21 August 2012

Pembejeo za uhakika ni muhimu kufanikisha kilimo kwanza



Na Cresensia Kapinga

MKOA wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa inayozalisha mahindi kwa wingi huku wakulima wakiendelea kutumia jembe la mkono.

Zaidi ya asilimia 70 ya Waafrika wanaishi vijijini huku shughuli yao kubwa ya kiuchumi ikiwa ni kilimo.


Licha ya kuwa tegemeo la kuzalisha chakula nchini, bado miundombinu ya kusafirisha mazao shambani na soko la uhakika kwa mazao hayo ni gumu hali inayozidisha ugumu wa maisha.

Unatakiwa mtazamo mpya wa kilimo hivi sasa kuangalia ni kubadili kilimo cha kiwango kidogo cha uzalishaji na kilicho nyuma kuwa cha kisasa.

Kila mwaka kumekuwa na ongezeko kubwa katika uzalishaji wa kila zao na hususan uzalishaji wa nafaka na hasa mahindi ambayo kwa Mkoa wa Ruvuma siyo tu zao la kuu la chakula bali ni la biashara.

Tanzania kuna ekari 29 milioni zinazoweza kutumika kwa kilimo cha umwagiliaji lakini ni ekari 300,000 tu zinazomwagiliwa kwa sasa.

Kilimo nchini kiko nyuma kwa sababu ya kutegemea zaidi mvua za msimu ambazo mara kwa mara zimekuwa hazikidhi mahitaji na kutokutoa fursa ya kutumika kwa rasilimali zilizopo kama ardhi kwa kipindi cha mwaka mzima huku ardhi inayoweza kutumika kwa umwagiliaji ikiwa kubwa.

Hivi karibuni Mkuu wa Mkoa huo, Bw.Said Thabiti Mwambungu ulifanya uzinduzi wa kampeni ya kimkoa ya matumizi ya matrekta makubwa katika kilimo ambayo ilizinduliwa na Waziri Mkuu, Bw.Mizengo Pinda katika viwanja vya Zimamoto Manispaa ya Songea.

Katika kampeni hiyo, Bw.Mwambungu anasema kuwa kilimo ndiyo sekta ya kutegemewa na wananchi wa mkoa huo ambapo zaidi ya asilimia tisini ya watu wa mkoa huo wanategemea kilimo kama chanzo cha mapato.

Anasema, kila mwaka kumekuwa na ongezeko kubwa katika uzalishaji wa karibu kila zao na hususan mahindi ambayo kwa mkoa huo siyo tu zao kuu la chakula bali pia ni la biashara.

Bw.Mwambungu anasema kwamba ukiondoa Wilaya ya Tunduru ambayo kiasi cha mahindi kinacholimwa ni kwa matumizi ya chakula zaidi, wilaya nyingine katika mkoa huo ni zao la chakula na biashara.

Anasema kuwa licha ya mahindi mazao mengine makubwa ya biashara ni korosho kwa Wilaya ya Tunduru, tumbaku -Namtumbo na Songea Vijijini,  kahawa Wilaya ya Mbinga pamoja na Wilaya ya Nyasa ambako imeinua uchumi wa wananchi wake.

"Mazao mengine yalimwayo sana mkoani mwetu licha ya mahindi, korosho tumbaku na kahawa ni pamoja na maharage pamoja na mpunga na nia ya mkoa kuona kwamba zao la mpunga linakuzwa na kuwa zao jingine kubwa la biashara kwa wilaya zote."anasema Bw.Mwambungu.

Anasema wakati mahitaji ya chakula kimkoa kwa mwaka ni tani laki tatu uzalishaji halisi wa mahindi kwa msimu wa 2010/2011 ulikuwa tani 520,587 na msimu wa 2011 /2012 uzalishaji umepanda na kuwa tani 535,653.

Anaeleza kuwa mafanikio hayo katika sekta ya kilimo kwa kiasi kikubwa yametokana na ari na utayari wa wananchi wa mkoa huo kushiriki kilimo bila kusukumwa kwani kilimo kimo katika damu yao.

Anasema, changamoto kwa wakulima ni upatikanaji wa pembejeo kwa wakati unaostahili na kwa ubora unaotakiwa.

"Wakulima wengi wanategemea kilimo cha jembe la mkono na nguvu za mwili kwa zaidi ya asilimia tisini hali hiyo ndiyo inayowafanya wabuni wazo la kuanzisha kampeni maalum ya matumizi ya matrekta makubwa katika kilimo ili kurahisisha kazi na kuongeza uzalishaji," anasema.

Anasema lengo la mkoa ni kupata matrekta 100 na tayari wameanza na matrekta 75 ambayo  yametoka katika Shirika la SUMA JKT na kufanikisha lengo hilo kwa asilimia 75.

Akizindua kampeni hiyo Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda  anasema kuwa kampeni hiyo ni nzuri kwani inaunga mkono jitihada za kilimo kwanza ambayo ndiyo sera ya serikali katika kuinua sekta ya kilimo.

Anasema kuwa juhudi ambazo wanaonesha katika kilimo ndizo zilizoufanya mkoa huo ukaongoza kwa ujenzi wa nyumba bora nchini.

Anawataka wananchi kujitokeza kwa wingi kununua matrekta hayo ambayo yanakopeshwa  kwa bei nafuu ndani ya miaka minne na kwamba bei ya matrekta hayo yamepunguzwa na vifaa vyake ili kutoa fursa kwa wananchi kukopa hivyo kwa wale wenye nia na dhamira nzuri wanatakiwa kukopa ili kuunga mkono jitihada za serikali katika kilimo kwanza.

Anatoa onyo kwa halmashauri za mkoa huo kupunguza vizuizi kipindi cha mavuno kwani vimekuwa kero kwa wakulima ambao wanatoa mazao yao mashambani na kuyapeleka sokoni badala ya kufuatwa shambani.

Mkoa wa Ruvuma umezindua matumizi ya matrekta ili kuinua kilimo kiwanufaishe wakulima kiuchumi kwa kutumia vifaa vya kisasa.

Mpango huo utasaidia pia kuongeza pato la Taifa kwa kuuza mazao nje ya nchi fedha zitakazoboresha miundombinu.

Kikwazo kikubwa katika utekelezaji wa kilimo kwanza ni ucheleweshaji wa malipo ya fedha zao pindi wauzapo kwa Wakala wa ununuzi wa mahindi.

Serikali inatakiwa kusimamia kwa makini suala la mbolea na mbegu ili kudhibiti matumizi ya mbolea na mbegu zisizo kuwa  na viwango.

Ili kufanikisha sera ya kilimo kwanza ni lazima serikali ishirikiane kwa karibu na sekta binafsi, wakulima wadogo na wakubwa pamoja na ushirikiano thabiti kati ya sekta ya umma na binafsi.



No comments:

Post a Comment