23 July 2012

Bagamoyo yapata msaada vitabu vya sekondari


Na John Gagarini, Bagamoyo

HALMASHAURI ya Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani, imepata msaada wa vitabu vya kiada na ziada kwa ajili ya shule za sekondari vyenye thamani ya sh. milioni 29 kutoka asasi isiyo ya kiserikali inayosaidia wanafunzi wasichana waishio katika mazingira magumu (CAMFED).

Akikabidhi msaada huo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Meneja miradi wa CAMFED, Bi. Fatina Kiluvia, alisema msaada huo ni sehemu ya mchango wa asasi hiyo kwa ajili ya wasichana waishio katika mazingira magumu ambao wanahitaji msaada wa elimu.

Bi. Kiluvia aliongeza kuwa, CAMFED kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wameanzisha mradi huo ambao ili kuwasaidia wasichana wanaokabiliwa na changamoto.

“Kutokana na kmamati huu, tunategemea kuongeza idadi ya wanafunzi wasichana ili waweze kupata elimu bila vikwazo kwa kuwapa misaada mbalimbali,” alisema Bi. Kiluvia.

Aliongeza kuwa, msaada huo utawanufaisha wanafunzi kutoka wa shule 193 za sekondari katika Wilaya 10 Kilolo, Rufiji, Iringa, Kibaha, Kilombero, Handeni, Pangani, Morogoro na Bagamoyo.

Akipokea msaada huo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Ofisa Elimu Sekondari, Bw. Benjamini Majoya, alisema msaada huo wameupata kwa wakati muafaka na utawasaidia walimu na wanafunzi wa shule zilizo katika mradi huo.

“Msaada huu tumeupata kwa wakati muafaka, ukosefu wa vitabu ni moja ya changamoto kubwa katika shule nyingi za sekondari nchini, nawashauri walimu na wanafunzi wavitunze vitabu hivi ili viweze kuleta manufaa zaidi kielimu,” alisema.

No comments:

Post a Comment