12 June 2012

TCRA yaiomba BASATA kuhamasisha wasanii



Darlin Said na Radhia Adam

TAASISI ya Mawasiliano (TCRA), imeliomba Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kuhamasisha wasanii kuongeza na kuboresha vipindi vyao, ili viweze kuleta maendeleo ya nchi katika tasnia ya sanaa na utamaduni.

Ombi hilo limetolwea na Mhandisi Mwandamizi wa masafa TCRA, Joel Chacha katika kongamano lililohusu teknolojia ya dijitali na faida zake kwenye sekta ya sanaa na wasanii, lililowasilishwa kwenye jukwaa la sanaa liliofanyika Dar es Salaam jana.


Chacha alisema katika mabadiliko ya utangazaji kutoka analogi kwenda dijitali sekta ya sanaa na wasanii nchini, watafaidika kwa kutangaza kazi zao za usanii na kuutangaza utamaduni wa Mtanzania ndani na nje ya nchi.

"Kupitia mabadiliko haya ya sanaa, Tanzania itapata soko kwa njia iliyo rahisi na kuwatangaza wasanii nje ya mipaka yetu, pamoja na kuutangaza utamaduni wetu na pia wasanii watapata ajira mbalimbali kutokana na kuongezeka kwa kampuni za sanaa," alisema.

Mbali na faida hizo, baadhi ya wasanii waliohudhuria kongamano hilo wameulalamikia mfumo huo mpya kutokana na changamoto watakazokumbana nazo ikiwemo upoteaji wa kazi zao za filamu na utamaduni wa Mtanzania.

"Kupitia mfumo wa dijitali, ambao unalenga kutumia ving'amuzi itakuwa rahisi kwa mtu wa nje ya nchi kuiba sanaa zetu kwa kunyonya kazi zetu na kwenda kutumia katika nchi zao," alifafanua Surchyang Raphael ambaye ni msanii na Mwenyekiti wa TASA, Ilala.

Naye msanii kutoka kundi la Kashkash, Amos Beda aliulalamikia mfumo huo kwa kusema kwamba mfumo huo ni wa gharama kwa mwananchi wa kawaida kuweza kuumudu katika kununua king'amuzi na kulipia gharama za uendeshaji.

Wakizungumza katika changamoto za mfumo wa dijitali wasanii hao, waliiomba TCRA kusimamia kudhibiti mfumuko wa bei ya ving'amuzi na pia kudhibiti uingiaji wa aina tofauti za ving'amuzi, ili iwe rahisi kwa mwananchi kumiliki king'amuzi kiurahisi zaidi ambacho kitaonesha chaneli zote.

Mfumo wa digitali ulizinduliwa rasmi Agosti mwaka jana na Rais Jakaya Kikwete, ambao ulienda sambamba na uzinduzi wa nembo ya dijitali kwa ambao utekelezaji wake unatarajiwa kuanza rasmi Januari 2013.












No comments:

Post a Comment