HAKUNA jambo lisilo na mwisho, ndivyo ninavyoweza kusema baada ya mgomo wa madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), kuhitimishwa jana na Waziri Mkuu, Bw.Mizengo Pinda.
Tangu kuanza kwa mgomo huo, Serikali imebebeshwa lawama za kila aina kutokana na vifo vya Watanzania wasio na hatia hasa wa kipato cha chini.
Kimsingi hali ya matibabu katika Hospitali ya Muhimbili ilikuwa ya kusikitisha na kuhuzunisha ambapo jana, Bw.Pinda kwa niaba ya Serikali, aliomba kukutana na madaktari pamoja na wauguzi ili kusikiliza kilio chao na kufikia mwafaka.
Madaktari na wauguzi hawakusita kueleza kilio chao katika mkutano huo na kuitaka Serikali, iwaondoe Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt.Hadji Mponda, Naibu wake Dkt.Lucy Nkya, Katibu Mkuu, Bi.Blandina Nyoni na Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt.Deo Mtasiwa kutokana na imani ndogo waliyonayo kwa viongozi hao.
Pia madaktari hao waliitaka Serikali isikilize madai yao ya msingi ili waweze kurudi kazini kuendelea na kazi ya kuokoa maisha ya Watanzania ambao wanahitaji matibabu.
Kutokana na maombi hayo, Serikali ilitoa tamko la kuwasimamisha kazi kwa muda usiojulikana, Bi.Nyoni na Dkt.Mtasiwa ili kupisha uchunguzi wa madai mbalimbali yaliyotolewa dhidi yao.
Bw.Pinda aliongeza kuwa, Dkt.Mponda na Dkt.Nkya, nao watachunguzwa kama wenzao lakini wataendelea na kazi kutokana na kofia waliyonayo kisiasa.
Sisi tunasema kuwa, kilichofanywa na Serikali kumaliza mgogoro huo ni hatua muhimu ya kuokoa maisha ya Watanzania hasa maskini ambao wanahitaji matibabu lakini wameyakosa kwa wiki kadhaa.
Jambo la msingi ni kuhakikisha kile kilichoafikiwa katika mkutano huo, kinafanyiwa kazi kwa muda waliokubaliana ili kuzuia maafa na mgomo kama huo usitokee tena.
Imani yetu ni kwamba, madaktari wote ambao mlikuwa kwenye mgomo, leo mtaingia kazini na kutoa huduma kwa upendo kama ilivyokuwa awali wakati Serikali ikishughulikia madai yenu.
Tamko la Serikali kuwa haitamchukulia hatua daktari yeyote aliyehusika na mgomo huo, liwe la kweli kwani kama itabainika kauli hiyo haina ukweli, upo uwezekano wa kutokea mgogoro mwingine unaoweza kuharibu sifa ya nchi yetu.
No comments:
Post a Comment