29 August 2012
Malinzi kuzindua Rock City Marathon
Na Mwandishi wetu
MICHUANO ya mbio za Rock City Marathon 2012, inatarajia kuzinduliwa leo jijini Dar es Salaam.
Mbio hizo zitanduliwa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Taifa Deoniz Malinzi na baadae washiriki watapata fursa ya kujaza fomu za maombi ya kushiriki.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mratibu wa mbio hiyo, Grace Sanga alisema maandalizi ya uzinduzi huo yanaendelea vyema na kuwataka wadau wa michezo watarajie maboresho makubwa kwa mwaka huu.
Alisema mashindano hayo yanadhaminiwa na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), African Barrick Gold, Nyanza Bottlers na Mfuko wa Pensions (PPF).
Aliwataja wadhamini wengine kuwa ni Geita Gold Mine, TANAPA, Sahara Communication, ATCL, New Mwanza Hotel, Airtel na New Africa Hotel.
Alisema mbio hizo zinatarajia kufanyika Oktoba 28, mwaka huu katika Uwanja wa CCM Kirumba na kushirikisha mbio za marathon, nusu marathon na mbio za kujifurahisha (Fun Race 5Km).
Mratibu huyo alisema pia kutakuwa na mbio za walemavu za kilomita 3, mbio za watu wazima za kilomita 3 na mbio za watoto kuanzia miaka saba hadi 10 za kilomita 2.
"Tunashukuru kampuni ambazo zimejitokeza kudhamini mbio hizi, tunaziomba kampuni nyingine kujitokeza kutusapoti na kuwa karibu na wateja wao," alisema.
Mashindano hayo yanafanyika kwa mwaka wa nne sasa tangu mwaka 2009, ambayo lengo lake ni kuibua vipaji na kutangaza utalii wa ndani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment