25 May 2012

Watu wenye ulemavu wasema ya moyoni



Na Florah Temba, Kilimanjaro

JAMII imetakiwa kuondokana na mitazamo potofu juu ya watu wenye ulemavu, pamoja na kuzingatia mahitaji ya watu hao wakati wa ujenzi wa miundombinu ili kuwawezesha kupita kwa urahisi pasipo usumbufu.

Rai hiyo ilitolewa na Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVIWATA) mkoani Kilimanjaro wakati wa mafunzo ya kuvijengea uwezo vyama  vya watu wenye ulemavu Manispaa ya Moshi ambapo walijadili mambo mbalimbali ikiwemo vikwazo na mitazamo hasi iliyojengeka katika jamii juu ya watu wenye ulemavu.

Katibu wa shirikisho hilo mkoani Kilimanjaro Bw. Zacharia Masawe alisema walemavu katika mkoa huo na nchini kote wanakabiliwa na changamoto kubwa ya mtazamo hasi ambapo wamekuwa wakionekana kuwa ni watu ombaomba na watu wasioweza kufanya chochote jambo ambalo si sahihi.

Alisema, mitazamo hiyo katika jamii imekuwa ikisababisha walemavu kudharaulika na kukosa haki zao za kimsingi ikiwemo elimu ambapo hata wakati mwingine hukoseshwa haki ya msingi ya kuishi kwa kuuawa.

“Kumekuwepo na mitazamo hasi katika jamii kuhusiana na sisi watu wenye ulemavu, kwani katika jamii tumekuwa tukionekana kuwa sisi ni watu ombaomba na hata wakati mwingine unakuta unakwenda katika ofisi ya kiongozi ikiwemo za serikali, lakini unapotaka kumuona kiongozi huyo unashangaa unaletewa sh. 500 na kuambiwa uondoke kwa kweli hii ni udhalilishaji na uonevu kwetu sisi,” alisema Bw. Masawe.

Bw. Masawe alisema ufike wakati sasa jamii ibadilike na iwaone walemavu kama watu wengine ambao wanahitaji kuthaminiwa, kuajiriwa na wasiwanyanyapae kwani hakuna mtu aliyezaliwa na kutaka  kuwa mlemavu.

Kwa upande wake Bw. Rumisha Masam alisema walmavu wamekuwa wakikumbana na vikwazo mbalimbali ikiwemo miundombinu mingi kujengwa pasipokuzingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu.

“Jamii kwa saa inapaswa kuthamini watu wenye ulemavu na kuondokana na ile dhana kuwa walemavu ni watu wa kusaidiwa na hawana msaada wowote kwa jamii na sasa ibadilike na iwathamini kwani walemavu ni watu kama watu wengine na wanaweza kufanya kazi endapo wataendelezwa, lakini pia ihakikishe miundombunu yote inayojengwa inazingatia mahitaji yao,”alisema Bw. Rumisha.

Aidha aliongeza kuwa ili kuwawezesha walemavu kuweza kuondokana na hali ya utegemezi katika jamii serikali iweke mpango mkakati maalumu wenye upendeleo chanya ili kupanua soko la ajira kwa watu wenye ulemavu hapa nchini.

No comments:

Post a Comment