08 June 2012

Wadhamini: Tuna imani na Taifa Stars



Na Mwandishi Wetu

KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL), ambayo ni mdhamini mkuu wa timu ya Taifa (Taifa Stars) kupitia bia ya Kilimanjaro Premium Lager imesema ina imani na timu hiyo pamoja na kocha wake Kim Poulsen na imeahidi kuedelea kuipa nguvu, ili ifanikiwe zaidi.

Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Meneja wa bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe wakati akitambulishwa rasmi kwa Taifa Stars na nahodha wa timu hiyo Juma Kaseja na Kocha Kim Poulsen na kupata chakula cha mchana na wachezaji.


Kavishe pia aliipongeza timu hiyo kwa kujitahidi wakati wa mechi yao na Ivory Coast Jumamosi iliyopita.

“Nimeelezwa kuwa mlicheza vizuri kwa kujituma na tulikosa nafasi nyingi za kufunga magoli,” alisema Kavishe.

Alisema kampuni yake inaamini huu ni mwanzo na timu hiyo ina nafasi ya kupata matokeo mazuri zaidi katika mechi zijazo, hasa hii ya Jumapili dhidi ya Gambia ya mchujo wa kufuzu kucheza Kombe la Dunia 2014.

“Lazima tuwafanye Watanzania wajione kama sehemu ya timu ya taifa, ili watushangilie wakati tunacheza na ifike wakati walie na sisi tunapolia na wacheke na sisi tunapocheka,” alisema.

Kavishe aliwataka wachezaji wawe karibu na wananchi, ili waweze kujiskia kama sehemu ya timu ya Taifa na kuongeza kuwa Watanzania wana matumaini makubwa na timu yao, hivyo ni jukumu laO kuendelea kuwapa imani na kujituma uwanjani.

Naye kocha Poulsen, aliishukuru TBL kwa udhamini wake mnono kupitia bia ya Kilimanajro Premium Lager na kuongeza kuwa timu haiwezi kuwa imara bila udhamini wa uhakika.

“Kwa sasa tunaweza kufanya mipango ya muda mrefu bila wasiwasi wowote kwa sababu udhamini ni wa uhakika,” alisema.

No comments:

Post a Comment