19 January 2012

'Soko linaharibika watendaji acheni tabia ya kukaa ofisini'

Na Theresia Victor, Dodoma

 UMOJA wa Wafanyabiashara wa Soko la Sabasaba lililopo katika Manispaa ya Dodoma
wamewataka watendaji wa idara ya afya katika halmashauri hiyo kuacha tabia ya kukaa ofisini, kusubiri taarifa za kuletewa na badala yake wafike katika maeneo husika ili kijionea hali halisi ya uchafu uliokithiri katika maeneo ya masoko.
Akizungumza na Majira jana sokoni hapo Katibu Msaidizi wa soko hilo, Bw.Gelgod Lugusi alisema, soko hilo lipo katika hatari kutokea kwa magonjwa ya mlipuko hasa kipindupindu kutokana na kulundikwa kwa uchafu wa muda mrefu bila kuzolewa.
Bw.Lugazi alisema, wafanyabiashara wa soko hilo waliamua kutoa ushauri huo kutokana na soko hilo kugeuzwa kuwa dampo la kutupia taka taka na kusababisha baadhi wafanyabiashara wenye vibanda kufunga kwa kuhofia kutokea kwa magonjwa ya mlipuko.
Alisema, pamoja na kutoa taarifa mara kwa mara katika ofisi za Idara ya Afya lakini bado watendaji hao huwa hawafiki kwenye maeneo husika na kujionea hali halisi ya uchafu wa takataka ulivyozagaa kwenye soko hilo.
“Tunashindwa kuwaelewa hao watendaji wa Idara ya Afya, kwa kukaa kwao muda mwingi ofisini na kusubiri taarifa za kuletewa, sasa sijuhi hawana vitendea kazi au ahadi wanazotoa zipo katika mtazamo wa kisiasa kwani sisi tunatoa ushuru lakini hatuoni utekelezaji wao,” alisema Bw.Lugusi.
Akizungumza na majira mmoja wa Maofisa wa Idara ya Afya wa manispaa hiyo ambaye hakutaka jina lake kutajwa gazetini kwa madai kuwa yeye siyo msemaji mkuu wa halmashauri hiyo, alikiri kuwepo kwa mlundikano wa taka hizo kwa ufafanuzi kuwa suala la vitendea kazi hususani magari ya kuzolea taka ndani ya manispaa hiyo ni kikwazo.
Ofisa huyo alisema, amna magari ya kusombea taka na yaliyopo kwa hivi sasa ni mabovu huku akidai yapo gereji kwa ajili ya matengenezo.
"Hata hivyo kinachofanyika kwa sasa ni kuona jinsi gani tutakavyokodisha matrekta kwa ajili ya kusombea takataka hizo ili kuondoa kero hiyo," alidai.

No comments:

Post a Comment