14 June 2012

Bajeti 2012/13 kutabiri mengi *Wengi wahofia utekelezwaji wake *Lipumba alia na ugumu wa maisha



Na Godfrida Jola

WAKATI bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2012/13, ikitarajia kusomwa leo mjini Dodoma, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, amesema bajeti ya mwaka 2011/2012 ambayo ilikuwa sh. trilioni 13.5, haijatekelezwa.

Alisema vipaumbele vya bajeti hiyo, vilikuwa na kasoro nyingi pamoja na wafadhili kutotoa fedha walizoahidi.

Prof. Lipumba aliyasema hayo Dar es Salaam jana alipozungumza na Majira kwa njia ya simu juu ya maoni yake kuhusu bajeti iliyopita na inayotajariwa kusomwa leo.

Alisema bajeti iliyopita imeongeza ukali wa maisha ya Watanzania mara mbili zaidi kutokana na ongezeko la matumizi ya ndani.

Aliongeza kuwa, asilimia 39 ya bajeti yote ilikuwa katika sekta ya maendeleo ambayo hadi kufikia Machi mwaka huu, asilimia 32 pekee ndiyo iliyotekelezwa.

“Bajeti ya kesho (leo), maendeleo yametengewa sh. trilioni 4 na bilioni 500 wakati mwaka 2011, ilikuwa trilioni 4 na bilioni 900 hivyo imepungua na haiwezi kufikia wanapotaka, hii inatokana na Serikali kunyimwa fedha na wafadhili,” alisema.

Alisema bajeti hiyo ilishindwa kumaliza tatizo la ajira kwa vijana kwa kutumia sekta binafsi, kufufua viwanda vilivyopo na kuboresha upatikanaji wa nishati ya umeme ili kuongeza uzalishaji viwandani na kuongeza ajira.

“Bajeti ilishindwa kufanikiwa kutokana na utegemezi wa fedha za wafadhili ambao waligoma kutoa fedha na kuipa Serikali wakati ugumu hivyo kuyumba katika matumizi yake.

“Tatizo la msingi Serikali kutokuwa na dira kwa sababu inafuata malengo ya milenia na utekelezaji wa Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (MKUKUTA 2), ambavyo vyote vimepitwa na wakati, muhimu kubuni njia nyingine ili kupiga hatua ya maendeleo,” alisema Prof. Lipumba.

Alisema Waziri wa Fedha kwa sasa, Dkt. William Mgimwa hajapata muda wa kutosha kuipitia bajeti iliyopita na hana utaalamu kuhusu uongozi hivyo hawezi kubaini kasoro zilizopo.

“Dkt. Mgimwa hana utaalamu wa kutosha wa 'fiscal policy', ni mwezi mmoja tu, toka aingie katika Wizara hii, atawezaje kujua kinachoendelea,” alihoji.

Wakati huo huo, Watanzania wengi wamekuwa na shauku ya kutaka kujua vipaumbele vilivyotolewa katika bajeti iliyopita vimefanyiwa kazi kwa kiwango gani.

Bajeti iliyopita, ilitaja mambo manne ya msingi ili kupunguza makali ya maisha na kutenga asilimia 14 ya bajeti yote kwa ajili ya kulipa deni la Taifa.

Mambo hayo ni pamoja na maboresho ya sheria za kodi,  kuongeza nguvu za uwekezaji katika sekta ya umeme, kupunguza bei ya mafuta ya petroli, matumizi ikiwamo ukubwa wa misafara ya safari za viongozi na kuongeza fedha katika sekta tano.

Pia bajeti hiyo ilitoa vipaumbele katika sekta ya miundombinu ya barabara, reli, bandari na mkongo wa mawasiliano wa Taifa ambao ulitengewa sh. bilioni 2,781.4.

Katika mchanganuo huo, nishati na madini ilitengewa sh. bilioni 539.3 ambayo kwa kiasi kidogo imepunguza tatizo la mgawo wa umeme.

Maji ilitengewa sh. bilioni 621.6  bilioni ikilinganishwa na sh. bilioni 397.6 mwaka 2010/11, sawa na ongezeko la asilimia 56, kilimo na umwagiliaji sh. bilioni 926.2 ikilinganishwa na sh. bilioni  903.8 mwaka 2010/11, sawa na ongezeko la asilimia 2.5.

Wakitoa maoni yao kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi walisema wanatarajia kupata unafuu wa ukali wa maisha kwa bajeti ya leo kutokana na hali iliyopo kuzididi kupoteza mwelekeo.

Walisema ni muhimu bajeti ya leo ikaweka vipaumbele ambavyo vitatekelezeka ila kuepuka lawama baada ya kuisha kwa mwaka wa fedha.

“Mwaka 2011 Serikali ilisema itasaidia kuweka mikakati ya kupunguza ukali wa maisha lakini imekuwa tofauti maana maisha yamepanda maradufu na kutuacha njia panda,” alisema Bi. Lenarda Christian, mkazi wa Dar es Salaam.

Alisema bajeti ya leo inatakiwa kuonesha namna ya utekelezaji wa malengo yaliyokusudiwa na pia iendane na mipango ya Serikali ya  ukusanyaji wa mapato na matumizi sahihi ya fedha.

Bw. George Martine, mkazi wa Magomeni alisema kutokana na bei ya mafuta na bidhaa kupanda mara kwa mara, imechangia kuongeza ukali wa maisha kwa wananchi.

Alisema Serikali inapaswa kuwaangalia wananchi wake hasa wa kawaida kwa kupunguza bei za nafaka ili kuwanusuru. “Hivi sasa vyakula vimepanda bei maradufu hivyo kusababisha maisha kuwa magumu,” alisema.

Bei za vyakula zilianza kupanda nchini mwishoni mwa 2011 ambavyo ndiyo hutumiwa na watu wengi ukiwemo mchele, maharage, sukari, unga na viungo vya mboga.

Mchele katika masoko ya Dar es Salaam umepanda na kufikia sh.2,300 hadi 2,500 kwa kilo moja, maharage sh. 2,300, 2,500 hadi 2,600 ambapo awali yalipatikana kwa sh.2,000 hadi Sh. 2,200 kwa kilo, unga umefikia sh. 1,000 hadi Sh.1,200 kwa kilo ambapo bei ya awali ilikuwa 800 hadi sh. 900 kwa kilo.

3 comments:

  1. TUNATAKA MCHUMI ATAKAYECHOCHEA UANDZISHWAJI WA VIWANDA ILI KUONGEZA AJIRA KUZALISHA BIDHAA ZA KUUZWA NDANI ILI FEDHA ZA KIGENI ZIFANYE SHUGHULI ZINGINE,TUNAHITAJI MCHUMI ATAKAYECHOCHEA UPANUZI WA KILMO CHA KUMWAGILIA KUAJIRI VIJANA WENGI WANAOZURURA KWENYE MIJI KAMA MACHINGA NA WAPIGA DEBE WAZKISHE CHAKULA CHA KULISHA WATANZANIA NA KUUZA NJE TANZANIA TUMEKUWA WATU WA NADHARIA VITENDO SIFURI TUJIULIZE CHINA NA UTITIRI ULE WA WATU IMEWEZAJE KUWALISHA NA KUWAVALISHA WATAALAMU CAPITALIST ECONOMY TUACHANE NAO SOCIALIST ECONOMY NAO PIA WAPO HATA MARIKANI INAKOPA CHINA ITATUSHAURI NINI???

    ReplyDelete
  2. Kwanini Serikali isimtumie Prop.Lipumba kusaidie kuinua uchumi wetu ?
    Mh.Lipumba ni Msomi mwenye fani ya Uchumi na Dunia inamfahamu hivyo basi tunaishauri Serikali kumpa nafasi ili aweze kutoa ushauri wake kwa faida ya Nchi yetu

    ReplyDelete
  3. Katika nchi zinazoendelea ni adimu sana kumpata mtaalam mwenye fani ya Uchumi katika ngazi ya PhD.

    Tanzania imejaaiwa kuwa na bahati, miongoni mwao ni Prof. Lipumba ambae aliwahi kuwa msahuri wa mambo ya Uchumi kwa upande wa Uganda na mchango wake ulionekana na kuweka rekodi nzuri nchini humo.

    Jamani katika masuala ya kitaifa kama hili tuitumieni hazina hii ya kichwa cha Uchumi maana hapa hatuangalii anatoka chama gani, mkoa, rangi kabila au etnicity ya mtu.

    Tubadilike.

    ReplyDelete