08 May 2012
Sijutii kukosa uwaziri-Dkt. Mwanjelwa
Na Charles Mwakipesile, Mbeya
MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Mbeya (CCM), Dkt.Mary Mwanjelwa, amesema hajutii kukosa kuteuliwa katika Baraza jipya la Mawaziri lililoapishwa jana kwa kuwa halikuwa lengo lake la kuwania ubunge na hana mpango wa kuhamia CHADEMA, kama inavyoelezwa.
Alisema uvumi huo unaenezwa na watu aliodai ni wapinzani wake kisiasa mkoani hapa.
Akizungumza na waandishi wa habari akiwa ameongozana na Katibu wa CCM mkoani Mbeya, Bi.Cerena Shumbuso, Katibu wa Itikadi, Siasa na Uenezi, Bw.Bashiru Madodi na viongozi wengine, Dkt.Mwanjelwa alisisitiza kuwa yeye ni kada aliyeivishwa na kuandaliwa na CCM kwa miaka mingi, hivyo hawezi kukurupuka kwenye kutoa maamuzi.
Alisema kamwe hawezi kuhama CCM kwa madai ya kukosa kuteuliwa katika nafasi za uwaziri kwa kuwa makubaliano yake ya kuwania nafasi ya ubunge ni kuwatumikia wananchi wa Mbeya na si kuteuliwa kuwa waziri.
Alisema anafahamu kuwa CCM ina wabunge wengi wasomi na wachapa kazi kama yeye, hivyo ni amri ya mamlaka ya uteuzi kuangalia mbunge yeyote anayeonekana kufaa kuteuliwa bila kuhojiwa wala mtu kuchukia na kuamua kukimbia chama.
"Siwezi kuhama CCM kamwe eti kwa sababu sijateuliwa kuwa waziri, hapana mimi nimefurahi sana wenzangu ndani ya chama kuteuliwa na kuonekana wanafaa tena anayeteua ni rais ambaye ninaamini hakurupuki na uwezo wake ni mkubwa wa kupembua mambo, hivyo siwezi kukosa akili kwa kuhama chama kwa madai ya kuchukia kutoteuliwa,"alisema.
Alisema anaamini kuwa bado anakubalika ndani ya chama hicho hususani Jumuiya ya Umoja wa Wanawake iliyomteua kutokana na imani waliyonayo kwake atagombea tena kupitia kundi la viti maalumu (CCM) mwaka 2015 kwa kuwa anaamini kuwa amefanya mambo makubwa ndani ya jumuia hiyo hadi sasa.
Dkt.Mwanjelwa alisema kuwa atagombea nafasi hiyo baada ya kumaliza kipindi cha miaka mitano ili kuonesha kuwa lengo lake ni kuwatumikia wananchi wa Mbeya.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment