07 March 2012

Pinda: Mgomo wa madaktari ni batili

 *Asema haujafuata taratibu, awasihi wasigome
*Akataa kuwafuta kazi Dkt. Mponda, Dkt. Nkya
*Wanaharakati wajitosa, wamtaka akamlilie JK

 Waziri Mkuu Bw.Mizengo Pinda akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana,kuhusu sakata la madaktari nchini.(Picha na Heri Shaaban)

Na Eckland Mwaffisi
WAZIRI Mkuu Bw. Mizengo Pinda, amesema Serikali ipo tayari kukaa meza moja na madaktari ili kufikia muafaka wa madai yao, lakini haiwezi kutekeleza sharti la kuwaondoa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Hadji Mponda na Naibu wake, Dkt. Lucy Nkya,  kwa sharti ambalo limetolewa na Chama cha Madaktari Tanzania (MAT).

Bw. Pinda aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari na kusisitiza kuwa, mambo mengi yaliyopo katika ripoti ya madai yao yanazungumzika ila sharti la kuwaondoa watendaji wakuu wa Wizara hiyo kwa lazima , limevuka mipaka.

Msimamo wa Serikali kuhusu sakata hilo, umetokana na mgomo uliopangwa kuanza leo nchi nzima ambao umetangazwa juzi na MAT kuishinikiza Serikali iwaondoe watendaji hao ili kutoa fursa ya kukaa meza moja kuzungumzia madai yao kwa mujibu wa ripoti.

“Suala la Rais Jakaya Kikwete kupewa saa 72 zinazoisha kesho (leo), awe amewafukuza Dkt. Mponda na Naibbu wake Dkt. Nkya, ili meza ya mazungumzo iweze kuendelea, binafsi siliafiki kabisa.

“MAT inasema sharti hili ni muhimu kutekelezwa na Serikali lakini naamini, hata Rais Kikwete hawezi kuliafiki labda kama wanamadai mengine, nilishatoa ufafanuzi wa jambo hili katika kikao nilichokaa na madaktari wa watumishi wengine wa sekta ya afya pale Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH),” alisema Bw. Pinda.

Alisema taarifa za mgomo huo ambazo zinatolewa na Rais wa MAT, wanazisikia kupitia vyombo vya habari lakini wao kama Serikali, hawajapelekewa barua rasmi wala jamii (Watanzania), haifahamu ukweli wa jambo hilo juu ya hatua ambazo zimefanywa na Serikali yao kuzuia mgomo huo usijirudie.

“Wito wangu kwa madaktari na watumishi wengine wa sekta ya afya, naomba wasifanye mgomo waendelee na kazi, migomo
 inasababisha kutoweka kwa utulivu, maelewano, amani hata kupoteza maisha ya wananchi wasio na hatia.

“Migomo inapunguza tija na uzalishaji, kuzorotesha ustawi na ukuaji wa uchumi Kitaifa ambapo kutokana na ukweli huo, ndiyo maana sheria za kazi zimeweka mifumo na taratibu za kutatua migomo ya kikazi kabla haijaanza,” alisema.

Alisema kwa kuzingatia masharti ya Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini namba 6/2004,  mgomo wa awali uliofanyika Januari-Februari mwaka huu, haukuwa halali Kisheria na ule unaotarajiwa kuanza kesho, nao si halali kisheria kwani haujazingatia masharti yaliyotajwa katika Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini.

Aliongeza kuwa, licha ya madaktari kutofuata taratibu za Kisheria, Serikali muda wote ilikuwa sikivu ikiwa na imani kubwa ya kumaliza mgogoro ambao ulikuwa katika mazungumzo.

Bw. Pinda alisema, Serikali inaamini madaktari watasitisha mgomo ili kunusuru maisha ya Watanzania wasioa na hatia ila kama wataendelea na msimamo wao, watachukua hatua za kutafuta madaktari wa ziada ili kuziba nafasi zao.

“Pia tutaangalia sheria inasemaje juu ya watumishi walio katika idara nyeti kufanya mgomo usio halali na kuumiza wananchi wasio na hatia, kwa mujibu wa kifungu cha 80 (1), cha Sheria ya Mahusiano Kazini namba 6/2004, mgomo halali ni ule unaohusu maslahi, ulioitishwa na Chama cha Wafanyakazi na umeungwa mkono na wanachama wengi kwa kupigiwa kura.

“Mgomo ulioitishwa na madaktari, haujawahi kuwasilishwa katika tume niliyounda ya watu 12 kutoka idara mbalimbali ambao ndiyo walipitia madai yao kwa ajili ya usuluhishi na haujaitishwa na chama kilichosajiliwa kwa mujibu wa sheria husika,” alisema.

Aliongeza kuwa, Machi mosi mwaka huu, tume aliyounda ilikuwa ikitane na madaktari na wawakilishi wa idara nyingine za afya ambao nao walikuwa na madai mbalimbali.

Alisema taarifa alizopewa, madaktari hao walikataa kujumuishwa na watumishi wa kada nyingine za afya ambao wanafanya kazi pamoja kama wafamasia, wauguzi, wanasayansi wa maabara za afya, wafiziotherapia na wataalamu wa mionzi kwa sababu wakiwa pamoja madai yao hayatapewa uzito unaostahili.

Baada ya serikali kuona si jambo zuri kuwatenda watumishi wa kada nyingine za afya, madaktari walitoka nje ya ukumbi ambapo makundi mengine yaliyobaki, nayo yalikataa kuendelea na majadiliano bila kuwepo madaktari.


“Hawa madaktari waliandika barua nyingine kuomba majadiliano yafanywe kati yao na Serikali, tuliwasikiliza na kupanga tukutane Machi 2 mwaka huu, baada ya kufika ukumbini, walikuja na sharti jingine la kuilazimisha Serikali itekeleze sharti la kuwaondoa Dkt. Nkya na Dkt. Mponda ndipo majadiliano yaendelee.

“Sharti hili lilikuwa ni nje ya madai waliyowasilisha kwa maandishi, viongozi wa MAT walikwenda kufanya mkutano wao wa Machi 3 mwaka huu na kufanya maamuzi kupitia vyombo vya habari kwamba Serikali itimize sharti la kuwaondoa viongozi wa kisiasa na kutoa saa 72,” alisema Bw. Pinda.

Mwandishi Goodluck Hongo anaripoti kuwa, wakati Serikali ikiwasihi madaktari wasitishe mgomo, wanaharakati wameitaka Serikali iwafukuze kazi Dkt. Mponda na Dkt,. Nkya ifikapo leo.

Walisema kufukuzwa kwa watendaji hao ni sehemu ya kutekeleza madai ya madaktari vinginevyo watawahamasisha wananchi waandamane nchi nzima.

Tamko la wanaharakati hao limetolewa Dar es Salam jana katika mkutano wao na waandishi wa habari kuelezea hatua ambazo watachukua kama mgomo huo utaanza leo.

Walisema kama Serikali na Rais Jakaya Kikwete angekuwa na nia ya dhati kutetea maisha ya Watanzania, angechukua hatua za haraka kuzuia mgomo huo ambao unaweza kusababisha maafa makubwa.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Bi. Lilian Liundi, alisema wao kama wanaharakati hawataki kuona mgomo mwingine ukitokea.

“Kama kweli Rais Kikwete na Serikali yake wangekuwa na dhamira ya kutekeleza madai ya madaktari, mgomo usingekuwepo lakini yupo kimya,” alisema Bi. Liundi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamuc (LHRC), Dkt. Hellen Kijo-Bisimba, alimshukia Bw. Pinda kwa kushindwa kuchukua hatua za kuzuia mgomo huo badala yake amebaki kusikitika.

“Waziri Mkuu anapenda kulia, tunamtaka achukue hatua sio kusikitika, kama anataka kuendelea kulia aende kwa rais na kugalagala ili hatua za haraka kumaliza mgomo ziweze kuchukuliwa kwani maisha ya Watanzania wenzetu yanapotea kwa kukosa huduma za matibabu,” Dkt. Bisimba.

Aliongeza kuwa, wananchi wanataka kuiona Serikali yao ikitekeleza madaia ya madaktari pamoja na kuwafukuza kazi watendaji wakuu katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushindwa kujiuzulu wenyewe.

Alisema mbali na kuwafukuza, mazingira ya kazi nayo yanapaswa kuboreshwa haraka iwezekanavyo na kama Serikali haitatimiza mambo hayo kuanzia leo, watawashawishi Watanzania kuchukua hatua.

“'Tunawasihi Watanzania wote wanaojali utu wawe tayari kuinuka kuchukua hatua itakayoifanya Serikali kutimiza wajibu wake ili kuzuia wananchi wasipoteze maisha,” alisema.

Naye Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) Bi. Ananilea Inkya, alisema haki ya kuishi ni ya kila Mtanzania na kama kitatokea kifo kwa ajili ya mgomo, anayetakiwa kuwajibika ni kiongozi kwa kujiuzulu.

“Rais mstaafu wa Aweamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi, alijuzulu wakati akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi baada ya kutokea maafa Shinyanga sasa hawa watendaji nao watumia busara kujizulu wenyewe bila kushinikizwa na rais,” alisema.



4 comments:

  1. Jamani mbona waziri haeleweki? wakati wa makubaliano ya awali alidai baada ya kuwasimamisha kazi K/mkuu na mganga mkuu wa serikali alisema kitakachofuata kwa waziri na naibu wake wote wanakijua sasa iweje adai haiwezekani? hivi bora lipi watu kufa ili hao wateule wao wabaki madarakani au kujiuzulu watu wapone!Isitoshe waziri mkuu amekuwa mtu kulialia tu hakuna utekelezaji kwa nini?hii inadhihirisha kuwa wapo kimaslahi zaidi na wala siyo kuwatumikia wananchi.Nami naungana na wanaharakati kufanya maandamano nchi nzima kuishinikiza serikali pamoja na mambo mengine kuwafuta kazi na kuvunja baraza la mawaziri kwani limeshindwa kumshauri rais vizuri.

    Haya shime watanzania tuamke kutoka usingizini.

    ReplyDelete
    Replies
    1. kujiuzulu sio suluhisho la matatizo ya madactari. walidai maslah yao yanashughulikiwa, wakijiuzulu hawa watazua jingine. Pinda fanya kama Kenya.

      Delete
  2. wazirimkuu kawa msanii iweje awali kukubaliana na madaktari kutatua matatizo yao kwa muda muhafaka kisha hadi kufika tarehe husika hakuna kilichofanyika huu si utawalabora.Dk. mponda na Nkya wana thamani ipi kitaifa hadi kupelekea kuhatarisha roho za mamilioni ya watanzania wanaohitaji msaada wa madaktari kwa kukumbatia watuhumiwa katika sekta ya afya .kuakumbatia inadhihilisha kua wote wana nufaika na yanayo endelea nyuma ya pazia katika sekta ya afya.

    ReplyDelete
  3. Hivi watanzania wenzangu mmesahau kama viongozi wetu wasanii na kwanini wankuwa wasanii kwasababu hatuwa haichukuliwi kusikiliza madai ya wananchi au maslahi ya wannchi kwasasbabu nyie wanapokujieni na ahadi au kukemea upinzani na kusema hawotowza kufanya waliyoyaahidi kwa masual ya kuwa pesa watatoa wapi pesa za kupeana posho na marupurupu au kila siku jkuongeza majimbo mapya ya uchaguzi zinatoka wapi? Mabwana wenzangu andamaneni hata kwa kutundika mabao kuwasapoti wataalamu wetu wa taaluma ya afya zetu imebakie MMungu siku ikifika haina cha daktari mzuri wala zana za kutosha lakini kwa kweli vifo vyingi vinasababishwa na kukosa zana za kutendea kazi ambavyo serikali zetu kama ni makini waache msururu wa masherehe na masafari watumie rasilmali vizuri waone kama daktari atagoma na akigoma itakuwa nae ni mbinafsi kama hao viongozi wetu .

    ReplyDelete