07 August 2012
Tanzania kujaribu tena bahati yake leo Olimpiki
Na Amina Athumani
TANZANIA itaingia tena leo katika kibarua kigumu cha kusaka medali katika michezo ya Olimpiki ambapo mwanariadha Zakia Mrisho atajitupa uwanjani katika mbio za meta 5,000.
Zakia ataingia uwanjani kusaka nafasi ya kuingia hatua ya robo fainali ya michuano ya riadha kwa wanawake ambapo katika kila kundi la wanawake watakaokimbizwa leo litatakiwa kutoa wanadada watatu kusonga hatua inayofuata.
Akizungumza kwa simu akiwa jijini London, Uingereza jana yanapofanyikia mashindano hayo, kocha wa timu ya ngumi za ridhaa ambaye yupo nchini humo na kikosi hicho Remmy Ngabo alisema Zakia ataingia uwanjani majira ya saa 5 hadi 5:30 asubuhi kwa saa za London.
Alisema katika ratiba yao inaonesha wanariadha hao watapangwa katika makundi ambapo kila kundi litatoa washindi wa kwanza hadi wa tatu kusonga hatua inayofuata.
Alisema kwa wanariadha watakaovuka hatua ya robo fainali watacheza hatua hiyo Agosti 8 na Agosti 9 watacheza nusu fainali na Agosti 10, zitakuwa fainali za meta 5,000.
Alisema kila mwanariadha ana ari ya kufanya vizuri katika mbio hizo na kwamba kwa upande wa Zakia amejipanga vyema na yupo katika hali nzuri ya kiushindani.
"Kama desturi yetu Watanzania hatuko nyuma katika kuombeana mema, hivyo basi Watanzania waendelee kutuombea dua kwani kwa sasa mchezo tuliobaki nao kama Watanzania katika mashindano haya ya Olimpiki ni riadha pekee mingine yote tumeshatolewa,"alisema Ngabo.
Alisema kwa upande wa wanariadha wengine wa Tanzania Samson Ramadhan, Faustine Mussa na Msenduki Mohamed wenyewe wataingia uwanjani Agosti 12, mwaka huu katika mbio ndefu za Marathon za kilometa 42.
Ikumbukwe kwamba ingawa zipo nchi nyingi mpaka sasa zimejizolea medali zaidi ya 50 ikiwemo China yenye medali 61 na Marekani yenye medali 60 katika michuano hiyo kwa Tanzania bado hatujafanikiwa kupata medali hata moja mpaka sasa.
Hadi sasa wanamichezo waliotolewa ni wa tatu ambao ni bondia Selemani Kidunda, Amar Gadiyali na Magdalena Mushi ambao ni waogeleaji.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment