawaona wanasiasa wakijipenyeza na kuanza kutuongoza," anasema Bw. Nannilah.

Anasema, wapo viongozi wa ushirika katika ngazi ya wilaya Mkoa, Taifa hadi dunia cha kushangaza wanaingiliwa na watu wasiojua ushirika wala sheria zake pengine viongozi wakuu wa serikali kupiga hodi kwenye ushirika badala ya kusimamia wao hutoa maamuzi ya mwisho.

"Matarajio yangu ni serikali kuliangalia hili kwa mapana zaidi ili kuruhusu ushirika bila kuingiliwa na watawala wasiojua sheria na kanuni zake, anasema Bw. Nannilah.

Awali ushirika ulianza kupata mafanikio mwanzo ukaja ukafa lakini Rais Jakaya Kikwete alirudisha heshima yake kwa kulipa madeni makubwa yalikuwa yanaukabili.

"Leo ushirika una kila sababu kujivunia kwa kujenga uchumi mzuri kwa kupandisha bei ya mazao ya biashara kama vile ufuta, korosho, pamba, kahawa na mengine mengi," anasema.

Anasema, hali hiyo inatokana na wakulima kuungana kwa pamoja na kupinga unyonyaji kwa mazao ya wakulima na kutengeneza na mfumo mmoja wa stakabadhi mazao ghalani hivyo kufanya bei kuwa ya umoja .

Kwa upande wake meneja mkuu wa TANECU Bw. Daimu Mpakate anasema mfumo wa stakabadhi wa maghala umeweza kuinua kipato cha wakulima na kuboresha maisha yao baada ya kupata kipato cha ziada.


Mfumo wa stakabadhi ghalani ulianzishwa kisheria (sheria Na. 10 ya 2005), kwa kutumia mazao kwenye maghala kama dhamana ya kupata mkopo kutoka kwenye benki na asasi zingine za fedha.

Tangu msimu huu ulipoanza kumekuwa na mafanikio makubwa kwa wakulima, vyama vya msingi na kwa halmashauri ya wilaya kwa ujumla.

Kwa kiasi kikubwa umepunguza tatito la u ambao uliyumbisha bei na soko kiasi cha kukatisha tamaa uzalishaji wa korosho kupunguza ushuru.

Anasema, zaidi wananchi wa vijijini wameweza kuelewa mafanikio na maana ya kuwa na ushirika kwenye maeneo yao wanayoishi.
              
"Kwa mfano sisi Tanecu tumeweza kuhudumia vyama 104 vya Wilaya ya Tandahimba na Newala vikipata mafanikio makubwa kuanzia mtu mmoja mmoja asiye mwana chama mpaka mwanachama wa ushirika," anasema.

"Ni matumaini yangu kwamba sisi wana Tanecu tunafanya mapinduzi makubwa  ya kuweza kufanya kutoka kwenye ushirika kwenda kwenye makampuni.

Chama kikuu cha ushirika cha Tanecu ni mfano bora wa kuigwa nchini ni Chama cha kwanza cha Ushirika chenye uwezo mkubwa wa kujiendesha chenye uchumi ulioimarika.

Ni chama chenye viongozi makini wenye uwezo moyo wa uzalendo wa kuweza kuongoza ushirika wa uaminifu mkubwa kwa jamii ya inayowazunguka bila kuingiliwa na wanasiasa wanakuwa ni mfano wa kuigwa.

Ni matumaini yangu kwamba serikali sikivu au kiongozi mwenye busara hawezi kukurupuka na kutoa amri ya utekelezaji ndani ta siku  saba. Inatakiwa kukaa na viongozi wa ushirika watatu wa msingi na wilaya mpaka Mkoa ili kujua matatizo na kusuluhisha.

  


No comments:

Post a Comment