08 June 2012
Makala mgeni rasmi Redd's Miss Chang'ombe
Na Victor Mkumbo
NAIBU Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Amos Makalla, anatarajia kuwa mgeni rasmi katika mashindano ya kumsaka Redd's Miss Chang'ombe 2012, yanayotarajiwa kufanyika kesho katika Ukumbi wa Quality Center.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mratibu wa mashindano hayo, Teddy Chebby alisema Makala ndiye atakuwa mgeni rasmi ambapo atafuatana na baadhi ya Wabunge wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.
Alisema mashindano mwaka huu, yatakuwa ya aina yake kutokana na maandalizi mazuri waliyoyafanya.
Teddy alisema jumla ya wanyange 14 watawania taji hilo, ambao kila mmoja amejitapa kuondoka na ushindi kutokana na maandalizi waliyoyafanya.
Alisema kuwa mshindi wa kwanza ataondoka na sh. 500,000, wa pili sh. 350,000, wa tatu atapewa sh. 250,000 wakati wa nne na watano wataondoka na sh. 200,000 kila mmoja na waliobakia watapata kifuta jasho cha sh. 100,000.
Mratibu huyo alisema mbali na warembo kujinadi ukumbini, pia kutakuwa na burudani kutoka kwa bendi ya Mapacha Watatu pamoja na msanii wa kizazi kipya, Naseeb Abdul 'Diamond'.
Aliwataja warembo watakaopanda jukwaani kesho kuwa ni Jesca Haule, Wensley Mabula, Frola Robert, Elizabeth Moshi, Latifa Mabewa, Debora Nyakisinda, Like Abraham, Catherine Masumbigana, Flora Kazungu, Clara Diu, Restituta Faustine, Mariam Ntakisuvya na Suzan Paulo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment