09 May 2012
Tanzania yaanza kwa kishindo Kombe la Afrika
Na Amina Athumani
TIMU ya Taifa ya Netiboli (Taifa Queens) imefungua vyema pazia la michuano ya Kombe la Afrika, baada ya kuifunga timu ya Taifa ya Lesotho kwa mabao 57-13 katika mchezo wa ufunguzi uliofanyika jana kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mchezo huo wa ilishuhudiwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mke wa Rais Mama Salma Kikwete, Waziri wa Habari Vijana Utamaduni na Michezo Fenela Mukandala, Mke wa Waziri Mkuu Tunu Pinda pamoja na wake wa Mawaziri, Mabalozi na viongozi mbalimbali.
Katika mchezo huo kikosi cha Taifa Queens kilionekana kuimarika zaidi mwanzo hadi mwisho wa mchezo, huku wachezaji machachari wa Lesotho wakishindwa kuhimili mikikimikiki ya Taifa Queens.
Katika robo ya kwanza ya mchezo huo, Taifa Queens ilikuwa ikiongoza kwa mabao 13-3, robo ya pili ikaongoza kwa mabao 23-9 yaliyoiwezesha Taifa Queens kwenda mapumziko ikiwa kifua mbele kwa jumla ya mabao 36-12.
Taifa Queens iliyokuwa ikiongozwa vyema na mfungaji wake wa kutegemewa Mwanaidi Hassan ambaye pia ni mwanamichezo bora wa mwaka wa tuzo zinazotolewa na Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA), iliingia kipindi cha pili cha mchezo huo kwa kufanya mabadilio kwa kumuingiza mfungaji Pili Peter na kumtoa Mwanaidi.
Katika robo ya tatu Taifa Queens iliendelea kuwapigisha jaramba wachezaji wa Lesotho kwa kuwafunga mabao 40-13 ambapo robo ya mwisho ikaichapa 57 huku Lesotho ikishindwa kufunga hata bao moja na hadi mwisho wa mchezo Taifa Queens ikaibuka kidedea na ushindi huo mkubwa wa mabao 57-13.
Kabla ya mchezo huo Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya michuano hiyo, Mama Tunu Pinda aliahidi kuwapa wachezaji hao sh. milioni moja kila mmoja endapo watahakikisha kombe la Afrika linabaki nyumbani.
Alisema kutokana na lengo la uchangishwaji fedha kwa ajili ya michuano hiyo kuvuka malengo waliyoyaweka fedha zote zitakazobaki mara baada ya kumalizika kwa michuano hiyo watakabidhiwa wachezaji.
Naye Mama Salma Kikwete aliwashukuru wadau wote waliofanikisha kufanyika kwa michuano hiyo mikubwa na kukipongeza Chama Cha Netiboli Tanzania (CHANETA) Kwa kuandaa mashindano hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yataitangaza nchi katika medani ya kimataifa.
Kwa upande wake Waziri wa Habari Vijana, Utamaduni na Michezo Fenela Mukandala alitoa rai kwa CHANETA na vyama vyote vya michezo kuhakikisha vinapanga programu zao vizuri zitakazoweza kuleta maendeleo na tija katika michezo huku akilita Baraza la Michezo Taifa (BMT) kusimamia vyema utekelezaji wake ili vyama vya michezo vilivyopo chini yao visipate tabu dakika za mwisho vinapopata fursa ya mashindano makubwa kama yaliyoweza kuandaliwa na CHANETA.
Michuano hiyo pia imehudhuriwa na Rais wa Shirikisho la Netiboli Afrika, Tebogo Lebotse na Mwakilishi kutoka Shirikisho la Netiboli Duniani (IFNA) Joan Smit.
Mchuano hiyo itaendelea tena leo kwa kuzikutanisha Malawi na Zambia, Botswana na Uganda, Zimbabwe na Lesotho, Tanzania na Malawi na mchezo wa mwisho utakuwa kati ya Uganda na Zimbabwe.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment