25 May 2012
Elimu kwa vijana mwarobaini kupunguza umashini nchini
Na Stella Aron
NI miaka mingi sasa tangu kupata uhuru, kumekuwa na harakati mbalimbali za kuwawezesha wananchi kutambua ama kushiriki mambo mbalimbali ya kuboresha maisha ya jamii.
Serikali na asasi zisizo za kiserikali zimeshiriki kwa namna moja au nyingine katika kuendesha harakati hizo.
Pamoja na mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika kuhamasisha wananchi, bado kuna mambo mengi ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi zaidi hasa katika kipindi hiki cha utandawazi pamoja na kukabiliana na mfumo wa soko huria.
Bi. Mayrose Majinge ni mwanaharakati mwenye elimu ya juu anazungumzia zaidi kuhusiana na nini Watanzania wanahitaji katika kuboresha na kupatikana kwa maendeleo nchini na hasa katika kipindi hiki cha utandawazi pamoja na kukabiliana na mfumo wa soko huria.
Anasema harakati za kuwahamasisha vijana wajue namna ya kukabiliana na umaskini itasaidia ili kuwawezesha kuendana na utandawazi na kukabiliana na mfumo wa soko huria.
Mwanaharakati huyo anasema kuwa, asilimia kubwa ya watanzania bado wanafikiri kwamba jitihada za kuleta maendeleo ni jukumu la serikali peke yake kwani ni tofauti na mtazamo walionao wananchi wa mataifa mengine yaliyoendelea kwani hilo ni jukumu la kila mtu katika nafasi yake.
Bi. Mayrose anasema, mwananchi ana uhuru wa kuchangia mawazo yake katika kuboresha mipango ya maendeleo bila ya kuvunja sheria za nchi. Anasema kuwa ili mwananchi aweze kuwa huru zaidi sasa imefika wakati wa kila mtu kushiriki vema katika mchakato wa uandaaji wa katiba mpya.
Anasema kuwa kwanza Rais Jakaya Kikwete anapaswa kupongezwa kwa kukubali kubadilishwa kwa katiba na kuunda kwa tume ya watu 30 iliyo chini ya Jaji Joseph Warioba kwa ajili ya kukusanya maoni kwa wananchi kuhusiana na mabadiliko ya Katiba mpya.
Kuundwa kwa tume hiyo kumeleta sura mpya miongoni mwa wananchi kutokana na kilio cha muda mrefu ambapo wengi walikuwa wakilia na baadhi ya vipengele ambavyo inadaiwa kuwa vimepitwa na wakati na vinatakiwa vifanyiwe marekebisho kulingana na wakati tuliopo sasa.
Historia ya Katiba yetu tuliyonayo hivi sasa, inaonyesha kulikuwa na ushirikishwaji hafifu wa wananchi. Hii inaanza kujidhihirisha tangu kupatikana kwa uhuru Katiba ya kwanza iliandikwa na Waingereza na kuikabidhi kwa serikali ambao ni wazalendo jambo ambalo lilionyesha kuwa katiba hiyo ilisheheni mapendekezo ya upande mmoja.
Katiba hiyo ilionyesha dhahiri kumkera Mwalimu Julius Nyerere kutokana na muundo wa uongozi ambapo mwaka 1962 aliifuta na kuiunda upya huku ikionyesha kumpa zaidi yeye madaraka badala ya ile ya awali ambayo watawala wa juu walikuwa ni Waingereza na yeye alikuwa kama ni Waziri Mkuu.
Kwa historia hii inaonyesha kuwa maamuzi hayo yalikuwa ni ya busara lakini hayakuwashirikisha wananchi ambao ndiyo wadau wakuu wa katiba hiyo.
Pia tume maalum ya Katiba iliyoundwa mwaka 1977 chini ya uongozi wa Sheikh Thabit Kombo na Pius Msekwa nayo ilionyesha kutokukidhi matakwa ya wananchi kwa kuwashirikisha vya kutosha katika kuchangia na kutoa maoni yao ya nini wanakihitaji na hawakitaki.
Katiba ya sasa, maana yake ni kwamba sasa tunafungua ukurasa mpya ambapo wananchi watashirikishwa tofauti na Katiba zilizopita ili kuondoa malalamiko na mapungufu yasiyo na lazima ambayo kwa kiasi fulani yamekuwa yakichangia kila kukicha kuibuka kwa mizozo isiyo ya lazima.
Wananchi ndiyo wenye Katiba hivyo wanapaswa kushirikishwa tangu mwanzo wa mchakato hadi mwisho, tukiangalia historia ya nyuma mwaka 1992, Rais mstaafu Ally Hassan Mwinyi aliunda Tume ya kuratibu maoni kuhusu mfumo wa vyama vingi vya siasa, tume hiyo iliyoongozwa na Jaji Francis Nyalali, ilifanya kazi na kutoa matokeo kwamba asilimia 80 ya Watanzania hawataki mfumo wa vyama vingi.
Bi. Mayrose anasema kuwa mbali ya mapungufu yaliyopendekezwa kufanyiwa marekebisho, Serikali ilikubali mfumo wa vyama vingi lakini ikaendelea kuzikumbatia sheria ambazo zinaonyesha zimepitwa na wakati.
Wakati ule pia Rais Mstaafu Benjamin Mkapa naye aliunda Tume ya Jaji Robert Kisanga ya mwaka 1998 ambapo baada ya kukusanya maoni hayakufanyiwakazi na serikali kwa madai kuwa tume hiyo imevuka mpaka.
Pia mwaka 2006 rais Mkapa aliunda Tume ya kuchunguza tatizo la rushwa nchini chini ya Jaji Joseph Sinde Warioba mbali ya mapendekezo ya mchakato mzima ya nini kifanyike ili kukomesha tatizo hilo, mapendekezo hayo hayajashughulikiwa ipasavyo hadi leo rushwa imeota mzizi na inaendelea kulitafuna taifa.
Anasema kuwa ana imani kuwa kwa tume iliyoundwa hivi sasa itakuwa ni kwa ajili ya maslahi ya wananchi na taifa kiujumla hivyo kilichobaki kwa wananchi ni kutoa maoni yao bila ya woga kwani ni kwa faida yao. Na anaamini kwa dhamira aliyonayo Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete atasimamia vema mapendekezo yote yatakayotolewa na Tume ya Katiba.
Mwanaharakati huyo anaendelea kusema kuwa Watanzania wanapaswa kuelewa kuwa rais ndiye mkuu wa nchi hivyo anapaswa kuheshimiwa hata kama atakuwa amemteua mtu mwenye umri mkubwa zaidi yake.
"Huyu anapaswa kuheshimiwa hata kama kuna mtu mwenye umri mkubwa zaidi yake kwani ndiye mwenye mamlaka ya juu zaidi ndani ya nchi yetu,'
Aliongeza "Rais anapaswa kupewa nguvu zaidi na ulinzi kwani ndiye mkuu wa nchi na asije akatokea mtu mwingine akawa mkuu zaidi yake na hiyo ni kwa ajili ya usalama wake ili isifike mahala akawa hana mamlaka ya kutoa maamuzi kwa baadhi ya vitu kwani taifa litakuwa lisilo kuwa na nguvu ya kutosha, " alisema.
Akizungumzia kuhusiana na matumizi ya lugha ya Kiswahili, anasema kuwa sasa ifike mahala kiswahili kitumike kwenye mikutano yote bila ya kujali ni mikutano ya kitaifa.
Anasema kuwa ni bora sasa kukawa na watu maalumu watakaokuwa wakifanyakazi ya kuwafundisha wageni lugha ya kiswahili badala ya kutumika lugha ya kiingereza.
Kutokana na kujali lugha ya kiingereza hivi sasa kwenye mikataba kumekuwa na utumikaji wa lugha ya kiingereza huku lugha yetu ikibaki nyuma kama mapambo.
Mwanaharakati huyo anasema kuwa ana imani kuwa kama Serikali itasimamia suala hilo kwa kushirikiana na Baraza la Kiswahi Tanzania (BAKITA) lugha hiyo inaweza kuendelea zaidi kuwa chimbuko la maendeleo.
Aidha mwanaharakati huyo amewashauri wanawake kujitokeza kwa wingi katika utoaji wa maoni kwenye katiba ili kwenye mapungufu yaweze kurekebishwa na kuwepo kwa uwiano sawa.
Anasema kuwa maendeleo ya taifa hili yanatokana na mwanamke kwani katika familia mwanamke anapokuwa ameyumba kwa asilimia moja kuhusiana na hali ngumu ya maisha basi mwanaume atakuwa na asilimia 2.
Aidha mwanaharakati huyo amewashauri wanaharakati wote nchini watilie mkazo suala la kila Mtanzania kwa nafasi yake kutimiza wajibu wake kikamilifu, kwani kazi ndio msingi wa kupata haki zote kwani itaweza kusaidia kuwakomboa Watanzania ambao baadhi yao wanakabiliwa na hali ngumu na kupatikana kwa maendeleo nchini.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment