29 August 2012

Elimu ya kujitambua itakomesha tatizo la mimba kwa wanafunzi


TATIZO la mimba kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini, linachangia kurudisha nyuma maendeleo ya elimu.

Takwimu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi zinathibitisha kuwa tatizo hili limekuwa likiongezeka siku hadi siku hasa baada ya kuanzishwa shule za kata.


Pamoja na shule hizo kupunguza tatizo la wanafunzi kukosa nafasi za masomo, bado zinakabiliwa na changamoto nyingi.

Miongoni mwa changamoto hiyo ni tatizo la mimba kwa wanafunzi ambao wengi wao hulazimika kukatisha masomo, uhaba wa vifaa, vyumba vya madarasa, walimu na madawati.

Tafiti mbalimbali zimebaini kuwa, tatizo la mimba kwa wanafunzi hasa wa sekondari ni kubwa na linagusa hisia za kila mpenda maendeleo.

Jambo la kusikitisha jamii kubwa bado haijahamasika kutoa ushirikiano wa karibu kwa vyombo vya dola ili kuwafichua wahusika wa vitendo hivyo.

Baadhi ya wazazi hupokea rushwa kutoka kwa watuhumiwa ili wasifikishwe katika vyombo vya sheria na kuchukuliwa hatua stahiki ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia za aina hiyo.

Sisi tunasema dhamira yetu ni kuona wazazi wanashirikiana na vyombo hivyo kuhakikisha watuhumiwa wanakamatwa ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

Kama jamii itaona umuhimu huu, Tanzania yenye wasomi wazuri waliobobea katika fani mbalimbali itawezekana na maendeleo yatakuwa kwa haraka.

Kitendo cha jamii kuendelea kuwaficha wahusika wa vitendo hivi, kinarudisha nyuma juhudi za Serikali na wadau wa elimu kuhakikisha mtoto wa kike anapata elimu bora.

Imani yetu ni kwamba, uwajibikaji wa viongozi wa vyama na Serikali unahitajika kwa kuhamasisha jamii iboreshe maendeleo ya elimu hasa kwa mtoto wa kike na kukomesha tatizo la mimba.

Umefika wakati wa wanafunzi wetu, kupewa elimu ya kujitambua na kufahamu wajibu walionao kwa jamii na Taifa ili waweze kujithamini na kuepuka vishawishi vinavyoweza kusababisha wapate mimba au kuacha shule.

Elimu ni nyenzo muhimu kwa maendelo ya Taifa lolote duniani kwani mapinduzi mengi ya maendeleo, hutegemea kiwango cha elimu kwa jamii husika.

No comments:

Post a Comment