08 June 2012

Mbunge asononeshwa, tabia za wanafunzi



Na Peter Mwenda, Aliyekuwa Dodoma

MBUNGE wa Viti Maalum (CUF) Mkoa wa Dodoma Bi. Moza Said amedai kusikitishwa kupata taarifa kuwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Ula wilayani hapa Ali Majengo amefungwa jela miaka 20 kwa kosa la kuwalawiti watoto.

Akizungumza na Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Ula Bw. Omari Chuchi hivi karibuni, Mbunge huyo alitaka kujua kabla ya hukumu hiyo shule hiyo ilipokeaje taarifa hiyo wakati kesi ilipokuwa ikiendelea mahakamani.

"Nimesikitika sana kusikia mtoto wenu mmoja amefungwa kwa kosa la kulawiti, acheni kukimbia masomo na kwenda kujificha vichakani mkivuta bangi.

"Hii ni sifa mbaya kwa shule yenu mwanafunzi kukutwa na kosa kubwa kama hilo, mkuu wenu wa shule kaniambia mnatorokea nyumba za jirani na kufanya mambo ya kihuni, nimemwambia apambane na wanafunzi wenye tabia hizo," alisema Mbunge Moza.

Mkuu wa shule hiyo Bw. Chuchi alisema mbali ya wazazi kushindwa kuchangia fedha za kuendesha shule hiyo ada inayolipwa amekuwa akiingia mikataba na vijana waliomaliza kidato cha sita kufundisha shule hiyo.

Wakati huo huo imebainikia kuwa kuzorota kwa elimu katika shule za msingi na sekondari katika Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma hali hiyo imetokana na wanafunzi kushinda njaa wakati wanatumia siku nzima kwenda na kurudi shule.

Wakitoa malalamiko yao kwa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma (CUF) Bi. Moza Said wanafunzi hao, walisema wanaondoka nyumbani saa 10 alfajiri bila kula kitu na wanashinda njaa wanapokuwa shuleni na wakirudi nyumbani saa mbili usiku wanakuwa wamezidiwa na njaa.

Mwalimu wa zamu wa shule ya Msingi Tumbelo Bi. Ramla Omari alisema ni kweli mahudhurio hafifu ya wanafunzi wa shule za msingi katika wilaya ya Kondoa kunatokana na njaa kwani wengi wao wanatoka katika vijiji vya jirani ambavyo havina shule ya msingi.

No comments:

Post a Comment