29 August 2012

Ushuru utumike kuboresha miundombinu sokoni



Na Lulu Malenda

MIUNDOMBINU ni sekta muhimu inayotakiwa kupewa kipaumbele ili kuongeza kasi ya maendeleo.

Nchi zilizoendelea zimewekeza katika miundombinu ambayo ndio kitovu cha sekta zote kwani kila kitu hutegemea usafiri ili kufika sehemu husika.


Hakuna nchi iliyoendelea huku wazalishaji wakiwa katika mazingira mabovu na kushindwa kusafirisha bidhaa vizuri.

Katika hali isiyokuwa ya kawaida masoko mengi ya bidha nchini yanaongoza kwa miundombinu chakavu na sehemu nyingine hakuna huku kodi zikikusanywa kila siku.

Ni dhahiri kwamba miundombinu iliyopo haikidhi mahitaji husika kwa watumiaji wake japokuwa wafanyabiashara wanapolipa fedha hizo hazitumiki ipasavyo.

Uduni wa miundombinu sokoni unahatarisha afya za raia kwa kiasi kikubwa kwani kinga ni bora kuliko tiba.

Nionavyo, kutokana na mazingira ya uchafu sokoni kuwa chanzo cha maambukizi ya magonjwa mbalimbali kama kipindupindu, matumbo ya kuhara ni vyema wahusika wakaanza sasa kurekebisha kasoro zilizopo.

Mitaro mingi katika soko la kariakoo imeziba na haifanyiwi usafai mara kwa mara hali inayosababisha harufu mbaya unapokuwa sokoni hapo.

Hali huwa mbaya kipindi cha mvua kwani kila sehemu hutapakaa maji machafu  ambayo hukosa sehemu ya kwena kutokana na uchakavu wa mifereji.

Hali hii alaumiwe nani? Kuna kila sababu ya kuwajibishana hususan kwa wanaokusanya kodi katika masoko hayo.

Pia suala la vyoo ni muhimu kuongezwa ili kupunguza uchafu pembezeni mwa maduka kutokana na idadi kubwa ya watumiaji.

Vinatakiwa kuwa katika ubora unaostahili ili kutumika kwa muda mrefu na kufanyiwa usafi kila mara.

Kinachoshangaza ni kuona wafanyabiashara wanalipa ushuru lakini hawajengewi miundombinu inayoridhisha. Hii inaonyesha dhahiri kwamba fedha hizo hazitumiki ipasavyo ama ushuru unaotozwa ni mdogo haukidhi mahitaji.

Nionavyo katika kila soko kuwe matanki ya maji ya kutosha kulingana wingi wa watu na mahitaji ya soko. Maji hayo yatafaa kwa matumizi ya wafanyabiashara, usafi wa mazingira ya soko na katika matumizi ya vyoo.

Je, hakuna mabwaba afya? Kama tunao mbona masoko hayapo katika hali ya usafi? Hayo ni maswali ninayojiuliza na kukosa majibu.

Serikali za mitaa tunazo tena zilizo hai je, wizara husika haioni tatizo hili? Tunaomba mabwana afya wawe wanapita mara kwa mara kukagua hali ya usafi na kuwalipisha faini wanaokaidi amri zinazowekwa.

Serikali za mitaa inabidi ziwajibike kikamilifu kulinda afya za raia wake kwa kusimamia na kuwaongoza wafanyabiashara wanaotumia soko husika.

Hii ni pamoja na kutoa elimu ya usafi wa mazingira na kutoza faini kubwa au kuwashitaki wataoenda kinyume na sheria.

Kila manispaa iandae mapipa ya taka na magari ya kutosha ya kubebea taka ngumu na kupeleka katika madampo yaliyoandaliwa na jiji. Pia  yawe yanapita mara kwa mara ili kuepusha mlundikano wa taka kwa muda mrefu sokoni ambapo huleta adha kubwa kwa wananchi wanaolizunguka soko na hatari ya milipuko wa magonjwa.

Hata kama ni gharama kubwa kutengeneza miundombinu ya soko, basi ni vema kuboresha miundombinu iliyopo ifikie kiwango kinachotakiwa ili kulinda afya za watumiaji.

Si hivyo tu, uongozi mzuri ndio kiini katika uendeshaji wa soko bora na si bora soko. Hivyo nashauri kuwe na uongozi utakao simamia mazingira ya soko na shughuli zinazoendeshwa sokoni.

0714504393

No comments:

Post a Comment