08 June 2012
Wahisani nchini watoa ufumbuzi hospitalini
HOSPITALI ya Wilaya ya Makete mkoani Njombe imepokea msaada wa vifaa afya na tiba vyenye thamani ya sh. milioni 200.5 kutoka Shirika lilisilokuwa la kiserikali la Uboreshaji wa Maisha Vijijini la nchini Uingereza
(TRR).
Shirika hilo lenye wanachama sita ambao ni raia wa nchi hiyo wakishirikiana na Watanzania wazaliwa wa Wilaya ya Makete ambao wanaishi jijini Dare es Salaam mara kwa mara wamekuwa wakifanya shughuli za maendeleo katika wilaya hiyo.
Akikabidhi misaada hiyo mwakilishi wa Wanamakete hao Bi. Sophia Ng'wango alisema, misaada hiyo imetolewa kwa lengo la kusaidia sekta ya afya na kutatua kero mbalimbali ambazo zinaikabili sekta hiyo.
Alisema, Shirika la TRR lilianza shughuli za kuwasaidia watu wa Makete tangu mwaka 2006 ambapo lilitoa fedha ambazo zilisaidia watoto yatima katika Kituo cha Bulongwa, ujenzi wa bweni katika Shule ya Sekondari ya Mwakauta na kununua vitabu katika shule ya Usililo na kwamba kila mwaka tangu mwaka huo shirika limekuwa likitoa fedha kwa ajili ya kusaidia sekta mbalimbali.
Bi. Ng'wango alisema, katika kipindi ambacho wameanza mahusiano na wahisani hao tayari wananchi kadhaa wamenufaika na misaada ambapo hadi sasa kuna maeneo mengi ambayo yamenufaika na msaada huo na kwamba katika sekta za kifedha wametoa misaada ya fedha za kutunisha mfuko katika Saccos ya Bulongwa na Juhudu Saccos.
Alisema, pia Shirika la TRR linajihusisha na utatuzi wa kero ya huduma ya maji katika maeneo mbalimbali na kwamba vijiji vya Iniho, Bulongwa na Unyangogo Serikali ilipelekewa fedha na wananchi hao ili kupeleka huduma ya maji katika maeneo hayo.
Ofisa Tawala wa wilaya hiyo Bw. Joseph Chota aliwashukuru wahisani na kuomba kama kuna fursa nyingine ni vyema waangalie uwezekano wa kusaidia serikali katika ujenzi wa nyumba za watumishi pamoja na kujenga uzio wa hospitali kwani inapungukiwa na vitu mbalimbali muhimu ikiwa ni pamoja na majokofu katika vyumba vya maiti.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete Bi. Imelda Ishuza alisema, ushirikiano unaoonesha na wananchi hao ni mfano wa kuigwa na kwamba serikali inapunguziwa mzigo wa majukumu na kwamba kama wananchi wengi wangelikuwa na moyo wa kujitolea kama hao matatizo katika wilaya hiyo hususan katika sekta mbalimbali yasingekuwepo.
Bi. Ishuza aliwashukuru wahisani hao na kuongeza kuwa serikali inathamini na kujali mchango wao na kwamba itasimamia kwa haki kuhakikisha kila mkilichotolewa kinatumika katika malengo ambayo yalikusudiwa na si vinginevyo.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Bw. Atilio Ng'ondeya kwa niaba ya wananchi aliomba uongozi wa hospitali hiyo kuhakikisha vifaa hivyo vinanufaisha wananchi wa eneo lililokusudiwa na kwamba vitumike kwa matumizi sahihi sawa na malengo yaliyokusudiwa.
ANCHOR
Wananchi kunufaika
na mradi wa umeme
SHIRIKA lisilokuwa la kiserikali la CEFA linalojihusisha na masuala ya kijamii mkoani Njombe limezindua mradi wa kufua nishati ya umeme katika Kijiji cha Ikondo ambao unatarajia kugharimu zaidi ya sh. bilioni 3.5.
Aidha, shirika hilo linafadhiliwa na mashirika ya ulaya na kufanya kazi na kampuni ya CEFA ya mjini Njombe, Kampuni ya Matembwe iliyopo Lupembe wilayani humo.
Shirika hilo lilianzisha mradi wa ufuaji wa umeme zaidi ya miaka 25 iliyopita na kusambaza katika vijiji vya Matembwe, Barazani na Lupembe.
Akitambulisha mradi huo kwa viongozi wa vijiji, kata, tarafa, wilaya na halmashauri katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya hiyo hivi karibuni Meneja Mradi wa shirika hilo Bw. Giacono Spigarelli alisema, mradi wa Ikondo unatarajia kuzalisha nishati ya umeme zaidi ya 'Kw. 240'
ambapo awali ulikuwa unazalisha 'Kw 80' huku matumizi yakiwa makubwa kulinganisha na kiwango kinachozalishwa.
Bw. Spigarelli alisema, wananchi wanaohitaji huduma ya nishati hiyo ni wengi, ambapo mradi uliopo ulianza mwaka 2006 na kwamba mradi unaotambulishwa hivi sasa utanufaisha wananchi katika kata zaidi ya 10 ambapo wananchi wameshiriki kikamilifu katika kuandaa mpango wa kukamilisha madi huo unaotarajia kukamilika miaka minne ijayo.
Kwa upande wake Bw. Johannes Kamonga alisema, CEFA lilianza kushirikiana na MVC baada ya kubaini kuwa wanaweza kuendesha miradi ya umeme kutokana na wao kufanikisha kusimamia mradi wao wa umeme ambao ni wa muda mrefu, na kwamba kazi ya usanifu na mitambo itasimamiwa na MVC.
Alisema, Kampuni ya MVC imekuwa msitari wa mbele katika masuala ya nishati ya umeme kwa kuwa pamoja na kujihusisha na mausuala ya uzalishaji vifaranga, pia wana mradi wa umeme ambao unahudumia vijiji vya Tarafa ya Kata ya Lupembe.
Bw. Kamonga alisisitiza madiwani na viongozi wa vijiji kuhakikisha wanasimamia uandaaji wa miundombinu katika maeneo ya mradi ili mafundi waweza kurahisisha ufikaji katika mradi.
Naye Father Camirro Cariall alisema, kazi ya ubunifu w a miradi ya maendeleo imekuwa ikifanywa na yeye na kwamba kila anachokiona chema machoni pake ni chema kwa jamii, kwa ujumla kwani kazi ya 'umishionari' ni kuangalia matatizo ya wananchi na kuyatatua.
Akizindua mradi huo Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya Bw. Steven Mkalimoto aliwashukuru wahisani na kuomba uharakishaji katika ujenzi wa mradi huo ili wananchi waanze kunufaika na mradi huo.
Alisema, sasa ni jukumu la viongozi kuhakikisha wanashirikiana na wahiisani hao ambao wanakuja kuangaza maisha ya wananchi ambao kimsingi hawana msaada hususan katika masuala ambayo ni nyeti na kuhakikisha nishati hiyo inafika katika, maeneo ya kutolea huduma za afya.
Alisiitiza ushirikiano na wahisani hao na kwamba, yapo amambo ambayo serikali inapaswa kushiriki moja kwa moja katika mradi huo, lakini nguvu za wananchi zitaharakisha kukamilika kwa mradi na kuleta tija.
Katika hafla hiyo fupi ya utambulisho wa mradi, wadau mbalimbali waliudhuria ambapo Diwani wa Kata ya Mtembwe Bw. Shaibu Masasi alisema, wananchi wameshiriki kikamilifu katika masuala ya maandalizi na kwamba ushirikishwaji ni muhimu katika mradi huo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment