20 January 2012

TBL yatoa pamba Yanga, Simba SC

Na Zahoro Mlanzi

KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL) kupitia Bia yao ya Kilimajnaro Lager
, imekabidhi vifaa mbalimbali kwa timu za Yanga na Simba kwa ajili ya mechi zao za mzunguko wa Pili wa Ligi Kuu Bara vyenye thamani ya sh. milioni 70.
Ligi hiyo inatarajiwa kuanza Jumamosi ambapo Yanga itaanza na Moro United Uwanja wa Taifa, Dar es Salam na Simba itashuka uwanjani Jumatano kucheza na Coastal Union ya Tanga.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo Dar es Salam jana, Meneja wa Bia hiyo, George Kavishe alisema hiyo ni mara ya pili kwa kutoa vifaa vipya tangu waingie mkataba mpya kwa timu hizo wa miaka mitano Agosti, mwaka jana.
"Tumetoa vifaa hivyo tukiwa tunatekeleza moja ya makubaliano yetu kayika mkataba tulioingia na pia tuna uhakika vifaa hivi vitatoa motisha kwa timu hizi kufanya vizuri zaidi katika mechi zao," alisema Kavishe.
Alisema mbali na hilo, pia Yanga ilipata sh. milioni 25 kutokana na kuwa bingwa na Simba ilipata sh. milioni 15 baada ya kushika nafasi ya pili na kwamba wataendelea kutekeleza yale yanayopaswa kufanywa katika mkataba walioingia.
Alivitaja badhi ya vifaa walivyotoa kwa kila timu ni jezi, mipira, vizuia ugoko, jezi za kipa, viatu vya mazoezi, mechi na nguo zake na nguo za viongozi ambapo kila timu ilikabidhiwa vifaa vyenye thamani ya sh. milioni 35.
Nao Makatibu Wakuu wa timu hizo, Evodius Mtawala wa Simba na Selestine Mwesigwa wa Yanga, waliishukuru kampuni hiyo na kuahidi watavifanyia kazi kama inavyotakiwa na kuahidi kutekeleza yale wanayopaswa kutekeleza katika makubaliano yao.
Mbali na hilo, aliulizwa kuhusu madai yaliyotolewa kuhusu uchelewaji wa mishahara kwa timu hizo, Kavishe alisema kampuni yao haiwezi kumaliza matatizo yote waliyokuwa nayo timu hizo, ila wanachofanya ni kutatua baadhi ya matatizo.
Alisema kwa kawaida hutoa mishahara kwa timu hizo kila tarehe 28 ya kila mwezi na kam ikichelewa hufika mpaka tarehe 3, sasa kama wachezaji wanakuwa hawapati hizo fedha ni suala la uongozi wa timu na si la kwao.
"Sisi tunachodai ni ripoti ya jinsi walivyowalipa mishara wachezaji hao zikiwa na sahihi zao, sasa kama kutakuwa na kitu kingine kinajitokeza ni ngumu kujua kwani timu hizo zina watawala wao," alisema Kavishe.

No comments:

Post a Comment