11 June 2012

Viongozi wanaokwamisha maendeleo wapewa somo


Na David John

VIONGOZI wa Serikali za Mitaa wametakiwa kuwapa hamasa wananchi ambao wanajitolea kufanya shughuli za maendeleo katika jamii inayowazunguka na si kuwavunja moyo.

Mwito huo ulitolewa  Dar es Salaam juzi na wananchi wa Mtaa wa Kingugi, Mbagala Kiburugwa wilayani Temeke baada ya viongozi wa Serikali ya Mtaa huo kusitisha ukarabati wa barabara uliokuwa ukifanywa na wananchi hao kwa kushirikiana na Tawi la Madereva wa Daladala (UWAMADAR) wilayani Temeke.

Akizungumza na gazeti hili hivi karibuni kwa niaba ya wezake,  makazi wa Mtaa wa Kingugi Bw. Athumani TimuTimu, alisema wameshangazwa na viongozi hao kwa hatua ya kusitisha jitihada zinazofanywa na wananchi kwa kushirikiana na UWAMADAR,  Tawi la Zakiem, ambao waliamua kufanya ukarabati wa barabara kwa njia ya kuchangishana fedha ili kurahisisha huduma ya usafiri.

"Barabara hii ya Kingugi kwa muda mrefu imekuwa kero kwa wananchi wa Kiburugwa na mara kwa mara tumekuwa tukiporwa  mali zetu na vibaka kwa sababu ya wananchi kulazimia kushuka kwenye magari na kutembea kwa miguu,"alisema.

Katibu wa UWAMADAR, Bw. Aziz Kamkosa, alisema wao  hawana tatizo, lakini wanaamini walichokuwa wanakifanya ni kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa eneo hilo.

Mwenyekiti wa  Serikali ya Mtaa huo alisema  walisimamishwa ili kufuata utaratibu.

No comments:

Post a Comment