08 June 2012
Wafanyabiashara wamlalamikia diwani Kondoa
Na Mwandishi Wetu
WAFANYABIASHARA wa Soko Kuu la wilayani hapa wamemlalamikia Diwani wa Kata ya Kondoa mjini Bw.Hamza Mafita wakidai ameshindwa kuwatetea wafanyabiashara kuhusu ushuru mkubwa wanaolipa.
Wakizungumza katika mkutano wa dharura katika soko hilo, wafanyabiashara hao walidai kuwa wanalipa ushuru wanaponunua bidhaa zao lakini bado wanatozwa wanapoingia sokoni na baadaye wanatozwa tena wanapoingiza mezani.
Wafanyabiashara hao pia walilalamika kuwa bidhaa zinapofika wilaya ya Kondoa watoza ushuru hawazitambui risiti hizo na kulazimisha kulipa ushuru mwingine.
Alisema wafanyabiashara hao hawana sehemu ya kushusha mizigo na hivyo kuwalazimu kushusha nje ambako huongeza gharama nyingine ya kubeba bidhaa hizo kuingiza sokoni.
Bi. Farida Seif alisema aliwahi kugoma kulipa ushuru kwa sababu ya mizigo yake kuibiwa kutokana na ulinzi hafifu hivyo wezi kuingia kwa urahisi na kuiba mali za wafanyabiashara.
Mmoja wa wabeba mizigo sokoni hapo ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema soko hilo linazidi kuharibika kwani linavuja na hakuna milango ya kuingia kwa gari ndani ya soko hilo.
Wafanyabiashara hao waliomba waandishi wa habari kusaidia kuibua kero zinazowakabili wananchi wa wilaya kongwe ya Kondoa ambayo mpaka sasa haina barabara ya lami.
Diwani wa Kondoa Mjini Bw. Mafita alipopigiwa simu kujibu malalamiko hayo alisema hayo si malalamiko ya kweli bali yanatokana na mambo ya kisiasa katika soko hilo wengi ni wafuasi wa Chama cha Wananchi (CUF).
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Bi. Moza Said aliwaahidi wafanyabiashara hao kufutilia malalamiko yao kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kondoa kupata ufumbuzi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment