29 August 2012
Mwakyembe ataka uundwaji tume kuboresha usafiri wa reli
Na Stella Aron
TANZANIA inakabiliwa na hali mbaya ya usafiri wa reli hivyo Serikali inapaswa kuunda kamati ambayo itatoa mapendekezo yatakayoboresha usafiri huo nchini.
Mwenyekiti wa Kamati ya Marekebisho ya Sera ya Usafirishaji nchini, Mhandisi Malima Bundala, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya Waziri wa Uchukuzi, Dkt. Harrison Mwakyembe, kufungua warsha ya siku mbili kwa kamati hiyo.
Alisema kamati hiyo ilipewa majukumu ya kufanya marekebisho ya sera hiyo na kubaini kuwa hali ya usafirishaji kwa njia ya reli ni mbaya.
“Hali ya usafirishaji kwa njia ya reli ni mbaya sana hivyo tunaandaa sera ambazo zitapelekwa serikalini zikafanyiwe marekebisho katika sekta ya usafirishaji majini, reli, barabara na anga,” alisema.
Aliongeza kuwa, sekta ya reli inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo uvamizi wa njia zake na kukosekana wawekezaji.
Kwa upande wake, Dkt. Mwakyembe alisema Serikali inasubiri sera hizo ili iweze kuzifanyia kazi kwani zitaweza kutumika katika kipindi cha miaka 50 kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
Akijibu swali linalohusu hatua ya Serikali kuagiza vichwa vya treni kutoka nje kwa ajili ya kuboresha sekta hiyo, Dkt. Mwakyembe alisema Serikali imelazimika kuongeza posho kwa wataalamu waliopo nchini ili kuvifanyia matengenezo vichwa hivyo.
“Tumebaini kuwa gharama za ukodishwaji vichwa hivi ni kubwa, tuliagiza vichwa 13 kwa ajili ya kuboresha usafirishaji wa reli, tulitarajia kukodisha vichwa 18, lakini tumeshindwa kutokana na gharama kubwa hivyo tumeamua kuongeza posho kwa wafanyakazi wetu mkoani Morogoro ili wavifanyie matengenezo,” alisema.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment