19 June 2012
Semina ya kuogelea yamalizika
Na Amina Athumani
KLABU a kuogelea ya Tanzania Marine Swimming Club (TMSC), jana ilimaliza mafunzo ya kuogelea na kujiokoa kwa watu zaidi ya 50 yaliyofanyika katika fukwe za chuo cha Mwalimu Nyerere, Kigamboni.
Mafunzo hayo ya siku mbili yaliandaliwa na TMSC na kudhaminiwa na Kampuni ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) yakilenga kutoa mbinu za uokoaji, kuogelea na jinsi ya kujiweka katika hali ya kusubiri kuokolewa pindi maafa yanapotokea.
Akizungumza wakati wa kufunga semina hiyo ambayo iliendeshwa kwa nadharia na vitendo Mratibu wa mafunzo hayo, Geofrey Kimimba alisema programu hiyo itakuwa endelevu kwa kuwa ni moja ya malengo ya klabu yake.
Alisema wameamua kuandaa semina hiyo kutokana na ukweli kwamba majanga ya majini yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara, lakini Watanzania wanashindwa jinsi ya kujisaidia pindi majanga hayo yanapotokea.
Kimimba alisema kwa kufanya hivyo itasaidia idadi ya watu wengi kujiokoa ama kuokoa wenzao, pale watakapopatwa na janga la kuzama kwa chombo cha majini ama mafuriko kama yaliyowahi kutokea jijini Dar es Salaam Desemba mwaka jana.
Alisema mikakati ya klabu yake ni kuhakikisha wanatoa mafunzo hayo mara kwa mara, ingawa muitikio wa Watanzania unahitaji zaidi kusukumwa kutokana na watu wengi kushindwa kujitoa hata pale wanapoamua kuendesha mafunzo hayo bila kiingilio.
Mratibu huyo alisema semina hayo ililenga zaidi kuwafundisha Watanzania ambao hawajawahi kuogelea na hawajui jinsi ya kujiokoa na kwamba mafunzo hayo yamefanikiwa kwa kiasi kikubwa, kutokana na washiriki wote kuelewa kwa vitendo walichofunzwa.
TMSC kwa sasa ina waogeleaji 55 tangu kuanzishwa mwaka 2009 ambapo mpaka sasa klabu hiyo imeshiriki michezo mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.
"Tumefanya hivi ili kusaidia kizazi chetu cha Tanzania, ambacho kisingekuwa na uwezo wa kulipia gharama kubwa katika klabu nyingine ambazo zinaonekana asilimia kubwa ya washiriki wake ni wazungu," alisema Kimimba.
Alisema klabu hiyo inatumia bahari katika kutoa mafunzo kwa waogeleaji wake, tofauti na klabu nyingine ambazo zinatumia mabwawa na kwamba waogeleaji wake, ingawa wanatumia bahari wamekuwa wakitoa upinzani mkubwa katika michezo ya ndani na nje ya nchi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment