20 July 2012

Mkakati mpya unahitajika kuepusha vifo vya mama na mtoto



Na Jesca Kileo

TANZANIA ni miongoni mwa nchi duniani ambazo zinatekeleza mpango wa kukabiliana na kutokomeza maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa UKIMWI kwa watoto.

Kupitia kauli mbiu ya taifa ya kuwa "Tanzania bila ya UKIMWI inawezekana" nchi imeweza kupiga hatua ya kudhibiti maambukizi kwa kiasi kikubwa.


Kufuatia taarifa iliyotolewa na Kaimu katibu mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Bi.Regina Kikuli ilionyesha kuwa maambukizi yanapungua kutoka asilimia 7.1 mwaka 2003 hadi kufikia asilimia 5.7 mwaka huu.

Bi. Kikuli anasema kuwa licha ya kuwapo kwa mafanikio hayo lakini bado kuna maambukizi kwa asilimia 6.9 katika kundi la wanawake wajawazito.

Anasema kuwa nchi inakadiriwa kuwa na watoto 120,000 wanaoishi na maambukizi ya VVU ambapo tayari watoto 78,000 wameweza kufikiwa na kupewa huduma.

Anasema kuwa bado mchakato unaendelea wa kuwafikia watoto wengi ili kuweza kudhibiti na kutokomeza maambukizi kwa watoto nchini.

Anasema kama wizara inatoa elimu ya kutambua watoto wenye maambukizi mapema na kuwapeleka kwenye huduma za tiba na matunzo ambazo zinatolewa nchini.

Bi. Kikuli anasema kuwa wizara yake itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha huduma za kuzuia maambukizi kwa watoto zinapatikana na kutolewa katika vituo vya afya nchini kote.

"Dawa za kutosha zinapatikana pamoja na kusambazwa katika vituo vya kutolea huduma ya afya nchini," anasema Bi. Kikuli.

Anasema kuwa wizara inafanya mkakati wa kupanua huduma kwa watoto wanaoishi na VVU ili kuifikia jamii kwa karibu zaidi na kutolewa bila ya usumbufu.

Anasema kuwa makongamano mbalimbali jamii inapata fursa ya kuelewa, kuelimisha na kutambua njia nyingine zinazoweza kusababisha maambukizi kwa watoto ikiwa ni pamoja na kukata kimeo, kuchanja kienyeji kwa kutumia vifaa visivyo salama, kubakwa pamoja na kuongezwa damu yenye maambukizi.

Bi. Kikuli anasema kuwa makongamano yanasaidia kutoa fursa kwa wataalamu kutathimini mwelekeo wa jitihada za serikali na za kimataifa katika harakati za kutokomeza maambukizo na ugonjwa wa UKIMWI kwa watoto.

Anasema kuwa jitihada hizi zinasaidia kupambana na maambukizi mapya ya VVU kwa watoto pamoja na kutanua wigo wa ubora wa huduma zinazotolewa na wizara.

Hata hivyo anasema kuwa shirika lisilo la kiserikali la Elizabeth Glaser Pediatric AIDS Foundation (EGPAF)  linashughulika na kupambana na maambukizi ya ugonjwa huu kwa watoto sambamba lilishirikiana na wizara.

EGPAF lilianza kutekeleza mipango ya VVU na UKIMWI nchini mwaka 2003 na kufungua ofisi yake nchini mwaka 2004.

Hadi kufikia machi 31 mwaka huu, EGPAF imeweza kusaidia upatikanaji wa huduma za kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ijulikanayo kama (PMTCT) katika vituo 1,280 vya huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU na UKIMWI katika vituo 165 katika Mikoa yote inayofanya kazi nchini.

EGPAF inatekeleza mipango ya (PMTCT) pamoja na huduma za afya ya uzazi na mtoto (RCH) katika mikoa sita ya Lindi, Mtwara, Kilimanjaro, Arusha, Tabora na Shinyanga.

Hata hivyo kuna huduma za tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU katika mikoa ya Lindi, Tabora, Arusha na Kilimanjaro na mpango wa kuwahudumia wagonjwa wa majumbani katika mikoa minne ambayo ni Mwanza, Zanzibar, Pwani na Tabora.
 
Mkurugenzi Dkt.Jeroen Bosch kutoka shirika la EGPAF anasema kuwa utoaji mzuri wa huduma mpya za kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ni njia muhimu itasaidia kutokomeza tatizo la VVU kwa watoto nchi nzima.

Anasema kuwa tangu mwaka 2003 hadi mwaka huu shirika hilo limewezesha kusimamia wanawake 1,827,052 kupewa ushauri nasaha na kupimwa ambapo kati ya hao 75,383 walikuwa na virusi vya UKIMWI na 65,810 walipewa kinga ya kuzuia maambukizi kwa watoto.

Anasema kuanzia mwaka 2003 hadi kufikia Machi 31, mwaka huu wamewezesha uandikishaji wa watu wanaoishi na VVU 177,298 wakiwemo watoto 15,007 walio chini ya umri wa miaka 15 katika vituo vya tiba ambapo miongoni mwao walioanzishwa dawa ni 94,057 wakiwemo watoto 8652 chini ya umri wa miaka 15.

Dkt. Bosch anasema mkakati huu unaweza kufanikiwa kwa kuhakikisha kila mama mjamzito anapata taarifa sahihi kuhusu upatikanaji wa huduma hizi na pia ni muhimu wajawazito  kufikiwa na huduma za kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

"Ahadi ya Tanzania katika kupanua huduma za matunzo na kinga ya VVU kwa wanawake na watoto inatusogeza karibu sana na lengo la kuondoa Ukimwi kwa watoto" anasema Dkt. Bosch

Anasema kuwa wanaamini kupitia makongamano mbalimbali watapata mikakati bora na mbinu sahihi zitakazoungana na jitihada za serikali ya Tanzania katika kutokomeza tatizo hilo.

Aidha anasema kuwa mpango na mkakati wa Taifa wa afya ya jamii na unaoshughulikia (National Health Sector HIV and AIDS strategic Plan) wa mwaka 2008-2012, wenye lengo la kuongeza idadi ya wanawake wenye VVU wanaotumia dawa za kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwao kwenda kwa mtoto kufika angalau asilimia 80 mpaka mwaka 2012.

Anasema shirika hilo limekuwa mstari wa mbele duniani katika mapambano ya VVU na UKIMWI kwa watoto, na limeweza kuwafikia wanawake zaidi ya millioni 14.2 na huduma za kuzuia maambukizi ya VVU kwa watoto.

Shirika hilo linategemea kuendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania na watanzania pamoja na wadau wengine wa masuala ya VVU kwa watoto na kuleta kizazi kisichokuwa na VVU na UKIMWI.

Pia limewezesha maabara 58 inazofanya nazo kazi katika kupima na kutoa majibu ya vipimo husika yenye ubora ili kutambua matizo na maendeleo ya wagonjwa ikiwemo vipimo vya kinga ya mwili.

Pamoja na hayo EGPAF hutekeleza shughuli mbalimbali za utetezi wa sera zinazolenga katika kuleta badiliko katika maisha ya mamilioni ya wanawake, watoto na familia zao ulimwenguni.

Aidha EGPAF linaipongeza wizara ya afya na ustawi wa jamii kwa jitihada zake kubwa katika mapambano yanayolenga kuondoa VVU na UKIMWI kwa watoto.

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Bi.Regina anatoa wito kwa wananchi kuhamasika kuhusu upimaji wa VVU na kuwapeleka watoto wao kupima VVU ili kufaidika na huduma zinazotolewa baada ya kupima.

"Huduma ya upimaji wa VVU hutolewa bure kwenye vituo naomba tutumie fursa hii kujenga tabia ya kupima afya zetu pamoja na watoto wetu na pale inapogundulikana mwananchi yeyote ameathirika aende mapema kwenye vituo vyetu  kupata huduma za ushauri, matunzo na tiba," anasema Bi.Regina.

No comments:

Post a Comment